SITTA AONYESHA KUJIKANYAGA KUJIBU SHUTUMA ZA DK. SLAA
Samweli Sitta akizungumza na waandishi wa Habari. |
SIKU
moja baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa kumrushia kombora zito Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Hamis
Mgeja amemtaka waziri huyo na wabunge wengine 55 wapime, watafakari na hatimaye
wachukue hatua kwa kuondoka ndani ya CCM.
Mgeja
ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, amesema tuhuma zilizotolewa
na Dk. Slaa dhidi ya Sitta na wabunge hao, zinathibitisha jinsi kiongozi huyo
na wenzake walivyo wasaliti ndani ya chama chao na serikali, na kwamba kitendo
cha kuigeuza ofisi ya spika kuwa kijiwe cha kupanga uhaini na usaliti ndani ya
CCM hakivumiliki hata kidogo.
Mgeja
alitoa kauli hiyo jana jijini Mwanza, alipozungumza na waandishi wa habari kwa
lengo la kumpongeza Dk. Slaa kwa kufichua uozo wa Waziri Sitta na wenzake hao.
Alisema Dk. Slaa ameisaidia CCM kutambua viongozi wake wanaokisaliti.
"Nianze
kwa kumpongeza Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa kwa kufichua madhambi ya Samuel
Sitta. Huyu mtu (Sitta), ni hatari sana katika maendeleo ya chama chetu.
"Dk.
Slaa ametueleza jinsi Sitta alivyotumia ofisi ya spika kama kijiwe cha kutaka
kukisaliti chama chetu na kuanzisha CCJ. Huyu mtu ni hatari sana... tunaomba
CCM imtose yeye na wabunge hao 55 maana uroho wao wa madaraka unaweza
kuigharimu CCM.
Mjumbe
huyo wa NEC na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga aliyejipambanua kupiga vita
ufisadi na vitendo viovu ndani na nje ya CCM, alisema historia ya Waziri Sitta
inajionesha wazi kwamba ni 'mkorofi na msaliti mkubwa', kwani mwaka 1966 akiwa
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alishiriki maandamano hadi Ikulu
kupinga sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Alisema
katika harakati zao hizo za kupinga sheria hiyo iliyotaka kila mwanafunzi wa
Chuo Kikuu lazima ajiunge na Jeshi la Kujenga Taifa, Baba wa Taifa wakati huo
akiwa Rais wa nchi na mkuu wa chuo hicho, alilazimika kumchapa viboko Sitta
kutokana na usaliti wake huo kwa serikali.
Mgeja
alisema mbali na kufanya maandamano hayo, Sitta na wenzake ambao wengine ni
marehemu kwa sasa walikuwa na mabango yenye ujumbe mkali kwa serikali, ukiwemo
uliosema 'Onyo kali na la mwisho kwa serikali', na kwamba alikuwa akiipinga pia
Serikali ya Baba wa Taifa huku akiusifu uongozi wa kikoloni.
"Huyu
Sitta ambaye leo hii anawadanganya watu, kipindi hicho akisoma Chuo Kikuu alikuwa
akiipinga serikali na kudai afadhali serikali ya kikoloni. Tusipoamini leo
usaliti wake huu tunasubiri hadi aje shetani atuambie usaliti wa Sitta ndipo
tuamini?
"Za
mwizi ni 40, ndiyo maana tumeambiwa toka mwaka 2005 hadi 2010 huyu Sitta
amekuwa akikisaliti chama chetu kupitia Bunge alilokuwa akiliongoza. Tunataka
chama kimtose na kisiwaonee haya wasaliti hawa wakubwa. Wasipoondoka kwa hiari
yao wataondolewa kwa nguvu ya wanachama wa CCM,” alisema.
Alimtuhumu
pia Waziri Sitta kwa kauli zake za kulalamikia serikali bila kutafuta ufumbuzi
wa matatizo yanayolikumba taifa, na alimtaka ataje jinsi alivyoisaidia serikali
kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, mfumuko wa bei, ufisadi na mambo mengine
ndani ya chama na serikali.
Kwa
mujibu wa Mgeja anayedaiwa kuanza kuundiwa mbinu chafu za kutaka kuangushwa
katika kinyang'anyiro cha uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga na kundi la kigogo
mmoja anayetajwa kutaka kugombea urais mwaka 2010, tuhuma hizo dhidi ya Waziri
Sitta zimekisaidia maradufu chama, kwani siyo Dk. Slaa pekee aliyewahi
kumshutumu kiongozi huyo kwa usaliti ndani ya chama.
Alisema
yupo tayari kusulubiwa, kutolewa kafara au kufukuzwa na chama kwa kusema ukweli
daima, kwani anayasema hayo kwa kufuata kiapo cha katiba ya CCM.
Sitta amjibu Dk. Slaa
Waziri
Sitta amemjibu Dk. Slaa akimwita dikteta na asiye na uvumilivu na kwamba ana
hulka ya kujisikia kuwa mawazo yake hayapingwi.
Waziri
Sitta amemwita Dk. Slaa kuwa ni mzushi, asiyeogopa kusema na kupindisha mantiki
ya jambo ili tu kushinda hoja.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, Sitta alisema amesikitishwa
na kauli hizo za Dk. Slaa alizoziita za jazba na mwangwi wa kiwewe alipokuwa
Iringa juzi hadi akafikia hatua ya kumwita mnafiki, mwongo, mtu wa hatari n.k
“Hali
hii inatia shaka juu ya uwezo wa kiongozi huyo wa kisiasa kuhimili kukosolewa
ambayo ni sifa muhimu ya maisha ya mwanasiasa yeyote hususani anapojinadi kuwa
anaweza kuchukua madaraka ya kuiongoza nchi.
“Iweje
mtu aliyenibembeleza nigombee urais kupitia chama chake mwaka juzi leo aseme
sifai kuongoza hata kata kwa sababu tu nimetamka ukweli juu ya udhaifu wa chama
chake cha siasa?” alihoji Sitta.
Alieleza
kuwa aliyoyasema Karagwe majuzi katika uchambuzi wake wa vyama vya siasa nchini
ni kwamba CHADEMA wamekuwa hodari wa kukosoa na kuishambulia CCM na serikali
zake lakini wanasahau kuwa ili wawe mbadala kwa kuiongoza nchi hawana budi
kurutubisha safu yao ya uongozi na uwe na watu wa kutosha kuweza kushika
madaraka ya ngazi mbalimbali.
“Kuukataa
ukweli kwamba safu ya uongozi wa CHADEMA ni nyembamba ni kujidanganya tu.
Kupita mikoani kutangaza kwamba matatizo yote ya wananchi yanatokana na CCM ni
kazi rahisi na ina mvuto wake kisiasa, lakini mwanasiasa makini hana budi
kwenda mbele zaidi ya hapo,” alisema Sitta katika taarifa yake.
Alimtaka
Dk. Slaa kueleza wapiga kura mipango ya chama chake inayoeleweka na
inayotekelezeka na iliyo makini kukabiliana na changamoto mbalimbali za
maendeleo ya nchi.
Amgwaya Mbowe
Kuhusu
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Sitta alionyesha kumgwaya akieleza kuwa
katika hotuba yake hakukejeli uzoefu wa kiongozi huyo wala hakusema ni mcheza
disko.
“Niliuchambua
wasifu wa viongozi wa CHADEMA na kutamka uzoefu wa Mhe Mbowe katika vitega
uchumi vya burudani, hii siyo kudharau bali ni kutamka ukweli tu.
“Huwezi
kuuelezea wasifu wa Mhe Mbowe bila kuelezea mchango wake mkubwa katika tasnia
ya burudani,” alisema.
Alieleza
kuwa mmoja wa marais maarufu wa Marekani, Ronald Reagan, alikuwa ni mcheza
sinema. Na hapa Tanzania kulikuwa na Rashidi Kawawa (sasa marehemu) ambaye
alianzia katika tasnia ya uigizaji hivyo Mbowe au Dk. Slaa wanaweza wakawa
marais wa nchi kwa maana ya kupigiwa kura za uchaguzi wa demokrasia.
“Kumudu
au kutoyamudu madaraka hayo ni suala tofauti. Tathmini yangu ilihusu safu nzima
ya uongozi wa CHADEMA kwa ujumla wao. Ni safu nyembamba mno,” alisema Sitta.
Kujiunga na CHADEMA
Kuhusu
suala hilo, alisema CHADEMA walifanya jitihada ya kumshawishi aingie kwenye
chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 na ili awe mgombea wao wa urais.
“Jambo
hili nililitafakari na kutafuta ushauri kwa watu wangu wa karibu na nikabaini
kwamba; CHADEMA wana migawanyiko yao ya uongozi tena ni ya hatari kwa sababu ni
ya kikanda za nchi – yaani nani anatoka wapi.
“Kutokana
na yaliyomo katika ilani yao ya uchaguzi 2010 – 2015 nilibaini mambo ya
kiitikadi ambayo siyakubali kama vile sera ya majimbo,” alisema Waziri Sitta.
Alisema
sera ya majimbo inawezekana katika nchi ambazo ni tajiri na pia isiyo na
tofauti kubwa ya hali ya maisha baina ya kanda mbalimbali za nchi kama vile
Marekani.
Sitta
alisema kuleta majimbo Tanzania ambako kuna tofauti kubwa za kimaendeleo baina
ya Kaskazini, Mashariki, Kati, Kusini na Magharibi ni kusababisha nchi ichanike
vipande vipande.
Kuhusu CCJ
Alisema
kama ilivyo kawaida kwa vyama vya siasa kutafuta wagombea bora, CCJ ni miongoni
mwa vyama vilivyomtafuta na baadhi ya wanasiasa wengine wakati wa maandilizi ya
uchaguzi mkuu.
“Jambo
hili si la siri wala la ajabu na nimelizungumza hili mara nyingi. Isitokee
katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mtu kutoka chama kumoja cha siasa na
kujiunga na chama kingine haiwezi kusemwa kuwa ni uhaini,” alisema Sitta.
Alisema
kama angeridhika na mambo yao angejiunga na CCJ mwaka 2010 lakini hakufanya
hivyo.
Alieleza
kuwa ni uzushi usio na msingi kumuhusisha na uanzishaji wa chama hicho kwani
waanzilishi wa chama hicho cha siasa wanajulikana na wapo hai lakini alieleza
kuwa ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania kuanzisha au kujiunga Binafsi na
chama chochote cha siasa. Hata hivyo mmoja wa waanzilishi wa CCJ, Fred Mpendazoe,
alimtaja Sitta kama mwasisi mwenzake ambaye hakutaka kujitokeza hadharani kabla
chama hakijapewa usajili wa kudumu.
Kuhusu
madai yake ya kutamka kwamba angehamia CHADEMA na wabunge wa CCM 55 alisema
hizo ni porojo za Dk. Slaa kama ulivyo usemi ‘ningeihama CCM siku chache kabla
ya kuvunjwa Bunge la 9’.
No comments:
Post a Comment