To Chat with me click here

Thursday, September 13, 2012

MADIWANI MWANZA WAMTUHUMU WENJE KWA USALITI

BAADHI ya madiwani na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamesema Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, ndiye msaliti na mvurugaji namba moja wa chama hicho.

Wakizungumza na vyanzo vya habari hii mjini hapa jana, madiwani hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini, walisema Wenje amekuwa akitaka kuabudiwa ndani ya chama hicho na amekuwa akiitumia nafasi yake ya ujumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA kunyanyasa viongozi, madiwani na wanachama wanaompinga.

Walisema kitendo cha Kamati Kuu ya CHADEMA kuwafukuza madiwani wawili ni kukurupuka na tayari wameungana pamoja na kumtangaza Wenje kama janga ndani ya chama hicho na wanatarajia kuandaa mkutano mkubwa kwa ajili ya kuwaeleza ukweli wanachama wa Mkoa wa Mwanza.

Madiwani hao walisema Wenje amekuwa akiweka mtandao wa viongozi ndani ya CHADEMA kwa ajili ya kujiweka sawa kwa ajili ya kuwania nafasi ya uenyekiti wa mkoa na viongozi na wanachama wanaompinga amekuwa akiwazushia uasi na kutimuliwa ndani ya chama hicho.

Walisema mbunge huyo anadaiwa kupanga safu ya meya na naibu meya wa Nyamagana na Manispaa ya Ilemela.

Walisema kufukuzwa kwa Diwani wa Kitangili, Henry Matata na Diwani wa Igoma, Adamu Chagulani ni mwendelezo wa Wenje kuwatimua kwa kutumia ushawishi wake katika vikao vya uamuzi.

“Kuna kiongozi wa vijana, Robert Gwanchele, huyu alishikiwa bastola na Wenje mbele ya Dk. Slaa katika mkutano, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na suala liko polisi Kituo cha Kati Mwanza.

“Badala ya Wenje kuchukuliwa hatua, Gwanchele pamoja na wenzake, Deus Lutalagula, Kahayi Igweselo, Makelemo Shigemelo walifukuzwa kama mbwa ndani ya chama kutokana na kutofautiana na Wenje,” alisema mmoja wa madiwani hao.

Akizungumza na vyanzo vya habari hii, aliyekuwa Diwani wa Kitangili, Henry Matata, alisema anatarajia kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.

“Mnapaswa msubiri na mkae mkao wa kula, nitatoa taarifa juu ya uamuzi nilioufikia na hatua ambazo nitazichukua na hatimaye iwe fundisho siku zijazo kwa watu ambao hawafuati demokrasia,” alisema Matata.

Kwa upande wake, aliyekuwa Diwani wa Igoma, Adamu Chagulani, alisema jana jioni anatarajia kufanya mkutano mkubwa kwa ajili ya kuwaeleza wananchi wa kata hiyo namna Chadema inavyoyumbishwa na Wenje na kundi lake kwa ajili ya maslahi binafsi.

“Hapa ninapozungumza niko Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro natoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza na jioni nitakuwa na mkutano mkubwa wa hadhara kuanika kila kitu, pia ninatarajia kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Kamati Kuu, hiki chama si mali ya mtu fulani, ni mali ya wanachama,” alisema Chagulani.

Akizungumza na vyanzo vya habari hii, Wenje alisema hababaishwi na jambo lolote linaloelekezwa kwake na kikundi fulani cha watu kutokana na uamuzi uliofikiwa na Kamati Kuu.

“Najua kila kitu ambacho kinafanyika dhidi yangu, siwezi kusema zaidi kwa kuwa hivi sasa niko katika kikao hapa Dar es Salaam,” alisema Wenje.

Toa Maoni yako kwa habari hii

No comments:

Post a Comment