MWANAHARAKATI
wa Kimataifa wa Haki za Binadamu nchini, Joram Kinanda, amependekeza katiba
mpya ieleze ikiwa rais wa nchi atajihusisha na vitendo vya rushwa, kupora au
kuhujumu uchumi, miradi ya maendeleo au kuhatarisha usalama wa taifa,
achukuliwe hatua gani.
Kinanda
ambaye ni Mjumbe wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu (Amnesty
International), alitoa mapendekezo hayo wakati akizungumza na Tanzania Daima,
na akasema hatua hiyo itaiwezesha nchi kusimama katika misingi imara na
inayokubalika na jamii.
“Tunataka
katiba ieleze kwamba rais wa nchi atachukuliwa hatua gani ikiwa kama
atajihusisha au atakiuka Katiba ya Tanzania, kuiba, kuchukua, kuchota au
kusogeza vitu vyovyote ili mradi ni wizi tu, kujipatia mapato isivyo halali na
kudhalilisha kiti anachokalia (urais),” alisema.
Kinanda
ambaye mwaka 2010 alitaka kugombea urais kama mgombea binafsi alipendekeza pia
katiba itamke kwamba uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani,
Jaji Kiongozi, na Jaji Mkuu uthibitishwe na Bunge baada ya rais kuwateua.
Alipendekeza
pia, tume huru ya uchaguzi na wajumbe wake wathibitishwe na Bunge, na wajumbe
wa Tume ya Uchaguzi wasitoke chama kimoja hata kama wamevaa kivuli cha
watumishi wa serikali.
“Katiba
tunayoitaka Watanzania ni ile itakayorudisha haki za watu zilizopotezwa au
kuporwa, ilete matumaini kwa waliovunjwa mioyo na kupoteza matumaini, iwe dira
ya kutufikisha tunapotaka kwenda kwenye maisha bora na sio bora maisha,”
alisema Kinanda.
Alisisitiza
kuwa, katiba hiyo iwe mali ya Watanzania wote na sio viongozi wa CCM peke yao
kama wanavyojinasibu kwa sababu waliitengeneza wao.
No comments:
Post a Comment