Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange salamu za
rambirambi kuomboleza kifo cha Luteni Kanali (mst) Adam Hussein Mwandu Makwaia,
aliyekuwa Mpambe wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere na Rais Ali Hassan Mwinyi.
Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Jenerali
Mwamunyange: “Nimepokea kwa majonzi na masikitiko taarifa za kifo cha Luteni
Kanali Makwaia ambaye nimejulishwa kuwa alipoteza maisha Jumanne, Septemba 4,
mwaka huu, 2012, katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo mjini Dar es Salaam.”
“Katika miaka yote ya utumishi wa Jeshi na utumishi wa
umma, Luteni Kanali Makwaia alikuwa mwadilifu na mwaminifu kwa nchi yake,
alikuwa na weledi wa kiwango cha juu katika taaluma yake ya kijeshi na alikuwa
mtiifu kwa viongozi wake. Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu zangu
za rambirambi kufuatia kifo hiki,” amesema
Rais Kikwete na kuongeza:
“Aidha, kupitia kwako natuma salamu za pole nyingi kwa
familia ya marehemu Makwaia ambao wamempoteza baba na mhimili wa familia. Pia,
kupitia kwako, natuma salamu za rambirambi kwa maofisa na wapiganaji wote wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao wamempoteza ofisa na mpiganaji
mwenzao.”
Luteni Kanali (mst) Makwaia alijiunga na Jeshi Machi
24, mwaka 1974, na alilitumikia kwa miaka 23 na miezi tisa kabla ya kustaafu.
Alikuwa Msaidizi wa Mpambe wa Rais kati ya mwaka 1978 na 1981 na kuwa Mpambe wa
Rais kwa miaka sita hadi 1987. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 62.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
6 Septemba, 2012
No comments:
Post a Comment