Katika
kile alichokiita kumshangaa IGP Mwema, Dk. Nchimbi alisema haelewi sababu za
kiongozi huyo wa polisi kuendelea kumwacha huru Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.
Slaa, wakati ametoa vitisho vilivyosababisha mauaji ya mwandishi huyo.
Akizungumzia
vitisho vya katibu huyo aliyewahi kugombea urais mwaka 2010, waziri huyo
aliwaonyesha waandishi wa habari ujumbe mfupi wa simu ya mkononi aliotumiwa IGP
Mwema kutoka kwa Dk. Slaa.
Ujumbe
huo ulisomeka hivi: ‘IGP nasubiri simu yako wajulishe polisi wako waandae
risasi za kutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha
kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya The Hague. Ni afadhali tufe
kuliko manyanyaso haya. Dk. Slaa.’
Kutokana
na ujumbe huo huku akizungumza kwa mafumbo, kauli ya Dk. Nchimbi ni kumtaka IGP
kumkamata Dk. Slaa na kumfikisha mahakamani kwa madai ya kutoa vitisho na
kusababisha mauaji.
“Namshangaa
IGP Mwema mtu anatoa vitisho lakini hapelekwi mahakamani, mtu ametuma ujumbe
kama huu halafu anarudi nyumbani kwake analala… anaendelea kuwa huru.
“Lakini
zaidi namshangaa Dk. Slaa licha ya vitisho hivyo na kifo cha mwandishi, bado
hajaenda kujisalimisha polisi,” alisema waziri huyo alipoulizwa hatua
anazochukua baada ya IGP kukaa kimya licha ya ujumbe aliotumiwa na Dk. Slaa.
Kwa
mujibu wa waziri huyo wakiwa kwenye kikao Agosti 28 mwaka huu, IGP Mwema
alitumia muda mwingi kumwomba Dk. Slaa asitishe mikutano ya hadhara kupisha
shughuli za sensa jambo lililofikia muafaka kwa wawili hao.
“Nilimsikia
IGP akiongea kwa upole… ‘nakuomba kaka yangu Slaa nielewe ndugu yangu nakuomba’
naamini waliafikiana,” alisema Dk. Nchimbi.
Akiendelea
Nchimbi alisema; “Nikiwa waziri mwenye dhamana ya kusimamia jeshi hili na kuona
haki inatendeka polisi wanaodhulumu raia hawatasalimika hata kidogo,
nitawashughulikia nanyi mtaona hebu nipeni miezi minne hivi.
“Baada
ya tume hii mtaona… tangu niingie kwenye wizara hii nimeshaunda tume tatu
ambazo matokeo yake nitayatoa hivi karibuni,” alisema Dk. Nchimbi na kuongeza kuwa
hakuna waziri mpenda haki kama yeye na wananchi hawatampata wa kufanana naye.
“Mtampata
wapi waziri kama mimi…(wote kicheko),” alisema waziri huyo ambaye kabla ya
kupewa wizara hiyo alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo aliyewaahidi
waandishi kusimamia upatikanaji wa sheria mpya ya vyombo vya habari jambo
lililokwama.
Alisema
milango ipo wazi kwa raia kupeleka malalamiko yao huku akisisitiza kwamba hana
tabia ya kupuuza kero za wananchi zinazowagusa askari polisi.
Katika
hatua nyingine, Askofu wa Kanisa Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya
Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa amesema anasikitishwa kuona raia
wakiendelea kuuawa na polisi bila kuchukuliwa hatua.
Dk.
Malasusa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utetezi wa masuala ya Kiuchumi, Haki
za Binadamu na Utunzaji wa Uumbaji, alisema hali hiyo inahatarisha amani na
utulivu nchini.
“Inashangaza
kuona uhai wa mwanadamu ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu unakatishwa kikatili
tena katika mazingira yasiyoashiria hatari,” alisema.
Alisema
KKKT inaitaka serikali kukomesha mauaji ya aina hiyo yasiendelee na polisi
wazingatie maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Taarifa
hii imeandaliwa na Irine Mark na Efracia Massawe Dar, Joseph Senga, Iringa na
Christopher Nyenyembe, Rungwe.
No comments:
Post a Comment