Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza kusitisha kwa muda
Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) mkoani Iringa na badala yake
kimeitisha kikao cha Kamati Kuu cha dharura kujadili mfululizo wa mauaji
yanayofanywa na polisi katika mikutano yao.
Mkuu
wa oparesheni hiyo iliyopangwa kufanyika mikoa mitano, Benson Kigaila, jana
aliwaambia waandishi wa habari mjini Iringa kuwa wamelazimika kukutana kujadili
hatua zaidi za kuchukua.
Alisema
kamati kuu itakutana jijini Dar es Salaam Jumapili hii na kutoa tamko juu
ya nini kifanyike baada ya wao kuwasilisha taarifa nzima juu ya matukio
mbalimbali yaliyotokea kuanzia siku ya kwanza ya operesheni hiyo.
“Tunahitaji
kukaa na kutafakari juu ya matukio haya kwa kuwa si jambo la kawaida, polisi
waue watu kwenye mikutano, nasi tukaendelea na mikutano yetu bila kuchukua
hatua stahiki,” alisema.
Alisema
wakati wote tangu kuanzia kutokea kwa msiba wa Mwangosi, kumekuwa na propaganda
nyingi zilizojitokeza juu ya hali hiyo, huku serikali, polisi na CCM wakitaka
kuhamishia lawama kwa CHADEMA.
Kigaila
aliongeza kuwa Watanzania wanajua kuwa mikutano na maandamano ambayo polisi
hawaingilii kuvunja haileti misukosuko wala vifo, kama ilivyokuwa kwenye mikoa
mbalimbali, ikiwamo ya Lindi na Mtwara.
Alisema wananchi wanapaswa
kutambua kwamba kuna kitu cha ziada ambacho serikali ya CCM na Jeshi la Polisi
wanakifanya dhidi ya CHADEMA, na si shughuli ya sensa ambayo imegeuzwa sababu
ya kusitisha mikutano yao, kwani wakati serikali inazuia CHADEMA kufanya kazi
zake, CCM inaendelea na mikutano na mchakato wa uchaguzi.
No comments:
Post a Comment