ASKARI
polisi aliyefyatu bomu lililomlipua na kumuua kinyama mwandishi wa habari wa
Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, David Mwangosi (40), amejulikana.
Tayari
mazishi ya masalia ya mwili wa Mwangosi yamefanyika jana katika Kijiji cha
Busoka, Kata ya Itete, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, huku ndugu, waandishi wa
habari, wachungaji na wananchi wengine wakililaumu Jeshi la Polisi kwa mauaji
hayo, na kwa kushindwa kuwachukulia hatua askari polisi waliosababisha kifo
hicho na jina baya la jeshi hilo.
Picha
zilizopigwa kwenye tukio la mauaji hayo, zinaonyesha askari wakiwa wamemzingira
na kumpiga Mwangosi, baadhi yao wakiwa na virungu, na wengine bastola. Mmoja
miongoni mwao, ameshikilia bunduki na kuielekeza tumboni.
Vile
vile, baadhi ya askari wamemtaja mwenzao aliyemlipua Mwangosi, wakataja na
mahali anakoishi mjini Iringa. Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni, polisi
ilikuwa haijasema wazi kama imemtia mbaroni yeye na wenzake, huku wizara na
jeshi hilo zikiunda tume za kuchunguza “chanzo” cha tukio hilo!
Baadhi
ya askari waliokuwepo siku ya tukio, walilieleza gazeti hili jana kwa sharti la
kutotaja majina yao kwamba askari aliyemlipua Mwangosi na kumuua papo hapo yuko
chini ya ulinzi tangu siku ya tukio pamoja na askari wengine walioonekana
wakimpiga mwandishi huyo.
Kutoka
mazikoni, habari zinasema kuwa haikuwa kazi ndogo kuzuia vilio na simanzi
zilizoonyeshwa na umati mkubwa wa waombolezaji waliofika kushuhudia mwili wa
marehemu Mwangosi ulioharibiwa vibaya ukionyeshwa baada ya Mchungaji wa Kanisa
la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Busoka, Mathayo Mwantemanie
kuongoza ibada ya mazishi.
Kifo
cha mwandishi huyo ambacho kimevuta hisia za wananchi wengi ndani na nje ya
nchi, hususani wakazi wa Wilaya ya Rungwe, kilimgusa kila mmoja akiwemo Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na wizara maalum, Profesa Mark Mwandosya na
mkewe, Lucy Mwandosya waliofika nyumbani kwa marehemu.
Profesa
Mwandosya alieleza jinsi msiba wa Mwangosi ulivyomgusa, kumuumiza moyo na
kumfanya ashindwe kujizuia kutoa machozi kwani tayari alishapoteza wazazi wake
wote wawili miaka michache iliyopita.
“Ni
vigumu sana kwangu kuzungumzia hali hii, Mwangosi ameniuma sana, nimezunguka
naye sana, nimefanya naye kazi kwa karibu sana, nimepotelewa na kijana wangu,
mtoto wangu, mwenzangu katika kazi, kila nilipokuwa naye alinipiga sana maswali
na mengi yalikuwa ya msingi,” alisema Profesa Mwandosya.
Kwa
upande wake, Dk. Slaa ambaye alikuwa kwenye msafara wa kusafirisha mwili wa
marehemu, alieleza mazingira ya kifo hicho na kusema msiba hauna itikadi, dini
wala rangi, na kubeza kauli za ubaguzi dhidi ya msiba wa mwanahabari huyo.
Alisema
CHADEMA itahakikisha haki ya Mwangosi haipotei na kuongeza kuwa binadamu si kuku,
kwani damu yake lazima ipiganiwe kwa haki na kueleza jinsi chama hicho
kinavyoshtushwa na vitendo vinavyofanywa na serikali dhidi ya vyombo vya
habari, hususani kulifungia gazeti la MwanaHALISI na sasa wameamua kupoteza
maisha ya mwanahabari huyo.
Naye
Mchungaji wa Kanisa la Kilutheri, Dk. Steven Kimondo na Mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Tumaini Idara ya Thiolojia, aliuliza umati huo baada ya kusema kuwa Jeshi
la Polisi linahusika na mauaji ya Mwangosi.
“Akili
yangu inakataa kusema uongo kuwa Jeshi la Polisi halihusiki na tukio la kifo
hiki, vitendo hivi vya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia vinajenga chuki kwa
wananchi dhidi ya serikali yao na kwamba lazima uchunguzi ueleze ukweli kuwa
marehemu hajafa kifo cha Mungu isipokuwa binadamu wamehusika,” alisema Dk.
Kimondo.
Dk.
Slaa alitoa ubani wa sh milioni 2, Mbeya Press Club (sh 700,000), Iringa Press
Club (sh 1,750,000), MISA-Tan (sh 500,000), huku Profesa Mwandosya akiahidi
kumsomesha mtoto mkubwa wa marehemu ambaye yupo kidato cha nne na wadogo zake,
na alitoa ubani wa sh 500,000.
No comments:
Post a Comment