To Chat with me click here

Monday, September 10, 2012

MASHUSHUSHU WAVAMIA WANAHABARI

WACHUKUA PICHA ZA MAREHEMU HOTELINI


KUNDI la watu wanaoaminika kuwa maafisa wa Usalama wa Taifa limevamia hoteli kadhaa jijini Dar es Salaam walizofikia viongozi wa klabu za waandishi wa habari kutoka mikoa yote hapa nchini wanaohudhuria mkutano mkuu ambao utatumika kutoa tamko rasmi juu ya mauaji ya mwandishi Daudi Mwangosi aliyeuawa na polisi hivi karibuni.

Habari za kuaminika zimebainisha kuwa zaidi ya maafisa usalama nane walivamia hoteli kadhaa walizofikia waandishi hao, ikidaiwa kusaka kila aina ya taarifa na nyaraka zinazohofiwa kuwa mikononi mwao na ambazo zinaaminika kuwa zitaiumbua serikali ikiwa zitachapishwa katika vyombo vya habari.

Imedaiwa kuwa, hadi sasa maafisa hao wamefanikiwa kunasa lundo la picha za marehemu Mwangosi alizopiga wakati wa uhai wake, zikiwemo zile zinazoonesha matukio yote yaliyotokea kwa siku nzima, kabla na wakati wa vurugu na tukio zima la kupigwa na kuuawa kwake.

Maafisa hao inasemekana wanatafuta pia picha hasa za waandishi wa mikoa ya Iringa na Mbeya ambazo zilipigwa kuonesha jinsi polisi walivyokuwa tayari na kuanza kuwaandama waandishi wa habari watatu ambao inadaiwa kuwa walikuwa walengwa pia wa tukio hilo.

Upelelezi huo unakuja kukiwa na taarifa kwamba, waandishi wa habari walifanikiwa kunasa mazungumzo ya polisi mkoani Iringa yanayoanika waziwazi kile kilichoongelewa na kukubalika kifanyike katika mikutano ya CHADEMA itakayofuata.

Kitu kingine kinachosakwa na maafisa hao ni madai kwamba waandishi wa habari, kutoka mkoani Mbeya na wale wa Mwanza, wanazo nyaraka na vielelezo sahihi vinavyoonesha mauaji yenye utata ya aliyekuwa mtangazaji wa ITV, John Lubungo na mwandishi wa habari wa Mwanza, Richard Masatu ambaye awali alikuwa mwandishi wa habari wa kujitegemea kabla ya kuanzisha gazeti la kasi mpya.

Inasemekana kuwa Masatu siku ya kifo chake alipigiwa simu akiwa anarudi mjini Mwanza kutoka kwenye maonesho ya Nanenane mwaka jana yaliyokuwa yanafanyika mpakani mwa vitongoji vya Igoma na Kisesa, na kukutana na afisa mmoja wa polisi na wa serikali ya wilaya katika baa moja, na baada ya kuachana nao, muda mchache aliokotwa mtaroni eneo la Igoma akiwa mahututi na alifia katika hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure.

Maafisa usalama hao, sasa imedaiwa kuwa wanasaka nyaraka za kifo hicho ambacho kama kilivyokuwa kile cha Mwangosi, polisi walitoa ripoti iliyokinzana kwa kiwango kikubwa na ile ya madaktari wa hospitali ya rufaa ya Bugando.

Katika ripoti ya polisi, ilidaiwa kuwa Masatu alikufa baada ya kugongwa na gari, lakini ile ya madaktari inadaiwa kuonesha kuwa alipigwa na kitu kizito kifuani, kutobolewa na kitu chenye ncha kali chini ya kidevu na kutokeza kwa nyuma na kuharibiwa kwa jicho la kushoto.

Aidha, baadhi ya mashuhuda walikiri kutotokea tukio lolote la ajali kama ilivyoelezwa na polisi, kwa vile eneo hilo lina shughuli nyingi za kijamii, na hivyo kama ajali ingetokea ingefahamika kwa wengi.

Maafisa usalama hao, wamegundulika baada ya wanne kati yao, kukutwa katika hoteli kadhaa zilizoko maeneo ya Sinza ambako waandishi wengi wamefikia.

Hata hivyo, mmoja wa maafisa hao alidiriki kujitambulisha akiomba waandishi wasiogope kuwapa kile wanachokijua kwa madai kuwa mauaji ya Mwangosi yamewaumiza hata wao.

Mwanausalama huyo katika hali iliyozidi kuwashangaza baadhi ya waandishi waliokuwepo katika eneo hilo, alidai kuwa wanahabari wasifikiri kuwa serikali imefurahishwa na tukio hilo, ndiyo maana wanalifanyia kazi suala hilo, hivyo ni vizuri waandishi wa habari watulie na waache kuropoka ovyo.

Waandishi wa habari zaidi ya 70 kutoka mikoani wamekutana jijini Dar es Salaam chini ya umoja wao wa klabu za waandishi wa habari hapa nchini (UTPC) katika mkutano wao wa nane ambao pamoja na kufanya uchaguzi wa bodi, utatoa tamko zito lililohusu mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi yaliyotokea Septemba 2, mwaka huu Nyololo Mkoa wa Iringa kwa kuuawa na polisi.

No comments:

Post a Comment