To Chat with me click here

Saturday, September 22, 2012

TENDWA: CHADEMA WAKITAKA WASUSIE RUZUKU


ASHANGAZWA KUTOHUDHURIA KONGAMANO LA AMANI, ADAI KAULI YA KUKIFUTA ILITAFSIRIWA VIBAYA

Msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa
KITENDO kilichofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kususia kongamano la kujadili umuhimu wa amani, usalama wa nchi na wajibu la Jeshi la Polisi na vyama vya siasa, kimemtesa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo mjini Dar es Salaam jana, Tendwa alisema kitendo cha CHADEMA kususia kongamano hilo si cha kiungwana.

Alisema, kongamano hilo, lilikuwa na nia njema ya kuwaweka karibu viongozi wa Jeshi la Polisi, vyama vya siasa pamoja na ofisi yake, ili kutafuta muafaka wa kitaifa.

Alisema CHADEMA kususia kongamano maana yake hawatimizi wajibu wa kisheria na haki, kwa maana hiyo, waendelee kuisusa pia ruzuku inayotolewa na ofisi yake.

“Kususia maana yake hutimizi wajibu, sheria, haki na Katiba ya nchi vinatambua mamlaka zilizopo, lakini pia nao wakichukua Serikali na wengine wawasusie?

“Kama hawamtaki yule anayetoa ruzuku, je watakuja kuidai? Sina tatizo na kususiwa, lakini nisusiwe kwa haki,” alisema Tendwa.

Kuhusu kauli yake aliyotishia kufuta vyama vya siasa vilivyosababisha mauaji katika mikutano yake, alisema alikuwa hailengi CHADEMA kama alivyonukuliwa.

“Mimi nilizungumzia vyama vyote vya siasa, sikuilenga wala kuitaja CHADEMA, sasa hili la kusema nimewalenga wao linatoka wapi?”

DK. BANA
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema harakati zinazoendeshwa na CHADEMA, hazikubaliki.

Alikosoa harakati za chama hicho kupitia Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), kwa kufanya mikutano kila kona ya nchi, kwamba hazina tija.

Katika mada yake, iliyohusu Mazingira Wezeshi na Hatarishi katika kujenga na kukuza mfumo wa vyama vingi vya siasa, Dk. Bana, alisema CHADEMA, ni chama kikubwa na chenye nguvu kuweza kuchukua dola, hivyo kinapaswa kuonyesha mfano kwa umma, hasa katika kutii na kuheshimu sheria.

Alisema mikutano na maandamano ya CHADEMA yanayofanyika kila mahali nchini hayana lengo zuri, kwa sababu muda huu si wakati wa kampeni.

Alisema wakati huu, ni wakati wa vyama vya siasa kujijenga kwa kufanya mikutano ya ndani ya chama, kuandaa viongozi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, uchaguzi mkuu 2015 pamoja na kuhamasisha wananchi washiriki shughuli za maendeleo na si kufanya mikutano na maandamano yanayofanana na kampeni za uchaguzi.

“CHADEMA ni chama kikubwa ambacho kimejijengea heshima kubwa na kinatarajiwa kuchukua dola wakati wowote, kwa hiyo hakina budi kufuata na kuzingatia sheria za nchi ili kuonyesha mfano kwamba kipo tayari kuongoza umma.


Dovutwa
Mwenyekiti wa Chama cha United Peoples Democratic (UPDP), Fahami Dovutwa, alilishauri Jeshi la Polisi kuzuia maandamano ya vyama vya siasa, kwa sababu yanatishia amani ya nchi.

Alisema, Polisi wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kutawanya maandamano ya baadhi ya vyama vya siasa na kusababisha watu kufa na wengine kuumia.

Mtatiro
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema wananchi hawawezi kutii sheria iwapo wanaowaongoza nao hawazitii pia.

Alisema Watanzania wa sasa, wanajifunza kutokana na mataifa mengine, hivyo polisi wa Tanzania wanapaswa kutumia busara kushughulikia masuala ya wanasiasa, hususani wa upinzani.

IGP Mwema
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Inspekta Jenerali Saidi Mwema, alisema anaongoza chombo ambacho hakipaswi kuwa na upande wowote na si kweli kwamba jeshi lake linazuia vyama vya siasa kufanya shughuli zake.

Akitoa takwimu, alisema kuanzia Julai mwaka 2011 hadi Julai 2012, barua za vyama hivyo kuomba vibali vya kufanya shughuli za kisiasa zilikuwa 1,994, kati ya hizo, 1,668 zilikubaliwa na 110 zilikataliwa kutokana na sababu mbalimbali.

No comments:

Post a Comment