Mkuu wa Chuo cha Ruaha, Gasper Msigalla |
TUHUMA
za baadhi ya walimu kuwafelisha kwa makusudi wanafunzi na wengine wa kiume
kutumia mwanya huo kuwaomba wanafunzi wa kike kufanya nao ngono, zinakikabili
Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilichopo Ipogolo, mjini Iringa.
Mkuu
wa Chuo hicho Gasper Msigalla (pichani) alikiri kuwepo kwa tuhuma hizo
zinazoendelea kuchunguzwa ili haki itendeke.
“Ni kweli kuna madai
hayo ya wanafunzi kufelishwa ambayo pia yamefikishwa kwenye Bodi ya chuo hicho
inayoongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa,” alisema.
Alisema
jumla ya wanafunzi 139 kati ya wanafunzi 682 wa mwaka wa pili walifeli mitihani
yao ya Februari, mwaka huu.
Msigalla
alisema uongozi wake na wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
inayosimamia chuo hicho ilitilia shaka matokeo hayo.
Hata
hivyo alisema wanafunzi hao walifeli mtihani huo baada ya kushindwa kupata
alama zinazostahili katika tahimini ya kila siku (continuous assessment) yenye
maksi 50.
“Alama
hizi na zile wanzotakiwa kupata katika mitihani yao ya darasani ambazo nazo ni
hamsini ndizo zinazopima ufaulu wa mwanafunzi baada ya kupata wastani wa alama
hamsini,” alisema.
Alisema
wanafunzi hao walifeli mtihani huo baada ya kupigwa penati na mwalimu mmoja
aliyetajwa kwa jina la Betha Lukasi kwasababu za kuchanganya zilizoelezwa na
wanafunzi hao.
Wanafunzi
hao walisema mwalimu huyo alikuwa akiuza chakula chuoni hapo kinyume na taratibu
za zabuni na alipoondolewa na uongozi wa chuo akatumia nafasi yake kulipa
kisasi.
Jitihada
za kumpata mwalimu Lukasi kutoa ufafanuzi wake kuhusiana na madai ya wanafunzi
hao hazikuweza kuzaa matunda na taarifa kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho zilidai kwamba
amelazwa katika hospitali ya Lushino, mjini Iringa.
Atakapotoka
hospitalini mtandao huu utamtafuta mwalimu huyo ili kwa upande wake atoe sababu
za wanafunzi 139 kufeli mitihani huo.
Katika
mazingira ya kutatanisha wakati wanafunzi hao wakidaiwa kufeli mitihani hiyo
kumekuwepo na madai kutoka kwa baadhi yao kutakwa kimapenzi na walimu wa kiume
wa chuo hicho ili wawasaidie kukabiliana na mazingira hayo.
Mkuu
wa chuo hicho hakuweza kuthibitisha madai hayo, hata hivyo alisema yatafanyiwa
uchunguzi na ikibainika yana ukweli walimu watakahusishwa watatolewa
mapendekezo ya kuondolewa chuoni hapo.
No comments:
Post a Comment