To Chat with me click here

Friday, September 14, 2012

MEYA ‘AUZA’ KISIWA

Tanga City Mayor, Mr. omar Guledi
MEYA wa Jiji la Tanga, Omary Guledi, ameingia katika kashfa nzito baada ya kudaiwa kutaka kuuza eneo la Kisiwa cha Mnyanjani kwa mwekezaji wa hoteli ya kitalii.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wa kisiwa hicho, wameapa kupinga jambo hilo kwa gharama zozote, kwa sababu kuuzwa kwa kisiwa hicho ni kuwapora ardhi yao.

Taarifa za meya huyo kuuza kisiwa ziliibuliwa jana mjini hapa, wakati wananchi hao wa Mtaa wa Mnyanjani walipokuwa wakitoa malalamiko yao kwa Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mwidau (CUF).

Mwidau, ambaye yuko katika ziara ya kichama mkoani hapa, alifika katika eneo hilo ili pamoja na mambo mengine, kusikiliza kero za wananchi hao.

Akizungumza katika mkutano huo, mkazi wa Mnyanjani aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Swalo, alisema tangu mwaka 2007, Meya Guledi amekuwa akishirikiana na wawekezaji kwa lengo la kutaka kuwahamisha wananchi katika kisiwa hicho ili amkabidhi mwekezaji atakayejenga hoteli ya kitalii.

Alisema kwamba, katika kufanikisha mkakati huo, meya huyo kwa kushirikiana na Diwani wa Kata ya Mzingani, Mohamed Kombora (CCM), wameanza kwa kuuza kiwanja cha michezo ambacho ni mali ya wananchi wa mtaa huo tangu mwaka 1966.

Kutokana na hali hiyo, alisema yeye na wenzake waliamua kuandika barua ili kupinga hatua ya ujenzi wa nyumba katika kiwanja cha michezo, lakini meya huyo alipingana na wananchi hao.

Katika kutekeleza jambo hilo, alisema meya huyo alitoa maelekezo kwa diwani ili amsaidie mwekezaji huyo kujenga katika kiwanja hicho cha michezo.

“Mheshimiwa Mbunge, hivi sasa kuna mpango ambao unaandaliwa na jiji kwa kushirikiana na diwani kutaka kuuza eneo hili la makazi yetu ya asili ili kuweza kujenga hoteli ya kitalii na mpango huu unafanywa na Meya wa Jiji kwa kushirikiana na diwani wa kata yetu.

“Katika mkakati wao wa kulifanikisha hilo, hivi sasa meya ameanza kuuza kiwanja cha michezo ambacho kipo tangu mwaka 1966 kama mali ya Serikali ya Mtaa wa Mnyanjani na kwa maelezo ya diwani mwenyewe, aliwahi kutuambia, kwamba anapokea vitisho kutoka kwa meya ili ahakikishe mwekezaji huyo anapewa kiwanja hicho.

“Huyo mwekezaji ameshamwaga mawe ili aweze kuchimba msingi, sasa tunakuambia mbunge wetu hatupo tayari kuiachia hali hii.

“Tupo tayari kufa huku tukitetea haki zetu, hasa hasa hili suala la ardhi, sisi ni wanyonge, tunajiuliza tumekosea nini katika nchi yetu, tunaamua sasa kupaza sauti zetu ili Mungu azifanyie kazi, iwe ni wakati wa jua au mvua.

“Tuna ramani ya Serikali ambayo inaonyesha eneo hili ni la wazi, lakini kwa kuwa lipo kando ya bahari sasa linanyemelewa na walafi na mafisadi wa mali zetu wanyonge ambao ni sisi masikini tulio ndani ya nchi yetu.

“Tunakuomba mbunge hebu fikisha salamu zetu kwa Waziri Tibaijuka ili aweze kuyajua haya, kwani hatua nyingine yoyote itakayofanyika hapa kinyume na maelezo haya, hapatakalika hapa,” alisema Mwalo huku akishangiliwa wa wananchi wenzake.

Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnyanjani, Sharifu Bwakame, alisema anaufahamu mgogoro huo na kwamba unachangiwa na Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji la Tanga.

“Nami nimekuwa nikiambiwa na watendaji wa halmashauri kuwa eneo hili limeuzwa kwa mwekezaji, lakini siku zote ninawaambia kama hilo lipo naomba barua ya kisheria inayoonyesha kuuzwa kwa eneo hilo.

“Hili la kiwanja cha michezo lilikuwapo tangu mwaka 2007 na limekuja hasa baada ya mtaa wetu kugawanywa.

“Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, hata katika kikao cha kata chini ya diwani wetu nilishangazwa na uamuzi wa upande mmoja wa kumpatia kiwanja cha michezo mwekezaji huyo,” alisema Sharifu.

Akijibu hoja za wananchi hao, Mbunge Mwidau aliwasihi wananchi hao kutojichukulia sheria mkononi, kwa kuwa suala hilo atalishughulikia baada ya kuwasiliana na mamlaka husika.

“Ninawaomba msimwage damu, ninachopenda kusema ni kwamba, nitawasiliana mapema na mamlaka husika ili kuweza kujua kiini cha mgogoro huu ambao kama ukiachwa unaweza kuchafua amani ya eneo hili.

“Ninajua vijiji vya Mnyanjani na Mwarongo ni vya asili tangu enzi na enzi, katika hili ninapenda kuwahakikishia nitalisimamia kwa kuanza kupata ukweli juu ya kuuzwa kwa kisiwa hiki cha Mnyanjani na kiwanja cha michezo ambacho nimeona kuna mawe yaliyowekwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya watu.

“CCM imekuwa haina tena huruma na maisha ya wananchi na kinachoonekana sasa ni wanyonge kuzidi kuonewa huku wenye mali wakiendelea kuneemeka kwa jasho la wachache, hili hapana silikubali, ninachowaomba msimwage damu ndugu zangu,” alisema Mwidau.

Meya Guledi alipozungumza kwa simu na vyanzo vya habari hii juu ya suala hilo, alisema hawezi kulizungumzia kwa kina na kwamba anayemtaka amtafute kwa muda wake.
Toa Maoni yako kwa habari hii

No comments:

Post a Comment