BARAZA
la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo, BAVICHA, limemtaka Rais Jakaya
Kikwete na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuiepusha nchi katika
machafuko kwa kuwawajibisha haraka viongozi wa dola katika Wizara ya Mambo ya
Ndani kutokana na tuhuma za unyanyasaji, mateso na mauaji kwa raia wasio na
hatia endapo wao hawataki kujitoa.
Waliotajwa
wajiuzulu au wawajibishwe na Rais kwa maslahi ya umma ni Waziri wa Mambo ya
Ndani Dk. Emanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Saidi Mwema.
Aidha
Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja, kamanda wa polisi mkoa wa
Morogoro, Faustin Shilogile, Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Michael
Kamuhanda, na wakuu wa kikosi cha kutuliza ghasia mikoa hiyo wamependekeza
washtakiwe.
Akisoma
maazimio ya baraza hilo la taifa lililofanyika mjini hapa kwa siku tatu,
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Heche, alisema tayari serikali imeiweka nchi
rehani kutokana na kufumbia macho matukio hayo yanayoendelea kufanywa na vyombo
vya usalama.
“Mpaka
sasa wananchi hawana imani na serikali yao hususan Jeshi la Polisi na haya
matukio yameubadilisha ulimwengu jinsi polisi wanavyoendesha unyama kwa raia
wasio na hatia kwa visingizio visivyo na maana,” alisema Heche.
“Uone
nchi hii inavyokwenda, huyu Kamuhanda aliua watu wanne Songea kumlinda
kahamishiwa Iringa nako amefanya hayo hayo mpaka sasa hajakamatwa, huyo
Shilogile aliua hapa Morogoro anafunikwafunikwa na hawa wote wamekuwa
wakilindwa na makao makuu kupitia mkuu wa operesheni jeshi la polisi Paul
Chagonja ambaye anaeneza uongo kwa umma kuwalinda polisi wenzie,” aliongeza.
Katika
maazimio hayo likiwemo la kuwataka kujiuzulu, kuwajibishwa au kufunguliwa kosa
la mauaji kwa mantiki ya ‘Common intention’ viongozi hao, BAVICHA pia lilimtaka
Rais Kikwete kuunda tume huru ya kiuchunguzi ya kimahakama katika makosa yote
yaliyotokea Arusha, Arumeru, Igunga, Ndago-Singida, Morogoro na Iringa.
Aidha
baraza hilo linakusudia kuunda kikosi kitakachotafiti matatizo ya vijana
likiwemo suala la elimu duni na ukosefu wa ajira na kutoa ushauri juu ya
mustakabli wa taifa baada ya 2015, kuendelea kuwaunga mkono walalahoi nchini
wakiwemo machinga, na imelaani CCM kuwatumia vijana katika mafunzo ya kijasusi
kwani yanalenga kulichafua taifa.
Mbali
na maazimio hayo pia baraza hili limetoa tahadhari kwa vyombo vya dola na
Msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa kuepusha kauli za vitisho
zinazohatarisha amani ya nchi huku wakimshauri kuifuta CCM kwa kufundisha
ujasusi.
Kwa
upande wake Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Sharifa Suleiman alisema baraza
limepitia na kuchambua kwa kina mustakabali wa kisiasa, vijana na sintofahamu
iliyopo na inayozidi kudhihirika kuwa uongozi uliopo umeshindwa kuongoza hasa
katika kusimamia rasilimali za nchi kwa faida ya Watanzania.
No comments:
Post a Comment