To Chat with me click here

Wednesday, September 26, 2012

TANZANIA, ILIPO NA IENDAKO


MAANDISHI ndilo chimbuko la utafiti; na unapotaka kuandika lazima utumie ushahidi aidha wa kuona, kusikia, au hata wakati mwingine kufukua yaliyofukiwa kwenye hazina ya elimu.

Falsafa ya elimu inasema kwamba, “elimu ni maarifa yanayotafutwa kwa utafiti unaozingatia uhuru, ukweli na uadilifu wa akili katika kufikia utashi wa mizania ya elimu na ukweli.” Kwa jinsi hiyo, hatuwezi kutafuta maendeleo yetu bila kutafuta ukweli wa nchi yetu kuanzia pale tulipokuwa, tulipo na tuendako!

Na kama tunataka kupata faida ya elimu yenye kuambatana na utendaji kwa ujenzi wa jamii ya watu walio sawa na huru, lazima tukubali kutafuta elimu kwa njia ya utafiti wenye lengo la kupata nguvu ya maarifa kwa kuzingatia taarifa sahihi kwa kuzingatia utafiti wenye vigezo vya uhuru, ukweli na njia muafaka ya kufikia hitimisho lenye mapendekezo ya kisomi (kwa kuzingatia weledi).

Haiwezekani kujenga nchi ambayo watu wake wameipa kisogo elimu yenye manufaa inayotokana na utafiti. Na kamwe nchi haiwezi kuendelea kama watu wake wataendeleza ubishi wa “kiwendawazimu” ilhali wanasahau wajibu wa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Tanzania, kama nchi inayoendelea, ina miaka takriban hamsini (50) ya uhuru. Na kwa vyovyote vile, si changa kama tulivyozoweshwa kuamini! Miaka hamsini si haba. Tumetoka wapi, tupo wapi na tunataka tuelekee wapi? Hili ni swali kwa kila mwananchi. Kila mmoja anapaswa kujiuliza na kupata majibu yake.

Hatuwezi, kama taifa, kuendelea kulaumu ukoloni kama alivyowahi kuandika Mwalimu Julius Nyerere (Tujisahihishe, 1962). Lawama kwa wakoloni nadhani tungaliweza kuzielekeza kwenye ile miaka mitano hadi kumi ya uhuru; sidhani kama tuna sababu tena ya kuendelea kuelekeza lawama kwa wakoloni! Kama Malaysia, Vietnam na Thailand wameweza sisi tushindwe tuna nini?

Mada hii imeanza na mchokoo wa kifalsafa na kimantiki katika kuonesha kwamba elimu ni ufunguo wa maisha ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hata hivyo, lengo mahsusi ni katika kutafuta kwa nini Tanzania iendelee kuwa nchi ya “kufikirika” kwa uongozi wa siasa kushindwa kuyapatia matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayowakabili wananchi wake? Tanzania ni nchi tajiri wa rasilimali na mali ya asili. 

Nimelitumia neno “kufikirika” kutokana na ukweli kwamba kwenye mada hii napenda nitumie falsafa ya Shaaban Robert inayopatikana kwenye kitabu cha “Kufikirika” kwa vile sehemu kubwa ya mtazamo wa kifalsafa aliouonyesha unafanana sana na hali ya Tanzania siku hizi!

Sipendi kuandika kwamba, “uongozi wa siasa-uchumi na uchumi-jamii wa Tanzania haujaleta maendeleo tangu uhuru,” hasha! Ninachotaka kuonyesha ni juu ya uongozi kushindwa kufikia utashi wa watu wengi wanaotaabika na maisha yaliyochoka na kukatisha tamaa ilhali sehemu kubwa ya utajiri wa nchi katika rasilimali na maliasili ikitumika kuwanufaisha watu wachache wakiwamo viongozi wasiozingatia masilahi mapana na endelevu ya watu na maendeleo yao.

Watanzania wamekuwa kama yatima wa maendeleo huku wakikodolea macho maendeleo ya nchi nyingine; hata zile zilizokuwa nyuma ya Tanzania kwa rasilimali na maliasili kama Thailand! Hata kama, na kama inavyosemwa ati “tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele,” sidhani kama tunaweza kutembea kifua mbele kwamba sisi ni nchi huru kiuchumi, kijamii na kisiasa!
Shaaban Robert aliandika, “Majuju ni taifa lafi na litishalo kabisa. Kila kitu kigumu kijulikanacho duniani kilikuwa laini kama mkate kati ya meno ya majuju; na kilicho kichungu kilikuwa kitamu kama asali katika maonjo yao. Kwa ulafi uliokithiri viumbe hawa, walikuwa hawajui halali wala haramu.” Dhana hapa ni juu ya ulafi wa watu (hususan wa viongozi) wanaotumia maliasili kwa ulafi uliopitiliza pasipo kujali haki ya wananchi katika kumiliki utajiri wa nchi.

Viongozi wa Tanzania kwenye saisa, uchumi na jamii wamesahau wajibu wao wa uhuru, haki, usawa na uadilifu katika kuwatumikia wananchi katika kuwaongoza kujiletea maendeleo yao; badala yake wamekuwa wakichukua utajiri wa nchi kwa njia za haramu. Huu ndio mtazamo wa Majuju kwa mujibu wa Shaaban Robert (Kusadikika, 1991 ukurasa wa 23, Mkuki na Nyota Publishers).

Shaaban Robert (kama alikuwa anatabiri jinsi viongozi watakavyokuwa waroho, walafi na wenye uchu wa kujitajirisha kwa kuiba maliasili na rasilimali za taifa) aliandika hivi:

“Kabuli alipopelekwa mbele ya Jeta alimkuta amekaa kitako midomo wazi. Mto mrefu na mpana ulikuwa ukimimika katika kinywa chake kikubwa sana. Tone la maji hata moja halikupata nafasi ya kukiepa kinywa hicho. Tani milioni moja za mwamba, milioni moja za chuma, milioni moja za magogo, na milioni nyingi za samaki zilimiminika pamoja na mkondo wa maji humo kinywani pia kila dakika tano. Lakini kila dakika moja Jeta alilia: Kiu, njaa, kiu, njaa!” Hivi ndivyo viongozi wetu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii walivyo siku hizi baada ya miaka zaidi ya hamsini tangu Shaaban Robert kuandika maneno haya ya kifalsafa na kimantiki.

Tazama, viongozi wa kisiasa walivyo walafi na wenye choyo wanaotamani kujimilikisha sehemu kubwa ya uchumi wa nchi! Wao, viongozi wa kisasa, ndio wanaotamani kumiliki uchumi wote kwa kutumia njia zisizozingatia uhuru, haki, usawa, uadilifu na insafu.

Wale waliyeaminiwa kupewa dhamana ya kuwaongoza wananchi wanyonge na masikini katika kuelekea kwenye saada ya maisha yao wamegeuka na kuwa watawala washenzi wasiyozingata haki na uhuru wa wananchi. Wamejipa utawala na wameacha nafasi yao kama viongozi wa umma. Badala yake, na kwa ari, nguvu na kasi ya ajabu wanawanyonya wananchi na au kujimilikisha haki za wananchi katika kuamua hatima ya maisha yao kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kwa upande mwingine, baadhi ya viongozi wa dini (na wa kijamii) wamekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza unyonyaji wa kitaasisi na kuwageuza wafuasi wao kama mtaji wa kiuchumi, kijamii na hata kisiasa!

Kwa vile kuna ushahidi wa moja kwa moja juu ya unyonyaji unaofanywa na madhehebu za dini dhidi ya wafuasi wa dini husika kuna kila sababu ya kuwaelezea viongozi wa dini kwa kuwa na (hao, viongozi wa dini) ni sehemu ya kuharibu mujtamaa wa maisha bora ya wananchi kimaada, kimaanawi na kiroho.

Wapo baadhi ya viongozi wa dini wanaotumia nafasi zao za uongozi wa kiroho kama sehemu ya kuwatia uzezeta wananchi na hata kuwaingiza kwenye msongo wa kuwatumia kisiasa, kiuchumi na kisiasa kwa minarafu ya kulinda nafasi zao kwenye taasisi zao!

Tazama, leo tunashuhudia (kama walivyo baadhi ya viongozi wa siasa), viongozi wa dini wameingia kwenye siasa za kifisadi huku wakimtumikia shetani mpenda ulimbikizaji wa mali, ulafi, na anayetamani kuwafanya wananchi wandelee kuwaabudia hata pale inapogundulika kwamba uongozi wao hauna tija kwa maendeleo ya watu na miundombinu ya kiuchumi.

Ufisadi wa baadhi ya viongozi wa dini kwa sehemu kubwa umewafanya baadhi ya wafuasi kuharibu mwendo murua (siasa) kwa vile siasa inayochanganywa holela na dini ina madhara mapana pale panapokosekana mizania ya uhuru, haki, usawa, uadilifu na insafu ya matumizi bora na endelevu ya rasilimali watu, fedha na vitu kwa manufaa ya umma.

Hata kama, na ndivyo inavyodhaniwa na watu wengi, kwamba: viongozi wa dini wanafanyakazi za kiroho zaidi kuliko kwa masilahi ya kidunia; bado ukweli unaonyesha kwamba baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa sehemu ya mfumo wa unyonyaji unaotumia taasisi kama sehemu ya kuchuma, kulimbikiza na kutumia mali hayo kwa manufaa ya watu wachache binafsi kwenye taasisi za dini pasipo kuzingatia haki na usawa kwenye jamii ya kidini.
Kama walivyo wanasiasa walafi, waroho na wenye uchu na choyo cha kutumia ufisadi wa kimfumo na wa ndani ya mfumo, wapo baadhi ya viongozi wa dini mashuhuri nchini wanaojitajirisha kwa mwendo huu. Nchi inaongozwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa, kiuchumi na kijamii (kama viongozi wa dini) wenye roho chafu na zilizofisidika; na hali hii inaifanya nchi kuzama kwenye shida, taabu na shaka kubwa ya kibinadamu.

Kwa kuwa uongozi wa aina zote (kisiasa, kiuchumi na kijamii) umefanywa mradi wa wachache kuchuma kutoka kwa walio wengi; Tanzania, kama alivyosema Shaaban Robert, imekosa kiasi.

Shaaban Robert anaandika: “Zamani za marejeo yake hapa, alisema habari za mamlaka ya kiasi, heshima iliyo ya wastani, uhuru wa kadiri, na nguvu yenye mpaka. Mtu mwenye mamlaka ya kiasi hawatesi watu waliyo chini ya mamlaka yake wala hajitesi yeye mwenyewe; mwenye heshima iliyo na wastani hujiheshimu yeye mwenyewe na wengine; mwenye uhuru wa kadiri ni muungwana yeye mwenyewe na wengine; na mwenye nguvu yenye mpaka hadhulumu na wala yeye hadhulumiwi.”

Haya maneno ni tunu adhimu na adimu kupatikana kwenye maandiko ya Kiswahili kwa miongo zaidi ya mitano sasa!

Tazama, ukosefu wa kiasi kwa viongozi wetu wengi kwenye siasa, uchumi na jamii. Wanasiasa wengi wanataka kuchuma mali kwa pupa; wafanyabiashara wanataka kuchuma kwa haramu (na hata wakati mwingine kwa ufisadi wa kiuchumi); na baadhi ya viongozi wa dini wameacha nafasi yao katika kuleta amani ya nafsi na ujenzi wa roho zenye matumaini kwa waumini na waamini wao, wanahubiri chuki na kuendesha harakati zenye kuligawa taifa huku wakitumia nafasi zao kujitajirisha na shughuli zinazochukua taswira ya dini ilhali ni ufisadi mpevu na wenye kunuka aina zote za roho ya shetani.

Mwendo wa uongozi umekuwa kama “chui” aliyejivika vazi la kondoo na kujinasibisha na wanakondoo katika kurahisha mawindo yake. Hii ndio hatari ya mfumo wa kitaasisi unaondeshwa na baadhi ya viongozi wa dini na taasisi zao ndani ya maisha mseto ya Tanzania.

Hapana shaka yoyote kwamba wapo viongozi wachache wa kada zote, yaani; siasa, jamii na uchumi wanaochukia hali ya mchafukoge katika jamii ya watu wa Tanzania.

Na vilevile, zipo taasisi za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazojishughulisha moja kwa moja na shida na tabu za wananchi wa Tanzania na kutafuta suluhisho la matatatizo yanayolikumba taifa kwa sasa kama vile: umasikini; magonjwa; ujinga; ufisadi na udhalimu. Hata hivyo, inaonekana kwamba nguvu ya viongozi hawa wenye nia na dhamira ya dhati ya kuendesha mapambano dhidi ya maadui wa taifa inazidiwa nguvu na wale wengi wenye roho mbaya na walafi.

Sehemu ya viongozi wa kisiasa wamekosa heshima kwa watu na hata kujivika “uungu-mtu” na kuendesha utesaji wa raia! Viongozi wengi kwenye msonge wa utawala na menejimenti ya siasa hawajiheshimu na hawaheshimu watu na ndio maana hakuna anayeweza kuendesha siasa murua kwa minajili ya kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo yanayowakabili wananchi wengi wa Tanzania.

Tazama, elimu yetu inadodorora na inaelekea kudidimia kwa kiasi cha kutishia mustakabali wa kizazi cha Tanzania ijayo! Nani awezaye kumfunga paka kengele juu ya kuboresha elimu ya Tanzania?

Elimu si kujua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK); hasha! Ni maarifa yanayoambatana na utendaji katika kumfanya mwenye elimu aweze kupambana na mazingira yake kwa kuzingatia uwiano wa utashi wake na mazingira. Elimu imeachwa iende kama inavyokwenda; huku viongozi wengi wenye ukwasi wakipeleka watoto wao kusoma nje ya nchi!

Tazama, viongozi walafi wanachuma Tanzania wanakwenda kuwekeza nje ya nchi kwa masilahi yao na vizazi vyao! Huu ni ujambazi wa kiserikali uliyoishika Tanzania kwa miongo kama mitatu sasa (1985 hadi 2012) na nadhani hali hii itaendelea kwa muda mrefu ujao kwa vile hakuna dalili na au dhamira na mikakati ya makusudi katika kurekebisha hali hiyo.

Viongozi wengi wenye dhamana ya uongozi ndani ya chama kinachotawala wamekuwa wakijiimarisha kwenye nafasi na au kutafuta nafasi zitakazowahakikishia kuendelea kutumia nafasi na satwa zao kwenye ujenzi wa nchi isiyozingatia uhuru, haki, usawa, uadilifu na insafu katika kuwaongoza watu kwenye maendeleo yao na kwa vizazi vijavyo vya Tanzania.

Hakika nchi yetu inaliwa na viongozi walafi; na kwa ulafi huo wamewekeza kwenye kada ya uongozi kama mtaji wa biashara unavyowekezwa kwenye sekta za uzalishaji.

Siasa, uchumi na jami kama sekta zinazoshirikiana zimevamiwa na watu wasiyojali utu, heshima na ubinadamu hata kufikia kiwango cha kupora haki ya wananchi katika kufikia utashi wa maisha yao. Uongozi wa zama hizi umesahau kwamba, “wananchi ndio msingi wa mamlaka ya uongozi wa nchi.”

Pahala pa uongozi wa umma pamewekwa uongozi binafsi unoatawala siasa, jamii na uchumi kwa maslahi ya kibinafsi na watu wachache kwenye mtandao wa mafisadi na makuwadi wa ufisadi. Hakuna anayechukua nafasi ya kuwaonea huruma wananchi wanaodhulumiwa na baadhi ya viongozi walafi; na hata anapotokezea mtu kwenye mfumo wa siasa kuwatetea wanyonge wanaodhulumiwa na mfumo kandamizi huonekana kama adui na njama za kummaliza kisiasa, kijamii au kiuchumi hufanywa na viongozi wenye satwa ya mamlaka isiyozingatia haki.

Tanzania haiwezi kuendelea kama itaendelea na ulafi wa viongozi na watawala usiyozingatia uhuru, haki, usawa, uadilifu na insafu ya uongozi na menejimenti ya rasilimali na au maliasili ya nchi.

Ni wakati muafaka sasa kuhakikisha kwamba katiba mpya inatoa fursa ya moja kwa moja kwa wananchi kumiliki nchi yao na kushiriki moja kwa moja katika ujenzi wa maisha yao yote kwa kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo kwa kuzingatia uongozi na menejimenti ya pamoja.

Uongozi ni dhamana; na viongozi wa kada zote (pamoja na taasisi za dini) wawajibike kwa watu kwa maendeleo ya watu. Hatujachelewa, tufanye mabadiliko! 

Na Bakari M Mohamed

No comments:

Post a Comment