NAPE ASEMA KAULI ZAO
HAZIWEZI KUSIKILIZWA KWANI HAWAJIAMINI
CHAMA
cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitishwi na baadhi ya viongozi wake ambao
wamekuwa wakitoa kauli zao barabarani kwa ajili ya kulalamika na kukikosoa
chama badala ya kupeleka malalamiko yao katika vikao husika.
Kitendo
cha viongozi hao kuendelea kutoa taarifa zao za malalamiko barabarani ni dalili
za kutojiamini na kuonyesha udhaifu wa kuhimili mikiki ya uchaguzi ndani ya
chama hicho na inawezekana wana agenda zao za siri.
Kauli
hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa ya chama hicho,
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
juu ya vikao vya chama ambavyo vinaendelea mjini hapa.
Licha
ya Nape kutowataja vigogo hao kwa majina, lakini ni wazi kuwa walengwa ni
pamoja na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye kwa
siku za karibuni amenukuliwa akilalamikia vitendo vya ufisadi kwenye mchakato
wa uchaguzi ndani ya CCM na hivyo kuibua mjadala mzito kwa baadhi ya makada
akiwemo Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja, wakimtaka awataje kwa
majina anaowatuhumu.
Wengine
waliosikika hivi karibuni wakilalamikia mchakato huo wa uchaguzi unaoendelea ni
Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Nimrod Mkono wa Musoma Vijijini ambao
inasemekena majina yao yamekatwa kwenye orodha ya wagombea, huku wakisema
hapatatosha iwapo wataenguliwa kweli kimizengwe.
Nape
alisema kuwa CCM inashangazwa na baadhi ya wanachama wake ambao wanaonyesha
woga wa kushindwa kuhimili mikiki ndani ya chama, hususan katika kipindi hiki
cha uchaguzi na badala yake wamekuwa wakitishia kujitoa kama majina yao
hayatarudishwa kwa ajili ya kuchaguliwa katika nafasi zao walizoomba.
Alisema
kuwa chama hakiwezi kuwasikiliza viongozi ambao wamekuwa na tabia ya kutoa
matamshi yao barabarani na kwamba kama wanataka kutoa kauli hizo, watumie fursa
ya kuwasilisha hoja zao katika vikao.
“Chama
hakiwezi kusikiliza kauli za barabarani ambazo zinatolewa na viongozi hao, kama
wana hoja wazilete katika vikao kwa maana nao ni viongozi, wasipofanya hivyo
basi huenda wana agenda zao za siri, ambazo wanazijua wao,” alisema.
Kuhusu
baadhi ya wagombea ambao walisikika wakidai kuwa majina yao yasiporudishwa
patachimbika, alisema kuwa inaonyesha ni jinsi gani hawajiamini kwani kiongozi
ni lazima awe mvumilivu na mwenye kuhimili mikiki ya siasa za sasa ambazo zina
ushindani mkubwa.
“Kama
kiongozi anaanza kusikia tetesi kuwa jina lake halitarudishwa halafu anaanza
kusimama barabarani na kudai kuwa hapatatosha, ni wazi kuwa ni mwoga wa
kuhimili ushindani, lakini nataka kusema kuwa haki itatendeka na busara
zitatumika.
“Hakuna
mtu ambaye jina lake litakatwa kwa ajili ya mizengwe, bali vigezo vitazingatiwa
ili kila mmoja apate haki yake, na lazima wagombea watambue kuwa kwa vyovyote
vile lazima apatikane kiongozi ambaye ataweza kuongoza jumuiya husika,”
alisisitiza Nape.
Aliongeza
kuwa kutokana na kuwepo kwa wingi wa wagombea katika nafasi mbalimbali, kuna
uwezekano wa kutokea msuguano mkubwa kwa wanachama kutokana na kila mmoja
kutamani kushika nafasi aliyoiomba.
“Kimsingi
wanachama waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali ni wengi zaidi ya mahitaji,
hii ni ishara kuwa chama bado kinapendwa… kunawezekana kukatokea msuguano wa
ndani kutokana na wingi wa wagombea, lakini chama kina utaratibu wa kumaliza
mambo kama hayo,” alisema.
Kuhusu
vikao kwenda kinyume na ratiba, Nape alisema kuwa kutokana na wingi wa wagombea
wa nafasi mbalimbali, imelazimika sekretalieti kukaa siku tatu badala ya moja
na kamati ya maadili ilitakiwa ikae siku moja, lakini imekaa mbili tofauti na
matarajio.
Nape
alisema kutokana na wingi wa wagombea, imewalazimu vikao kuchukua muda mwingi
kujadili kwa makini ili kuhakikisha haki inatendeka na kuongeza kuwa, kwa
nafasi ya wenyeviti wa mikoa zinazotakiwa ni nafasi 31 ila walioomba ni 187,
katibu siasa na uenezi mkoa zinatakiwa nafsi 31 walioomba pia ni 187.
Alisema
kuwa makatibu wa uchumi/fedha wa mkoa nafasi zinazohitajika ni 31 ila walioomba
ni 170, wenyeviti wa wilaya nafasi ni 31 walioomba 148, wenyeviti wa wilaya
wanahitajika 161 walioomba ni 965, wajumbe wa NEC taifa wanahitajika 221,
lakini walioomba ni 1,380 na wajumbe wa NEC taifa wanahitajika 20 bali
walioomba ni 89.
Nape
alisema kuwa nafasi nyingine ni wenyeviti wa Jumuiya Taifa ya UVCCM ambayo
inahitajika nafasi moja ila imeombwa na wagombea 47, UWT nafasi moja nayo
inagombewa na watu 9, Jumuiya ya Wazazi nafasi moja imeombwa na watu 22 na makamu
mwenyekiti UVCCM inahitajika nafasi moja, lakini walioomba ni 27, UWT nafasi ya
makamu imeombwa na watu watatu huku ile ya wazazi ikiombwa na watu 10.
Hata
hivyo, Nape alisema kuwa hatua ya mwisho ya kupitisha majina ya wagombea hao ni
NEC na kwamba vikao vingine vinapitisha na kutoa alama za sifa ya wagombea.
Wazee wamvaa Sitta
Wazee
wa CCM mkoani Shinyanga, wametishia kufanya maandamano ya amani kuhusiana na
kauli tata zinazoendelea kutolewa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta.
Katika
tamko lao, wazee hao walisema wakati umefika sasa Sitta awaeleze Watanzania juu
ya kauli zake hizo, ikiwemo ile ya kuwepo kwa mafisadi ndani ya chama na
aliyoitoa hivi karibuni akiwa Karagwe, ya maisha bora kwa kila Mtanzania
hayatawezekana.
Kwa
niaba yao, Shomvi Ibrahimu Saidi, alisema kuwa waziri huyo ambaye pia ni mjumbe
wa NEC na mbunge wa Urambo Mashariki, amekuwa akikaririwa akitoa tuhuma nzito
ndani ya serikali na chama, hivyo ni vema akaweka wazi majina ya watuhumiwa wa
ufisadi.
Pia
walikumbushia jinsi kiongozi huyo alivyowahi kuitolea maneno makali Kamati Kuu
ya CCM katika kipindi cha ‘Dakika 45’ kinachurushwa na Televisheni ya ITV,
akisema kwamba ilihongwa na mafisadi ikabadili utaratibu wa kuchagua Spika wa
Bunge.
Wazee
hao wamemuomba Waziri Sitta kama hana ushahidi wa kutosha wa kuupeleka kwenye
vikao vya chama na vyombo vya dola kama TAKUKURU, polisi na mahakama, ni
afadhali akae kimya kuliko kuendelea kuwachanganya watu.
No comments:
Post a Comment