To Chat with me click here

Friday, September 28, 2012

UONGOZI MPYA WA CCM SASA NDANI YA BAHASHA

MIGIRO MAKAMU MWENYEKITI, NAPE KATIBU MKUU, NGELEJA KATIBU MWENEZI. 

 
UONGOZI mpya wa CCM sasa uko ndani ya bahasha. Kilichobaki ni uamuzi wa kura za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ( NEC ) kufungua bahasha hiyo na kuweka siri hiyo wazi.

Kumalizika kwa vikao vikuu vya chama kunatoa taswira ya uongozi mpya wa CCM, hasa kuzingatia kilio cha muda mrefu kutoka kwa wanachama kuisihi CCM irejee kwenye uasilia wake.

Sasa ni sura mpya na taswira mpya. Kauli ya Mwenyekiti Taifa, Rais Kikwete kuwa “Hatuwezi kuwa na Chama cha wazee tu, hapana, tumeona tuwape nafasi vijana wengi, tena wasomi waweze kugombea…Ni muhimu kupata sura mpya ya chama na taswira mpya kwa kuingiza wasomi”, ni kauli inayoashiria mabadiliko makubwa katika CCM yanayotarajiwa.

Anaendelea kusisitiza akiwaeleza wajumbe wa NEC, kuwa “lengo ni kuunda timu ya ushindi ya Chama kwa mwaka 2014 katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, na mwaka 2015 katika Uchaguzi Mkuu.”

Nasaha kwa wale “wenye ndimimbili” anasema kuwa “isiwe nongwa ukiwa basi ni kulalamikia chama hiki kimefanya nini, ukishafikia hivyo wewe haukuwa na moyo na chama ila moyo wako ulikuwa na shida ya uongozi.”

Wakati hali ikijiri hivyo, hali ndani ya chama inaripotiwa kuwa ni tulivu hata mara baada ya kupita panga la kung’oa visiki, hii ikiashiria kuwa sasa chama kinajivua ‘gamba’, na hii imepokewa kwa shangwe na furaha na wana-CCM wengi.

Watu wanaanza kupata matumaini makubwa, hasa wanachama na wananchi waliokuwa wameanza kupoteza matumaini.

Chanzo kutoka ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu Taifa ( NEC ) kilisema hali ndani na nje ya ukumbi imepokewa vizuri kutoka kwa watu wa kada mbalimbali ambao wametoa mawazo yao kuhusu matokeo ya kuchuja majina ya wagombea ndani ya CCM, na kutemwa kwa baadhi yao, hasa wanaodhaniwa wamekosa maadili na mwalekeo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao kuhusu uchujaji na upitishaji wa majina ya wagombea kuanzia Kamati ya Maadili, Kamati Kuu ( CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ( NEC ) zinasema kazi ya kupitia majina imekamilika na ilikuwa ngumu.

Kazi ya kupitia majina ya wagombea ilifanywa na Kamati ya Maadili kupitia majina ya waliopendekezwa na vikao kutoka wilayani na mikoani.

Imeelezwa kuwa idadi ya wagombea 2,853 waliomba kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama, na wengine 2,104 waliomba nafasi za uongozi kupitia jumuiya za Chama. Vikao vyote vilifanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama.

Matazamio ya wananchi wengi ni kuona wajumbe wa vikao hivyo wanafanya uchaguzi sahihi na makini kupata watu watakaoleta mabadiliko makubwa na kuwa viongozi bora katika chama hicho, ambao watakuwa na uwezo na dhamira ya kweli ya kusimamia sera na kuwa wabunifu wa mikakati ya kukuza uchumi na kuhakikisha serikali inatekeleza ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Moja ya safu ambayo ni nguzo na muhimili ni nafasi ya wasaidizi wa karibu wa Mwenyekiti Taifa, wakiwamo Makamu wa Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Katibu Mwenezi.

Katika Chama, hao wanaelezwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa ndio hasa wana uzito wa pekee wa kuwezesha kupeperusha vyema bendera ya chama na kuiaminisha CCM katika jamii ndani na nje ili iendelee kukubalika.

Tathmini, utafiti na uchambuzi unaonyesha kuwa upepo unavuma kuwaelekea aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro, kushika nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti Tanzania Bara, Katibu Mkuu kuwa Nape Nnauye na Katibu Mwenezi na Itikadi ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kushika nafasi ya Nape ili kwa pamoja wasukume mbele gurundu la CCM hadi mwaka 2015.

Imeelezwa kuwa CCM sasa inataka kuwa na viongozi wenye uadilifu, shupavu, hodari na wenye kukitetea chama. Aidha, kuwa na timu ya ushindi wa chama na si ushindi wa mtu binafsi, na kuachana na viongozi wenye ndimimbili.

Wachambuzi hao wa siasa na tathmini wanaeleza kuwa chama kiendelee kuwa taasisi si mtu kuwa zaidi au juu ya chama, dhana ambayo ni potofu.

Nukuu ya Baba wa Taifa inawakumbusha wajumbe wa Kamati ya Maadili, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa kwamba, “chama dhaifu huzaa serikali dhaifu”.

No comments:

Post a Comment