Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi(CCM) wakifuatilia hoja kutoka kwa mmoja miongoni mwa wajumbe katika mjadala
wa kupitisha majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya Umoja huo ngazi
ya Mkoa na Taifa.
UMOJA wa Vijana wa
Chama cha Mapinduzi (UVCCM), wamemaliza kikao cha baraza la umoja huo ambapo
wamejadili ajenda mbalimbali za msingi kuhusu Uchaguzi na pia wamejadili juu ya
hali ya siasa nchini na mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa amani na mauaji,
ambapo wamekinyooshea kidole Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa
kuwa vinara wa matukio ya mauaji, kitu ambacho ni hatari kwa Taifa.
Hayo yamebainishwa na
Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela wakati wa mkutano wake na waandishi wa
habari uliofanyika katika ofisi ya Katibu Mkuu, jengo la Mikutano (whitehouse)
katika Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi, Dodoma.
Alisema kuwa,kumekuwa
na matukio ya mauaji kwenye mikutano ya chama hicho katika mikoa ya Singida,
Igunga, Tabora, Morogoro na Iringa hali ambayo imekuwa ikitishia Usalama na
Amani ya Nchi.
“Tunalaani Chadema
kuwa vinara wa vurugu zinazosababisha mauaji na kila tukio linapotokea viongozi
wa Chadema wanakuwepo, hali inayoonyesha kuwa siasa wanazoendesha si za
kistaarabu” alisema
Alisema kuwa Chadema
wanachojenga ni hatari kwa Taifa na pia hatari kwa Umoja wa Vijana pia na kama
wana mapenzi ya kweli na watanzania waache siasa zinazasababisha mauaji mara
kwa mara.
Katika hatua
nyingine, Shigela amesema kuwa,Kikao cha baraza Kuu kilimalizika jana na
kufanya maamuzi baada ya kujadili na kupitisha majina ya wagombea na baadhi ya
nafasi majina yatapelekwa halmashauri kuu ya taifa (NEC) ambacho ni chombo cha
mwisho cha maamuzi katika Chama.
Amezitaja nafasi
ambazo tayari zimetolewa maamuzi, kuwa ni nafasi ya mwakilishi mmoja kutoka
UVCCM kwenda UWT, Mwakilishi mmoja kutoka UVCCM kwenda wazazi, Baraza Kuu taifa
nafasi tano Zanzibar na nafasi tano Bara, na sasa orodha hiyo inaandaliwa ili
majina ya waliochaguliwa yatangazwe rasmi.
Amesema kuwa,katika
nafasi nyingine ikiwemo Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti tayari yamewekewa alama
na yatapelekwa Halmashauri kuu ya Taifa (NEC).
Pia amewataka
wagombea ambao tayari wamefanyiwa uteuzi waache siasa za kuchafuana na zile za
makundi.
Aidha alisema kuwa
Mkutano Mkuu wa taifa unatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 20, mwaka huu na
kutaka wajumbe wote kuhakikisha wanafika Dodoma Oktoba 19.
Shigela amesema kuwa,
Baraza kuu lilipata nafasi ya kuwapongeza vijana wa Jumuiya kwa kuthibitisha
kuwa umoja huo ni tanuru la kuoka viongozi kwa baadhi yao kuteuliwa nafasi
mbalimbali serikalini na kwenye Chama na kulitaka Baraza kuu kuzingatia
mahitaji ya vijana ili wapate fursa zaidi za kugombea ili umoja huo uweze
kupeleka sura nyingi za vijana ndani ya chama.
Pia alisema kuwa
wametapa nafasi ya kuitafakari taarifa ya kazi nzuri ya Serikali kwa
kuwawezesha vijana katika suala la kuwapatia elimu na kuwawekea mikakati ya
miaka mitano ya kusaidia vijana.
Shigela aliitaka
Serikali kuwa na mipango ya kudumu ili kuweza kudhibiti majanga mbalimbali
yanayotokea hapa nchini k.v mafuriko, kuzama kwa meli, mauaji n.k.
No comments:
Post a Comment