To Chat with me click here

Saturday, September 22, 2012

JAJI LUBUVA AVIONYA VYAMA VYA SIASA


Jaji Mstaafu Damian Lubuva
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imevionya vyama vya siasa nchini kwa kuvitaka viache kutumia lugha chafu kabla na baada ya uchaguzi wowote. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu, Damian Lubuva, alisema lugha chafu zimezidi kukithiri katika kampeni za siasa, hali ambayo inaweza kuchangia uvunjifu wa amani endapo haitadhibitiwa.

“Tume haitavumilia tabia hiyo ambayo si ya kistaarabu, kwani inachochea vurugu. Sisi tusingependa vyama vya siasa vijihusishe na kashfa katika kampeni wala kabla ya kampeni, kwani lugha zisizofaa hazileti picha nzuri katika jamii.

“Tuna tume ya maadili ambayo inaweza kutoa adhabu kwa chama ambacho kinaenda kinyume na maadili ya nchi yetu, nasema chama cha siasa kikianza kampeni zake kinatakiwa kitoe taarifa, ili kiwekewe ulinzi na kupitia kwa viongozi wao, lazima wawaelimishe wagombea wao kutumia lugha iliyo sahihi,” alisema Jaji Lubuva katika mkutano huo, uliokuwa wa maandalizi ya chaguzi ndogo za madiwani katika kata 29 zilizoko katika halmashauri 27. Chaguzi hizo, zinatarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Pamoja na hayo, Jaji Lubuva alizitaka asasi za kiraia na wadau wengine nchini, kuunga mkono kazi za tume hiyo, katika kuhamasisha wananchi waishio maeneo unakofanyika uchaguzi.

Alisema umefika wakati kwa vyama vya siasa kunadi sera za vyama vyao na kuacha ubabaishaji wa kutoa lugha chafu ambazo ni kinyume na maadili.

Pia alisema kuwa, marekebisho ya maadili ya uchaguzi ili yaweze kutumika, lazima yatiwe saini kati ya Serikali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyama vya siasa.

“Nashukuru marekebisho hayo yametiwa saini karibu pande zote husika isipokuwa vyama viwili vya siasa hadi sasa havijatia saini.

“Kwa maana hiyo, nawaomba na kuvikumbusha vyama husika kutia saini marekebisho ya maadili ya uchaguzi haraka iwezekanavyo.

“Nayasema haya kwa sababu bila hivyo, kisheria vyama vya siasa havitaruhusiwa kufanya kampeni zake, kwani kama vikifanya kampeni bila kusaini marekebisho haya vitakuwa vinakiuka sheria,” alisema Jaji Lubuva.

Naye, Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Msafiri Mtemelwa, alisema tume hiyo inatakiwa kuwa na mtandao ambao hautatenganisha vyama.

No comments:

Post a Comment