To Chat with me click here

Thursday, September 27, 2012

WAZIRI AMNG'OA MKUU WA SHULE ILBORU

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa
Serikali imemsimamisha kazi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ilboru iliyoko mkoani Arusha, Jovinus Mutabuzi, kufuatia tuhuma mbalimbali dhidi yake, yakiwamo matumizi mabaya ya madaraka.

Tuhuma hizo zilisababisha wanafunzi wa shule hiyo ya vipaji maalum Jumatatu wiki hii kuandamana hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, wakishinikiza ang’olewe.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, Kasimu Majaliwa, alitangaza uamuzi huo jana baada ya kusikiliza madai ya wanafunzi katika mkutano uliofanyika shuleni hapo.

Baada ya Mutabuzi kusimamishwa kazi, Naibu Waziri Majaliwa alimteua Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Lorna Nteles, kukaimu nafasi hiyo.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Halfa Hida, kuteua mkaguzi wa ndani kufanya uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili Mutabuzi, ikiwamo ya kutumia stakabadhi bandia anazodaiwa kuhalalisha malipo ya wanafunzi.

Katika mkutano wake na wanafunzi hao, Majaliwa alibaini kuwa hoja zao zina msingi, ikiwamo ya matumizi mabaya ya Shilingi 800,000 alizoziingiza kwenye Chama cha Kuweka na Kukopa (SACCOS) ambazo alikuwa akizikopesha kwa riba kwa walimu na watumishi wa shule hiyo.

Katika maandamano ya wanafunzi hao, pia walidai kuwa Mutabuzi ameisababisha shule hiyo kudorora kitaaluma na kuwadhalilisha wanafunzi kwa kuwaita mashoga.

Mkuu wa Mkoa Magesa aliwasihi wanafunzi hao kurejea shuleni na kuendelea na masomo wakati suala lao likishughulikiwa.

Hata hivyo, baaada ya kurudi shuleni walianzisha mgomo wa kutoingia darasani na kutokula chakula.

Hali hiyo ilimlazimu Majaliwa kwenda shuleni hapo na kuwasikiliza wanafunzi hao na kabla ya ya kufanya mkutano alitembelea maeneo yote yanayolalamikiwa na wanafunzi hao. Maeneo hayo ni jiko, mabweni na choo cha matundu mawili kinachodai kujengwa kwa Sh. milioni 25.

Akizungumza katika mkutano huo, Majaliwa aliwasihi wanafunzi hao kutovunja sheria kwa kuitisha migomo na maandamano yasiyo rasmi huku akimtaka kaimu mkuu wa shule hiyo kusimamia nidhamu ya wanafunzi hao.

Naibu Waziri huyo akiwa amefuatana na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa na mabomu na silaha za moto, alilazimika kutumia zaidi ya saa tano kutoa ufafanuzi wa madai ya wanafunzi hao ambao muda wote walionekana kumsikiliza kwa makini huku hoja yao kubwa wakidai hawamtaki mkuu wa shule.

Hata hivyo,  Mjaliwa alikerwa na mabango aliyoyakuta yamebandikwa kwenye kuta katika majengo yote ya shule hiyo ya vipaji maalum yakiwa na ujumbe mbalimbali wa kumpinga Mutabuzi huku baadhi yake yakiwa yamechorwa
vikaragosi vinavyomfananisha utawala wa marehemu Nduli Idd Amini Dada wa Uganda.

Pamoja na kuwasihi kuwa wawe wavumilivu wakati hatua zaidi zikichukuliwa, lakini wanafunzi hao walipaza sauti wakidai kuwa hawapo tayari kuingia darasani bila kuondolewa kwa mkuu wao hali iliyomlazimu Naibu Waziri kutamka kuwa amemsimamisha kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

Tamko hilo la Naibu Waziri Majaliwa la kumsimamisha kazi Mutabuzi liliamsha shangwe na nderemo kutoka kwa wanafunzi hao.

Naibu Waziri huyo alipiga marufuku michango isiyo na tija shuleni, matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi, adhabu za malipo ya fedha, matumizi ya M-Pesa mashuleni pamoja na kuziagiza bodi za shule kutatua matatizo ya wanafunzi pale yanapoibuka kabla ya kuleta madhara.

Hii ni mara ya kwanza kwa Waziri kumsimamisha kazi mkuu wa shule papo kwa papo kutokana na madai ya wanafunzi.

No comments:

Post a Comment