LISSU
ATAJA WABUNGE WALA RUSHWA
KAMBI
rasmi ya Upinzani Bungeni imetaka kuchunguzwa kwa madai ya Naibu Kiongozi wa wa
kambi hiyo, Zitto Kabwe, kuhongwa.
Kambi
hiyo pia imetaja majina ya wabunge sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa
wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika wa Bunge, Anne
Makinda, mwishoni mwa wiki, ikidai kuwa kwa namna moja ama nyingine walihusika
na vitendo vya rushwa.
Wabunge
hao wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa kampuni za mafuta ili kuipigia debe
menejimenti ya Shirika la Ugavi wa umeme nchini (TANESCO).
Akizungumza
jana na waandishi wa habari mjini hapa, Mnadhimu Mkuu wa kambi hiyo, Tundu
Lissu, alisema wamesikia tuhuma nyingi dhidi ya Zitto lakini hawajamhoji
kiongozi huyo.
Alisema
wanaviomba vyombo vinavyohusika vimchunguze Zitto ili ukweli ujulikane na hatua
zinazostahili zichukuliwe kama atathibitika kuwa na makosa. “Chama
hatujakaa na Zitto kumsikiliza lakini tunataka achunguzwe, hatuna masilahi
yoyote katika uchafu huu wa rushwa. “Uchunguzi
huu utatupa msingi wa kumchukulia hatua kama chama ikiwa itathibitika
amehongwa,” alisema.
Alibainisha
kuwa, mbunge wao huyo amekuwa akihusishwa na kumtumia ujumbe mfupi wa vitisho
Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakimu Maswi.
Alisema
ni vema Zitto achunguzwe na apewe nafasi ya kujieleza kama itakavyokuwa kwa
wengine kuliko kuendelea kusambaza maneno ya kufikirika.
Alibainisha
wamejiridhisha pasipo shaka kuwa wabunge wao watatu waliokuwa wajumbe kwenye
Kamati ya Nishati na Madini, John Mnyika (Ubungo), David Silinde (Mbozi
Magharibi) na Mwanamrisho Taratibu Abama (Viti Maalumu), hawajahusika kwa
lolote katika sakata hilo la rushwa.
“Kama
kuna mtu ana ushahidi zaidi ya huu tulionao tunaomba atuletee ili hatua zaidi
ziweze kuchukuliwa, lakini mpaka sasa wabunge wetu hawa watatu hawajashiriki
kwa lolote katika kuomba rushwa,” alisema.
Kauli
ya Lissu inashabihiana na aliyoitoa Zitto juzi ambapo alisema hajachukua hongo,
ila kuna watu wana lengo la kuchafua jina lake.
Zitto
alisema kuwa uchunguzi dhidi yake ndiyo njia pekee ya kuudhihirishia umma kuwa
hahusiki na chochote kama baadhi ya watu wanaoeneza maneno ya kumchafua.
Awataja
wala rushwa
Kuhusu
majina ya wabunge wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, Lissu
alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge na Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, wabunge hao walipaswa kutaja masilahi yao
kibiashara kwenye shirika hilo.
“Sasa
wabunge hawa hawajawahi kufanya hivyo na wameendelea kuwa wajumbe wa Kamati ya
Nishati na Madini na wengine kufanya biashara na TANESCO,” alisema Lissu na
kuwataja kuwa ni Munde Tambwe, Sara Msafiri, Mariam Kisangi wa Viti Maalumu,
Yusuf Nassir (Korogwe Mjini) na Charles Mwijage Muleba Kaskazini.
Lissu
alifafanua kuwa Tambwe na Msafiri wana tenda ya kuiuzia TANESCO matairi na
kwamba hawajawahi kutangaza masilahi yao katika jambo hilo kwenye kamati zao.
“Mwijage
ni mtaalamu mwelekezi wa Kampuni ya PUMA Energy iliyopewa tenda na Maswi
kuiuzia mafuta TANESCO, hivyo kama mjumbe wa Kamati ya Nishati ana mgongano wa
kimasilahi. Nassir na Kisangi hawa wanafanya biashara ya mafuta wanamiliki
vituo vya mafuta na wana mgongano,” alisema.
Kuhusu
Christopher ole Sendeka, Lissu alidai kuwa amekuwa akizipigia debe kampuni tatu
zilizonyimwa tenda ya kuiuzia mafuta TANESCO akiwashawishi wajumbe wa kamati
kuwa serikali ilikiuka kanuni kuipa tenda Kampuni ya PUMA Energy. Mbunge
mwingine aliyetajwa ni Vicky Kamata wa Viti Maalumu ambaye alidaiwa kuwa na
mgongano wa kimasilahi na Maswi.
“Tunampongeza
Spika kwa kuivunja Kamati ya Nishati na Madini lakini tunataka azivunje pia
zile za LAAC, inayoongozwa na Augustine Mrema (TLP) na POAC ya Zitto, kwa kuwa
baadhi ya wajumbe wake wamekuwa wakitajwa sana kujihusisha na vitendo vya
rushwa.
Fukuto
la kutajwa kwa majina ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa lilitawala mjadala wa
Bunge jana, ambapo wabunge, Kangi Lugora (Mwibara), James Mbatia (Kuteuliwa),
Ali Keisy (Nkasi), Joshua Nassari (Arumeru Mashariki na Salum Baruani (Lindi
Mjini), waliomba mwongozo wa Spika wakidai wahusika wawekwe wazi.
Hata
hivyo, katika mwongozo wake, Naibu Spika, Job Ndugai, alisema kuwa Kamati ya
Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge inaendelea na uchunguzi kama ilivyoagizwa na
Spika ndipo hatua nyingine zitafuata.
“Wabunge,
baadhi mtaitwa kusaidia kamati hiyo lakini si kwamba ukiitwa kuhojiwa na kamati
inamaanisha umepokea rushwa, ni katika hatua za mwanzo tu kufikia ukweli wa
kile kinachochunguzwa. Labda niwaeleze kuwa Spika amekubali kuiangalia kamati
hii ili wale wajumbe wenye mgongano wa kimasilahi waondolewe,” alisema.
Alikataa
kutaja majina ya watuhumiwa akisema kuwa Spika pamoja na yeye hawawajui
wahusika ndiyo maana wanachunguza kuwabaini. Lakini aligusia kuwa Taasisi ya
Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeanza kuwahoji baadhi ya wabunge.
Ndugai
pia alitolea ufafanuzi mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail
Rage (CCM), aliyetaka kujua ni kwanini kiongozi wa upinzani alitaja majina ya
watuhumiwa wa rushwa kutoka CCM wakati kwenye chama chake cha CHADEMA kuna
watuhumiwa pia.
“Mimi
ningewashauri kuwa katika jambo hili tuwe na subira na tukitaka kulizungumza
tutende haki kwa pande zote, maana hakuna chama chenye sera ya kura rushwa,
tusilifanye kisiasa kwa kuoneana,” alisema Ndugai.
Watuhumiwa
wajitetea
Tanzania
Daima iliwasiliana na watuhumiwa kujua wana kauli gani dhidi ya tuhuma hizo
ambapo Mwijage, Msafiri na Munde simu zao ziliita pasipo kupokewa wakati Ole
Sendeka, Kisangi na Nassir walizikanusha.
Nassir
alisema kuwa si kweli kuwa anafanya biashara ya mafuta bali aliwahi kufanya
kazi katika Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ambapo alipata ujuzi na
hivyo kuwa na nia ya kutaka kuanza biashara ya gesi.
“Lissu
ni mwanasheria lakini nashindwa kuelewa ni kwanini anafanya ‘generalization’
katika jambo hili, mimi sifanyi biashara ya mafuta na TANESCO wala serikali
kupitia wizara husika, nampuuza kwa madai yake na nitamchukulia hatua,”
alisema.
Kwa
upande wake Kisangi alikiri kufanya biashara ya mafuta, akisema anamiliki vituo
vya mafuta eneo la Mbagala Rangi Tatu, lakini akafafanua kuwa kila wakati
alipochangia hoja ndani ya Bunge na kwenye Kamati ya Nishati na Madini
alitangaza masilahi yake.
“Mimi
niko vizuri sina wasiwasi, rejea kumbukumbu rasmi za Bunge utaona kuwa
nimetangaza masilahi yangu, hivyo namshangaa huyu mwanasheria. Ina maana naye
kuwa kwenye Kamati ya Sheria ni mgongano wa masilahi kwa vile ni mwanasheria?”
alihoji.
Ole
Sendeka naye alisema kuwa hakuwahi kuzipigia debe kampuni anazohusishwa nazo
kwani alichokifanya kwenye kamati ni kuwaeleza wajumbe namna Maswi alivyovunja
sheria ya manunuzi ya umma.
“Maswi
ameichukua PUMA Energy kama mashati ya mitumba sokoni wala haikuwa
kushindanishwa, sasa kama Lissu ambaye ni mwanasheria haoni hilo napata taabu,”
alisema.
Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment