CHADEMA KUWASHITAKI
RPC, MORO, IRINGA
MATUKIO
ya kuuawa kwa raia, vitisho na vurugu zenye mwelekeo wa kumwaga damu,
vimeliweka taifa katika mtikisiko mkubwa huku shinikizo la kuwataka Waziri wa
Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Saidi
Mwema wajiuluzu nyadhifa zao likizidi kuongezeka.
Katika
mahoajiano maalum, viongozi mbalimbali wa dini na siasa wamesema
kuwa, hali ya nchi imefikia mahali pabaya na watanzania sasa wanaishi kwa hofu
kwa kuwa hawana uhakika na usalama wa maisha yao.
Askofu
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Karagwe,
Benson Bagonza alisema viongozi wa serikali na jeshi la polisi waliopewa
dhama ya kulinda uhuru na maisha ya watu, wameoneshwa kushindwa kiasi cha
kuifanya nchi kuwa katika hali ya mashaka makubwa.
Askofu
Bagonza, alisema kuwa mauaji ya raia yanayaodaiwa kufanywa na jeshi la polisi
katika mikoa kadhaa hapa nchini kwa visingizo mbalimbali, ni ishara ya wazi ya
kukosekana kwa utawala wa sheria, pia dalili ya kutowajibika kwa viongozi.
Aliongeza
kuwa, kuna ushahidi wa polisi kuua watu ovyo, lakini tume zinapoundwa hakuna
jambo lolote la maana linalofanyika kutokana zaili ya kulindana huku raia wema
wakipoteza uhai.
“Kwa
mfano polisi analalamikiwa kuua…serikali inaunda hicho kilichoitwa kamati,
ikija na majibu ikasema polisi aliyefanya tendo hilo alitumwa na mkubwa wake
je, huyo mkubwa atakuwa tayari kuwajibika au ndiyo tunataka tu uundwaji wa tume
tu,” alisema.
Kiongozi
huyo alisema kuna ubaguzi wa waziwazi katika uendeshji wa shughuli za siasa, na
kwamba wizara na jeshi la polisi limetumika kunyanyasa makundi mengine hasa
chama kinachoonekana kukubalika na wengi.
“Kuna
kikundi cha watu kinaweza kuandamana na bila kuwa na kibali na wala hakuna
mauaji yanayotokea…lakini wengine wakiomba kibali wananyimwa je, huoni kuwa
hapa tulipo sasa ni pa hatari zaidi kuliko huko tuendako,” alihoji.
Shinikizo
la kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kujiuzuru
nafasi hiyo limetolewa pia naKatibu Mkuu wa Chama cha CCK, Renatus Muabhi
kutokana na kushindwa kwake kuwadabisha askari wake waliohusika na tuhuma za
mauaji ya raia, likiwemo la kuuawa kwa mwandishi Daud mwangosi.
Muabhi
alisema, mbali ya kujiuzulu kwa Nchimbi, pia makamanda wa polisi wa mikoana
askari wao wanapaswa kuona umuhimu wa hatari ya uzembe na ukiukwaji wa sheria
za polisi unaosababisha vitendo vya mauaji ya raia.
Alisema,
watanzania bado wanalihitaji jeshi hilo, hivyo ni vema kutizamwa upya mfumo wa
maadili ya taasisi hiyo ili kuondokana na wale wakorofi ambao hujichukulia
sheria mkononi, lakini kwa mfumo mbovu wa kubebana na kufanya sifa ya idara
hiyo kuporomoka na kupoteza imani kwa wananchi.
SAU yamshukia Tendwa
Nacho
Chama Cha Sauti ya Umma (SAU), kimemshukia Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini,
John Tendwa kikimtaka afute kauli yake ya kutishia kukifuta Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) kwa madai ya kuhusika na mauaji ya raia.
Mwenyekiti
wa taifa wa SAU, Paul Kyara alisema Tendwa anapaswa kutoa tafsiri ya sheria ya
vyama vya siasa na ile ya polisi, kwa kuwa kukinzana kwa sheria hizo ndio
chanzo cha vurugu na mauaji yanayotokea.
“Tangu
kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992, idadi kubwa ya Watanzania
wameshapoteza maisha kutokana na vurugu zinazoibuka katika mikutano ya hadhara,
ikiwa ni pamoja na matukio ya hivi karibuni yaliyotokea mkoani Iringa, Morogoro,
Singida na Arusha,” alisema.
Kyara
alisema sura ya 258 ya sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1993 na ile ya polisi
iliyofanyiwa marekebisho 2002, ndio chanzo cha tatizo.
Kyara
alisema, moja ya kazi ya chama cha siasa ni kufanya mikutano, lakini vyama
vimekuwa vikikutana na vikwazo, hivyo ni vyema kuweka utaratibu maalum hata
kubadilishwa kwa sheria hizo mbili ili kuondoa tofauti inayojitokeza.
Alisema
kuwa sheria ya vyama vya siasa inatoa uhuru kwa vyama vya siasa kufanya
mikutano ya hadhara na maandamano na hutakiwa kutoa taarifa polisi ndani ya saa
48 kabla ya maandamano hayo kufanyika.
Alisema
sheria hiyo ndiyo inayochangia kuwepo kwa mvutano unaopelekea kutokea kwa
mgogoro kwa sababu chama hujiona kuwa na haki huku polisi nao wakijiona kuwa na
haki ya kulinda amani ya raia.
Mwenyekiti
huyo, alisema kuwa ni lazima ufumbuzi wa haraka upatikane kabla madhara
hayajawa makubwa zaidi kwa kuwa hata Chama Cha Wananchi CUF nacho kimeanza
mikutano yake katika mikoa mbalimbali.
Alisema
suala hili lisipoangaliwa kwa upana kuna hatari ya taifa kukumbwa na maafa
makubwa kwa kuwa vyama vya upinzani vitafanya mikutano yake kwa lazima, ambapo
polisi nao wataonesha ubabe na hivyo kuzua balaa.
TEC wavuta pumzi
Wakati
viongozi hawa wakieleza hofu yao, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),
limekataa kusema lolote kuhusiana na hali tete katika taifa.
Katibu
Mkuu wa baraza hilo, Padri Antony Makunde alipotakiwa kutoa msimamo wake,
alisema kwa hali ilivyo katika nchi, hawezi kusema lolote.
Alidai
kwamba mambo yanayoendelea katika taifa hili hususan mauaji ya raia yanahitaji
kutolewa kauli na rais wa baraza lake, na sio mtu mwingine yeyote akiwemo yeye.
Hata
hivyo, jitihada za kumpata Rais wa TEC, Askofu wa Jimbo la Iringa, Mhashamu
Ngalalekumtwa zilikwamba baada ya simu yake kutopatikana.
Msimamo wa CHADEMA
Wakati
hayo yakijiri, CHADEMA kwa upande wake, kimetoa msimamo wa kukataa kwanza,
kamati ya uchunguzi iliyoundwa na Waziri Nchimbi kuchunguza mauaji ya Mwangosi
huko Iringa, lakini pia kinakusudia kuwafungulia mashitaka ya mauaji makanda wa
polisi wa mikoa ya Morogoro na Iringa.
Akizungumza
hayo mbele ya waandishi wa habari jana mjini Morogoro, Ofisa Habari wa CHADEMA,
Tumaini Makene aliongeza kufikishwa mahakamani kwa askari mmoja anayetuhumiwa
kumuua Mwangosi hakuwezi kumaliza kiu ya wapenda haki, akidai kuwa watuhumiwa
wengine bado wanatamba mitaani.
“Uamuzi
wa Kamati Kuu iliyokaa karibuni ni kwamba RPC wa Iringa, Michael Kamuhanda
akamatwe na afikishwe mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya Mwangosi, kwa sababu
yeye ndiye alikuwa akiongoza operesheni wakati polisi wanafanya mauaji hayo,
alikuwa field.
“Lakini pia CHADEMA
tunasema maaskari wote wanaoonekana kwenye picha wakati Mwangosi anakamatwa,
kupigwa na kuuwawa ni watuhumiwa wanapaswa kukamatwa na kufikishwa mahakamani
kwa mauaji, chini ya hapo ni kuwahadaa wapenda haki Tanzania na duniani kote
ambao sasa wanaanza kuiangalia Tanzania kwa jicho la aina yake kutokana na
mauaji yanayofanya na vyombo vya dola,” alisema Makene.
No comments:
Post a Comment