ANAYETUHUMIWA KUUA
MWANDISHI AKWAMA KUFIKISHWA MAHAKAMANI
WINGU jeusi limeendelea
kutanda ndani ya Jeshi la Polisi mkoani Iringa baada ya baadhi ya askari mkoani
humo kunyoosheana vidole kuhusu tukio la polisi kuua mwandishi, huku baadhi yao
wakimlaumu Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC), Michael Kamuhanda.
Askari kadhaa
waliozungumza na gazeti hili kwa siri jana, walisema kama RPC angesikiliza
ushauri wa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) kuhusu namna ya kukabiliana na
wanachama wa CHADEMA, maafa yasingetokea.
Walisema Kamuhanda ndiye
aliwaamuru askari wake kuwakamata viongozi wa CHADEMA waliokuwa kwenye mkutano
wa ndani wa ufunguzi wa tawi katika Kijiji cha Nyololo, kwa maelezo kuwa
hakuwaruhusu kufanya hivyo.
“Kama mnakumbuka, RCO
mwanzo alizielewa hoja za CHADEMA juu ya vikao vyao vya ndani, lakini alipokuja
RPC hali ikabadilika kutokana na kupewa maelezo na mkuu wetu wa kikosi cha
kutuliza ghasia mkoa,” alidokeza mmoja wao.
Walisema kwamba hata
katika tawi la kwanza walilofungua viongozi wa CHADEMA, RCO alifika lakini
hakuwashambulia. Wakati wakifungua tawi la pili, ndipo RPC akafika, na amri
zikatolewa kuwashughulikia viongozi na wanachama wa CHADEMA.
Kwa maelezo ya polisi
hao, viongozi na wanachama wa CHADEMA hawakuwa wameleta fujo yoyote, na kwamba
kama polisi wangelinda tu mikutano yao yaliyotokea yangeweza kuepukwa.
Askari hao walisema
inasikitisha kwamba uamuzi wa mtu mmoja umelifanya jeshi zima lionekane baya
mbele ya umma; na kwamba hata wao wanatii amri kwa sababu kazi yao haiwaruhusu
kuhoji amri za wakubwa wao.
Baadhi yao walisema hata
maneno na vitisho vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali, kwamba
CHADEMA kina vurugu, ni uonevu na propaganda za kisiasa, kwani vurugu zilitokea
pale CHADEMA walipoanza kutawanywa.
Habari ambazo
hazijathibitishwa kutoka mkoani humo zinadai kuwa baadhi ya askari waliohusika
kwenye vurugu hizo si polisi halali wa jeshi hilo, bali ni vijana wa mtaani
ambao walivishwa sare kwa lengo la kuwadhibiti CHADEMA, ndiyo maana walikuwa
wakibabaika katika matumizi ya silaha.
Wakati huo huo, jeshi
hilo jana lilishindwa kumfikisha mahakamani askari polisi anayetuhumiwa
kufyatulia bomu lililomchanachana na kumuua mwandishi wa kituo cha Channel Ten,
Daudi Mwangosi.
Awali, taarifa za
mtuhumiwa huyo kupandishwa kizimbani zilizagaa kila kona; gazeti hili likapiga
kambi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa, lakini mtuhumiwa hakuletwa
mahakamani.
Jana gazeti hili
liliripoti taarifa za kukamatwa kwa siri na kuhojiwa kwa askari watano kati ya
saba akiwamo yule anayetuhumiwa kumuua marehemu Mwangosi.
Tanzania Daima
lilidokezwa kuwa askari wanaoshikiliwa kwa mahojiano zaidi ni wale walioonekana
kwenye picha mbalimbali za magazeti na mitandao wakimpiga marehemu huyo kabla
ya kumsababishia kifo.
Habari za ndani zilieleza
kuwa mtuhumiwa huyo wa mauaji hakuweza kufikishwa mahakamani kama
ilivyotarajiwa kutokana na kuendelea kutoa maelezo mbele ya mlinzi wa amani.
Chanzo cha taarifa
kilidai kuwa utaratibu huo wa kutoa maelezo ulianza juzi na huenda mtuhumiwa
atafikishwa mahakamani Jumatatu.
“Suala la mauaji ni
kubwa, si kama mashitaka ya mwizi wa kuku au karanga. Hivyo, juzi na jana yule
bwana alikuwa anaendelea kutoa maelezo yake kwa mlinzi wa amani. Sasa suala la
kukiri kuua au kutokuua litabaki katika moyo wake,” kilisema chanzo hicho.
No comments:
Post a Comment