Katika
hatua nyingine, serikali imeunda tume huru ya watu watano wa kada tofauti
akiwemo mtaalamu wa milipuko kuchunguza mauaji ya Mwangosi.
Licha
ya kuwepo kwa tume nyingine iliyoundwa na Jeshi la Polisi chini ya Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, tume ya serikali itafanya kazi kwa siku 30
na imepewa hadidu sita za rejea.
Mwangosi
aliuawa Septemba 2 mwaka huu kwa kitu kinachoaminika kuwa ni bomu
lililoelekezwa kwake na askari polisi waliokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa CHADEMA
waliokuwa kwenye ufunguzi wa tawi katika Kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi,
mkoani Iringa.
Akitangaza
kuundwa kwa tume hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi,
aliwaeleza waandishi wa habari aliokutana nao ofisini kwake jana kwamba hakuna
askari atakayenusurika iwapo itathibitika kuwa alishiriki kwenye mauaji hayo.
Dk.
Nchimbi ambaye muda mwingi wa mazungumzo hayo alijinasibu kuwa muumini mzuri wa
utawala wa sheria, aliwataja wajumbe wa tume hiyo kuwa ni wanahabari Pili
Mtambalike kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Theophil Makunga kutoka
Jukwaa la Wahariri (TEF) ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi
Communication inayochapisha magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti.
Wengine
ni Kanali Wema W. Wapo ambaye ni mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Naibu Kamishna wa
Polisi, Issaya Mungulu na Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mstaafu Pivel Ihema.
“Tume
hii itafanya kazi zake kwa uhuru na iwapo wataona wataalamu wa hapa ndani
wameshindwa jambo fulani wasisite kutueleza… serikali itautafuta utaalamu huo
kutoka nje ya nchi.
“Ninaomba
kuwahakikishia Watanzania kwamba askari yeyote atakayeguswa na tume hii
hatabaki salama, sikubaliani na dhuluma hasa ya vifo vya raia na sipuuzi
malalamiko yao,” alisisitiza Dk. Nchimbi huku akikwepa kujibu baadhi ya maswali
ya waandishi wa habari.
Kwa
mujibu wa waziri huyo, hadidu hizo za rejea zimetokana na taarifa iliyotolewa
na Jukwaa la Wahariri ambayo ni kujua chanzo cha kifo cha Mwangosi, ukweli
kuhusu uhasama kati ya polisi wa mkoani Iringa na waandishi wa huko.
Aliitaka
pia tume hiyo kueleza iwapo kuna orodha ya waandishi wa habari watatu mkoani
Iringa wanaowindwa na polisi, na usahihi wa nguvu ya polisi iliyotumika kuwadhibiti
wafuasi wa CHADEMA.
Jukumu
lingine la tume hiyo ni kueleza kwa kina utaratibu wa vyama vya siasa kukata
rufaa pale vinapohisi kutotendewa haki na kama kweli kuna uhusiano mbaya kati
ya polisi na vyama vya siasa hasa wapinzani.
Kwa
msisitizo Dk. Nchimbi alisema vurugu zilizofanyika Iringa ni matokeo ya
kuongezwa kwa muda wa kazi ya sensa ya watu na makazi ambapo Jeshi la Polisi
liliwazuia wanasiasa wote kufanya mikutano ya hadhara.
Hata
hivyo, waziri huyo alishindwa kutoa ufafanuzi wa mkutano wa uzinduzi wa kampeni
za uchaguzi mdogo huko Bububu visiwani Zanzibar ambapo Makamu wa Rais, Dk.
Gharib Bilali, alishiriki.
Waziri
huyo alisema serikali inajiuliza iwapo suala la sensa si muhimu kwa CHADEMA
kiasi cha kushindwa kuvumilia kwa siku saba za nyongeza.
Katika
hali inayoonyesha waziri kukosa hisia na kuguswa na ukatili wa jeshi lake,
aliilaumu CHADEMA kwamba ndiyo iliyosababisha mauaji hayo.
“Hivi
CHADEMA wanajisikiaje katika kipindi cha miezi mitatu kwenye mikutano yao
mitatu wamesababisha vifo vya watu watatu, familia za marehemu hao
zinawachukuliaje… unajua harakati za siasa hawakuanza wao, Mwalimu Nyerere
aliutafuta uhuru wa nchi hii kwa miaka saba bila kumwaga damu (Tangu 1954 hadi
1961) tena akiwa na serikali ya kikoloni,” alisema.
No comments:
Post a Comment