BARAZA la Wanawake la
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na lile la Wazee kwa pamoja
yamelaani vikali kitendo cha Jeshi la Polisi mkoani Iringa kumuua mwandishi wa
habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Naibu Katibu Mkuu wa
BAWACHA Taifa, Subira Waziri, alieleza kuwa wanalaani nguvu zote za mauaji
yanayoendelea nchini yakifanywa na Jeshi la Polisi ambao waliamini kuwa ni
walinzi wa wananchi na mali zao.
“Tulikuwa tunaliamini
Jeshi la Polisi, lakini kutokana na nguvu zinazotumika za kuua watu wasio na
hatia na kugeuka kuwa ndio wauaji wakubwa, hatuna tena imani nao,” alisema
Subira.
Aidha, BAWACHA wameeleza
kushangazwa na kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa ya kutishia
kuvifuta vyama vya siasa ambavyo vitasababisha vurugu na mauaji katika mikutano
yao.
“BAWACHA tunatambua kuwa
kauli hiyo inailenga CHADEMA ili kutekeleza dhamira ovu ya Tendwa aliyotumwa na
Serikali ya CCM. Tunamtaka msajili awaeleze Watanzania iwapo kauli yake hiyo
haitatumiwa serikali kupitia polisi ili kusababisha vurugu kwenye mikutano
yetu?” alihoji.
Nalo baraza la wazee wa
CHADEMA, limewataka wazee wote nchini kuungana pasipo kujali itikadi zao kwa
ajili ya kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete atoe tamko juu ya mauaji
yanayoendelea nchini hususan yale yanayofanywa na vyombo vya dola.
Taarifa ya wazee hao kwa
vyombo vya habari iliyosainiwa na Kaimu Katibu wa baraza hilo, Erasto Gwota,
ilisema kuwa imeshangazwa na ukimya wa Rais Kikwete ambaye ndiye mkuu wa nchi
hasa katika mambo mazito yanayoikabili nchi.
“Sisi wazee wa CHADEMA
tunawaomba wazee wote nchi tuungane tumwambie kijana wetu kuwa hali
inayoendelea haitaweza kuiacha nchi salama na yeye kama kiongozi wetu ana
jukumu la kuingilia kati na kutoa kauli yake ili iwe faraja na njia kwa
Watanzania,” ilisema.
Gwota alisema, baraza
hilo linatambua kuwa kuna mpango madhubuti ambao umeandaliwa na CCM kuwadhuru
wananchi wanaojitokeza katika mikutano ya vyama vya upinzani kwa lengo la
kuwatisha.
Alieleza kuwa serikali ya
CCM imeshindwa kusimama katika misingi iliyoachwa na Baba wa Taifa hayati
Mwalimu Julius Nyerere ya kukubali kukosolewa na kujisahihisha na badala yake
imeamua kutumia nguvu katika kujihalalisha kutawala.
No comments:
Post a Comment