Mo Blog: Shibuda umekuwa mwasiasa kwa
siku nyingi nini rai yako kwa viongozi wenzio wa kiasiasa.?
Shibuda: Napenda kutoa
rai kwa vyama na viongozi wa kisiasa ambavyo viko karibu 21 hapa Tanzania, la
kwanza kila chama kijifanyie tathmini, kinawajibika vipi kutekeleza mipango ya
kuendeleza amani na utulivu katika hii nchi.
Vinatekeleza mipango gani? Na kila
chama kifanye tathmini kijiuze mambo gani ambayo ni makosa kwa ustawi na
maendeleo ya nchi yetu inaoongozwa na kulindwa na tabia, mila na desturi za
mtanzania.
Vyama vya siasa viwe na wito unaoitwa ‘kwa maslahi ya umma’
na viongozi pia watekeleze wito unaoitwa kwa maslahi ya umma.
Mo Blog: Kwani una shaka na baadhi ya
vyama?
Shibuda:Vyama ambavyo
vina mdudu shetani anayeitwa ibilisi wa kujenga tafrani, migongano, misuguano
au vyama vinavyoitwa ‘chama kampuni’ kwa maslahi binafsi, havistahiki kuwa
sehemu moja wapo ya mbegu ya kuzalisha amani.
Hivyo watanzania tutafakari,
tusemezane, tutazame viwango vya kila chama, katika vyama 21 kwamba je? Tija ya
kila chama ni kwa kujenga ustawi na maendeleokwa jamii? Ili mwaka kesho
tusherehekee tena siku ya amani duniani.
Mo Blog: Lipi la msingi ungependa
kusisitiza kwa watanzania?
Shibuda: Jambo la
msingi ningependa kusisitiza ni kwamba watanzania tuanze kupambanua, tuanze
kutafakari, tuanze kusemezana kuwa hivi vyama 21 ni mapumulio dhidi ya
majinamizi na dhuluma ambazo taifa hili limekuwa nazo kwa muda mrefu dhidi ya
ustawi wa jamii?
Mimi ningependa kusisitiza ya kwamba
watanzania wenzangu tupokee vyama 21 kuwa ni changamoto ya mchakato wa kuwa
tuna sauti ya umma, yenye mti mmoja wenye mchipuo unaoitwa uzalendo, uaminifu
na utiifu kwa maslahi ya umma.
Matawi haya 21 yaonekane kweli
yanawakilisha maslahi ya umma.
Mo Blog: Lakini kwani una shaka na
lipi au na nani?
Shibuda: Lakini kama
kuna watu wamejiona tu ya kwamba wana mashinikizo na matatizo yao binafsi
wakasema kwamba tunaanzisha chama, wajue kuwa hiyo ni SACCOS ambayo haina
ustawi na maendeleo ya nchi bali wanatafuta michango, wanatafuta wapate ruzuku
wapate kuchangiwa kwa maslahi yao binafsi.
Chama lazima kitambulishe juhudi zake,
jitihada zake, dhamira, azma ya kuhakikisha ya kwamba wana wito wa kuwatumikia
watanzania kwa ari moja, nguvu mpya na kuhakikisha kweli ni uamsho kwa ustawi
na maendeleo ya Tanzania.
Mo Blog: Kwani unashaka kuwa nini
kitatokea yasipofanyika hayo unayoyasema?
Shibuda: Ninachokisema
ni kwamba la si hivyo tutakuwa na vyama vingi ambavyo ni sawasawa na nyumba
ambayo ina bati moja lakini limetoboka toboka na linaingiza mifereji ya maji
ndani ya nyumba, badala ya kupata sakafu iliyokavu, tunajikuta tunahamisha
vitanda kupeleka huku na kule lakini kila unakopeleka kitanda chako kunavuja,
hatutaki watanzania imani zao ziwe za kutangatanga.
Mo Blog: Kwa kumalizizia lipi neno
unaachia watanzania?
Shibuda: Kila
mtanzania apate mgutuko anapoona viongozi wa chama hawana maadili mema, hawana
wito, hawana vitendo, hawana kauli zinazoshabihiana na mtu mwenye wito wa
kutumikia au kama shekhe ama askofu hana vitendo vinavyoshabihiana na imani yake,
basi ujue huyo ni mtu tu sawa na chui aliyevaa ngozi ya kondoo ili aingie
kwenye zizi lakini dhamira yake ni kuwatafuna.
Tujitahadhari na watu ambao
wamekuja na jina la siasa lakini kumbe ni chui mla watu.
No comments:
Post a Comment