SIKU moja baada ya Mahakama Kuu Kanda
ya Dar es Salaam, kulitupilia mbali ombi la Shirika la Ugavi wa Umme nchini
(TANESCO) la kutaka izuie utekelezwaji wa ulipwaji wa fidia ya Kampuni ya
Dowans Tanzania Ltd, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amesema
mafisadi waliohusika ndio wabebeshwe hasara hiyo badala ya wananchi.
Juzi, mahakama hiyo, ilitupa ombi la
TANESCO lililokuwa likiomba itoe amri ya kuzuia utekelezwaji wa ukazaji wa
hukumu ya mahakama hiyo iliyoruhusu tuzo ya dola 65,812,630.03 za Marekani
iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara
(ICC) mwaka 2010 kwa Kampuni ya Dowans Hodlings SA (Costa Rica), sasa Dowans
Tanzania Ltd isajiliwe hapa nchini.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo
(CHADEMA), alitoa kauli hiyo jana kupitia taarifa yake aliyoisambaza kwenye
vyombo vya habari akisema kuwa serikali isitumie kizingizio cha uamuzi wa
mahakama kuharakisha mpango wa kulipa Dowans kwa fedha za walipa kodi wa
Tanzania.
Vile vile, Mnyika alisema kuwa ikiwa
serikali ya Rais Jakaya Kikwete imezidiwa na Dowans kwa sababu ya kujiingiza
katika mikataba mibovu, inapaswa kuwabebesha deni hilo wazembe, mafisadi na
waliokuwa wakihujumiana na kusababisha hasara hiyo.
“Serikali kupitia Waziri wa Nishati na
Madini, Prof. Sospeter Muhongo, anapaswa kueleza ni hatua gani ilichukua kutoka
TANESCO ilipowasilisha Mahakama ya Rufani taarifa ya kusudio la kupinga hukumu
iliyotolewa na Jaji Emilian Mushi, Septemba 28 mwaka jana ikiruhusu tuzo hiyo
isajiliwe,” alisema.
Aliongeza kuwa, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali naye anapswa kueleza ni kiasi gani cha fedha kilichotumika kwenye
kuendesha kesi za Dowans na IPTL mpaka sasa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya
mawakili wa TANESCO na makampuni binafsi yanayotuhumiwa kusababisha mzigo
mkubwa wa gharama za kesi ambazo serikali inashindwa.
“Ni muhimu umma ukafahamu kuwa kwa
mwaka wa fedha 2011/2012 pekee, jumla ya sh bilioni 10 zimetumika kwa ajili ya
gharama za kuendesha kesi hizo kwa kuilipa Kampuni ya Rex Attorneys na
makampuni mengine ambayo kwa nyakati mbalimbali yamekuwa yakiiwakilisha
serikali na TANESCO,” alisema Mnyika.
Alishauri kuwa hukumu ya juzi inapaswa
kuibua tena mjadala uliodumu kwa miaka minne, kuanzia mwaka 2008 tangu
yalipopitishwa maazimio 23 ya Bunge juu ya mkataba baina ya TANESCO na Kampuni
ya Richmond Development Company LLC ikiwamo kuhusu mkataba na Dowans.
Alisema katika mazingira hayo, Waziri
Muhongo anapaswa kueleza kwa umma ni mabilioni mangapi yamelipwa na TANESCO
mpaka hivi sasa kwa kampuni hiyo na nyingine.
“Kama hoja binafsi niliyoiwasilisha
ofisi ya Bunge mwaka jana kutaka utekelezaji wa maazimio yote yaliyobaki kuhusu
mkataba kati ya TANESCO na Richmond ingejadiliwa bungeni, hatua zaidi
zingechukuliwa kwa mafisadi na wahujumu uchumi waliohusika,” alisema Mnyika
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA.
TANESCO wanena
Wakati huo huo, TANESCO imesema kuwa
hakuna hukumu yoyote iliyotolewa na Mahakama Kuu kuamuru shirika hilo kuilipa
Dowans dola za Marekani milioni 96.
Taarifa iliyotolewa jana jioni na ofisi
ya uhusiano ya TANESCO, ilisema kuwa kilichoamriwa na Mahakama Kuu ni kwamba
Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza utekelezaji wa hukumu ya ICC, hivyo
mamlaka hayo yapo katika Mahakama ya Rufaa.
“Kwa sasa TANESCO imepeleka ombi la
kuzuia utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya ICC kwenye Mahakama ya Rufaa
Tanzania na hatimaye kuendelea na taratibu za kukata rufaa,” ilisema taarifa
hiyo.
No comments:
Post a Comment