To Chat with me click here

Monday, September 17, 2012

WAANDISHI IRINGA WAIGOMEA KAMATI YA NCHIMBI

KUTOKANA na tukio la mauji ya mwandishi wa habari wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, marehemu Daud Mwangosi, waandishi wa habari mkoani humo wamegomea kukutana na Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Hatua ya waandishi hao ilikuja baada ya Kamati hiyo kutoa taarifa ya kutaka kukutana nao katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma.

Kwa mujibu wa wanahabari hao, wanadai wamekosa imani na RC Ishengoma baada ya kushindwa kutoa ushirikiano katika msiba huo licha ya marehemu Mwangosi kufanya kazi kwa ujirani na ofisi hiyo.

Kamati hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Steven Ihema, mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, huku wajumbe wengine wakiwa ni mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishina wa Polisi, Isaya Mngulu, iliomba kukutana na wanahabari kwa taarifa kupitia baadhi ya viongozi wa chama hicho kwa kusambaza ujumbe mfupi wa maneno.

Aidha, Kamati hiyo ilihitaji kufanya mazungumzo na waandishi katika ukumbi wa ofisi ya RC Ishengoma, ambapo ujumbe huo ulisomeka: “Mkuu kesho Kamati ya Nchimbi inaomba kukutana na waandishi katika ofisi ya RC, toa maoni yako.”

Hatua hiyo iliwafanya wanahabari kurudisha ujumbe wa kugomea mkutano huo, kutokana na eneo la mkutano kudaiwa si sahihi kwa waandishi.

Waandishi hao waligomea kabisa mkutano huo, ambapo jioni kupitia taarifa walizopeana kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno walikutana katika ofisi yao kujadili hatua ya Kamati hiyo kutaka kuwakutanisha eneo hilo ambalo wao wanahisi si salama.

Moja kati ya sababu walizoainisha wanahabari hao za kugomea kukutana na Kamati hiyo ni pamoja na ofisi hiyo kuwa ni ya Serikali na mwandishi mwenzao ameuawa na Jeshi la Polisi ambalo ni Serikali.

“Hatuwezi kufanya upuuzi wa aina hiyo, sisi tumetoa tamko la kutofanya kazi na Jeshi la Polisi, lakini tumesitisha uhusiano wetu na mkuu wa mkoa huu.

“Ni mambo ya ajabu, hakuna asiyefahamu ushiriki wa Mwangosi katika shughuli za mkoa, mfano katika Kamati ya Sensa ya Watu na Makazi marehemu Mwangozi alikuwa katibu wa kamati hiyo.

“Pia sherehe za maandalizi ya wiki ya usalama ambayo kitaifa inatarajiwa kufanyika mkoani hapa Mwangosi alikuwa ni Katibu na Mkuu wa Mkoa ndiye mwenyekiti wake, lakini kinatushitua kitendo cha kushindwa hata kutuma sms ya pole. Jambo hili linatukosesha imani sisi kama waandishi, lakini pia tukitafakari jambo hili linatupa majibu tofauti,” alisema.

Kutokana na msimamo huo, Kamati hiyo ililazimika kubadili eneo la mkutano na kuwataka waandishi hao wa habari kufanya nao kikao leo kwa kukutana katika ukumbi wa MR. Hotel.

Hatua hiyo imekubaliwa na wanahabari na siku mbili nyuma RC Dk. Ishengoma aliambulia patupu baada ya kuomba kukutana na waandishi ambao waligoma kufika katika ofisi yake.

Kamati hiyo iliyoundwa kuchunguza tukio hilo la marehemu Mwangosi iliingia Mjini Iringa Jumanne wiki iliyopitam, kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mauaji hayo yaliyotokea Septemba 2, mwaka huu wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi za uandishi alipokuwa katika Kijiji cha Nyololo wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) kilipokuwa kikifungua matawi yake.

Toa Maoni yako kwa habari hii

No comments:

Post a Comment