MKANDA WA MAUAJI
WAWALIZA WAJUMBE
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemshukia Rais Jakaya Kikwete
kikieleza kushangazwa na ukimya wake kuhusu mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa
Kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, yaliyofanywa na Jeshi la
Polisi.
Akifungua
kikao cha Kamati Kuu cha dharura jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema chama hicho kimeshitushwa na kusikitishwa na
hali hiyo hasa ikizingatiwa kuwa rais ni Amiri Jeshi Mkuu na kwamba moja ya
chombo chake cha dola kimehusika katika tukio la kinyama la mauaji ya mwandishi
wa habari.
Alisema
inafahamika kuwa Rais Kikwete ni mwepesi kushiriki, kuhudhuria na kutoa salamu
za rambirambi katika misiba mbalimbali, lakini katika tukio hili la mauaji ya
kusikitisha na kutisha, amekuwa kimya kana kwamba hakuna jambo lolote
lililotokea ndani ya nchi anayoiongoza.
“Rais
yupo Kampala anasuluhusisha mgogoro wa Kongo wakati tuna migogoro ndani ya
jamii yetu,” alisema.
Alisema
katika siku za hivi karibuni kumeibuka migogoro mbalimbali hapa nchini ikiwamo
ya madaktari na walimu na kwamba sasa imeingia kati ya Jeshi la Polisi na
wananchi.
Mbowe
alisema katika hali hii ya huzuni na hofu kubwa miongoni mwa waandishi wa
habari na Watanzania wengi kutokana na kukithiri kwa mauaji ya raia
yanayofanywa na polisi, CHADEMA imeshangazwa na kushitushwa na matamshi ya baadhi
ya watendaji serikalini ambayo yanajaribu kuficha ukweli wa mauaji na uvunjaji
makusudi wa haki za binadamu.
Aliongeza
kuwa wakati watu wakiwa katika taharuki kutokana na mauaji hayo, ni jambo la
kushangaza kuona baadhi ya watendaji wa serikali wakiibuka na kutoa kauli
zilizojaa uchochezi na kuvunja amani.
Mbowe
alitaja moja kwa moja matamshi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John
Tendwa, aliyotoa hivi karibuni akitishia kukifuta CHADEMA kwa kile alichosema
ni kusababisha mauaji, kuwa ni za hatari na zilizolenga kuonesha kuwa mauaji
hayo yanatokana na mgogoro kati ya polisi na chama hicho.
Picha zawaliza wajumbe
Baadhi
ya wajumbe wa kikao hicho walishindwa kujizuia na kuangua kilio baada ya
kuonyeshwa picha za mnato na video za mauaji ya Mwangosi.
Picha
iliyowaliza wajumbe ni ile inayoonekana mabaki ya mwili wa marehemu Mwangosi
baada ya kupigwa bomu la machozi tumboni ambalo lilisababisha utumbo kutoka
nje.
Dk. Slaa afafanua SMS
Katibu
Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa inawezekana IGP, Said Mwema
na Waziri wa Mambo ya Ndani, Nchimbi ni mbumbumbu wa sheria kutokana na kudai
ujumbe wake mfupi wa maandishi (SMS) ni wa kichochezi.
Alisema
kama si mambumbumbu wa sheria, basi hawajui maana ya neno uchochezi na kuhoji
kama ujumbe huo ni wa uchochezi kwa nini mpaka sasa hawajamkamata.
“Nilimtumia
ujumbe ule IGP, lakini aliupeleka kwa Waziri Nchimbi maana yake anaomba ushauri
ambao pia waziri ameshindwa kumpa mpaka mauaji yametokea.
“Nchimbi
ameshindwa kutimiza wajibu wake, hivyo anatakiwa kujiuzulu kwa kushindwa
kuufanyia kazi ujumbe wa thadhari,” alisema.
CUF: Kuuawa mwandishi ni aibu kwa taifa
Chama
cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa tukio la kuuawa kwa mwandishi Mwangosi ni aibu
kwa taifa.
Akizungumza
jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Jangwani jijini
Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, Professa Ibrahimu Lipumba, alisema
kuwa mauaji hayo yamelichafua taifa zaidi na ni ishara ya serikali kuwafanya
wananchi waogope kueleza mambo yanayowaumiza.
“Kuuawa
kwa mwandishi wa habari kwa nchi isiyo na vita ni aibu kwa taifa na kuwafanya
wananchi wasiweze kupata habari zinazoendelea katika taifa lao,” alisema.
No comments:
Post a Comment