Jaji Sophia Akuffo |
JAJI
Sophia Akuffo kutoka Ghana amechaguliwa kuwa Rais wa Mahakama ya Haki za Binadamu
ya Afrika akichukua nafasi ya Jaji Gerard Niyungeko kutoka Burundi aliyemaliza
muda wake baada ya kutumikia nafasi hiyo kwa vipindi viwili tofauti.
Mwanamama
huyo ambaye alikuwa makamu wa rais wa mahakama hiyo katika muhula uliopita,
alichaguliwa kushika nafasi hiyo juzi mara baada ya kumalizika shughuli ya
kuwaapisha majaji wapya wawili: Ben Kioko kutoka Kenya na El Hadji Guissé
kutoka Senegal kwenye makao makuu ya mahakama hiyo yaliyoko jijini hapa.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari na afisa habari wa mahakama hiyo, Jean-Pierre
Uwanone, ilisema kuwa uchaguzi wa makamu wa rais ambao ulikuwa uende sanjari na
huo wa rais utafanyika baadaye ingawa hakutaja ni lini hasa.
Jaji
Akuffo aliteuliwa kuwa jaji wa mahakama hiyo mwaka 2006 kwa kipindi cha miaka
miwili kabla ya kuteuliwa tena kwa kipindi kingine cha miaka sita mwaka 2008
ambapo mwaka huohuo alichaguliwa kuwa makamu wa rais wa mahakama hiyo kwa
kipindi cha miaka miwili, mwaka 2010 alichaguliwa tena kuendelea na wadhifa huo
mpaka juzi alipochaguliwa kuwa rais wa mahakama hiyo.
Jaji
huyo kutoka mahakama ya juu ya Ghana (Supreme Court of Ghana) pia ni mjumbe wa
taasisi mbalimbali ikiwemo Kamati ya Ushauri ya Taasisi ya Elimu ya Masuala ya
Mahakama ya Jumuiya ya Madola (Committee of the Commonwealth Judicial Education
Institute).
Rais
aliyemaliza muda wake, Jaji Niyungeko (Burundi), alitumikia mahakama hiyo kama
rais kwa vipindi viwili tofauti kikiwemo kile cha 2006/08 ambapo alichaguliwa
tena kushika nafasi hiyo 2010/12 ambapo kwa mujibu wa taratibu za mahakama hiyo
nafasi hiyo huweza kushikiliwa kwa vipindi viwili tu.
Awali
uchaguzi huo ulitanguliwa na zoezi la kuwaapisha majaji wapya wawili, Kioko
kutoka nchini Kenya na Guissé kutoka nchini Senegal zoezi lililoshuhudiwa na
wageni mbalimbali ambapo kwa sasa mahakama hiyo itakuwa na majaji 10 kutokana
na Jaji Joseph Mulenga kutoka Uganda kufariki mwezi uliopita.
Kwa
mujibu wa mkataba wa uanzishwaji wa mahakama hiyo mwenye jukumu la kuteua
majaji wa mahakama hiyo ni mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika ambapo majaji hao
hutumikia mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka sita.
No comments:
Post a Comment