WABUNGE WALIOWEKA
SAINI KUMNG’OA PINDA KUKATWA NEC
Mwenyekiti wa CCM Taifa - Dr. Jakaya M. Kikwete |
PANGA
la vikao vya juu vya mchujo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), limenolewa.
Vikao
hivyo vya mwisho vya mchujo ambavyo vitaendeshwa na Mwenyekiti wake taifa, Rais
Jakaya Kikwete, vinatarajia kuanza rasmi Septemba 21 na 26.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa wakati vikao hivyo vikianza, CCM
imepanga mkakati mzito kukata majina ya baadhi ya wagombea uongozi ambao pia ni
wabunge ndani ya Bunge la Muungano.
Kundi
lingine la walengwa wa mkakati ule ni la viongozi wa CCM hasa wenyeviti wa
mikoa na wilaya waliokuwa wakiendeleza makundi na malumbano na kusababisha
kuporomoka kwa hadhi ya chama hicho.
Habari
zaidi kutoka ndani ya CCM, zinasema kuwa NEC imepanga kufanya maamuzi magumu ya
kuwakata baadhi ya wagombea waliokuwa wakiandamwa na tuhuma za ufisadi hata
kama watakuwa wamepita bila kupingwa au kupitishwa na vikao vya chini.
Tayari
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, mmoja kati ya makada wanaoandamwa
kwa tuhuma za ufisadi, amepita bila kupingwa wakati majeruhi mwingine wa
ufisadi, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, amepitishwa na vikao vya chini,
sasa wanasubiri idhini ya NEC.
Duru za siasa kutoka ndani ya CCM, zinasema kuwa wabunge wanaolengwa kwenye panga hilo ni wale waliokuwa kimbelembele kuikosoa serikali bungeni na kufikia hatua ya kusaini majina yao kwenye fomu zilizokuwa zikipitishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ili kupata saini 70 za kumng’oa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Tayari
athari za saini za kutaka kumng’oa Waziri Pinda zimeshaonekana kwa Mbunge wa
Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ambaye hivi karibuni alienguliwa katika kikao cha
mchujo wilayani na yeye kutahadharisha kama jina lake halitapitishwa NEC, ndani
ya CCM patachimbika.
Mkono
ambaye ni wakili maarufu nchini, aliwania nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazee taifa. Wengine waliowania nafasi hiyo ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, Joson
Rweikiza, Matha Mlata na Salum Chicago.
Waliopendekezwa
na vikao vya chini kuwania kiti hicho ni Abdallah Bulembo, Matha Mlata na
Halima Mamuya.
Kwa
upande wa Umoja wa Wanawake, waliopendekezwa ni pamoja na Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sofia Simba, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango
na Mayrose Kavura Majinge.
Mbunge
mwingine aliyekwishaenguliwa na vikao vya chini ni Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,
Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, ambaye alikuwa akichuana vikali na
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
“Tunaambiwa
wabunge wengi walioomba NEC watakatwa hasa wale waliotaka kumng’oa Pinda na
sababu ya pili ni kwamba wabunge wana nafasi kumi za NEC ndani ya Bunge, hivyo
hawana sababu ya kuwania NEC nje ya Bunge,” alisema mtoa habari wetu.
Mkono,
Nagu na wengine waliopendekezwa kuachwa na vikao vya chini, sasa wanategemea
kudra za NEC.
Mkoani
Shinyanga, taarifa zinasema kuwa mgawanyiko umetokea baada ya kuwapo taarifa
kwamba kuna mpango wa kulikata jina la mwenyekiti wa sasa wa CCM mkoa huo,
Khamis Mgeja.
Habari
zinasema kuwa mkakati huo unapangwa na vigogo wa CCM kutoka ofisi ndogo ya
makao makuu, Lumumba, jijini Dar es Salaam na kumhusisha mtoto wa kigogo.
Hatua
hiyo imedaiwa kuwa ni moja ya mikakati ya viongozi hao kupanga safu ya uongozi
mwaka 2015 ambapo Mgeja anatajwa kuwa mmoja wa watu anaopingana nao hivyo kuwa
kikwazo katika kufanikisha mipango yao.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wana CCM mjini hapa,
inadaiwa kwamba vigogo hao hivi sasa wanajitahidi kuwashawishi wajumbe wa vikao
vya juu ili kuhakikisha jina la Mgeja linakatwa na linabakizwa la mtu ambaye ni
chaguo lao.
Yapo
madai kwamba mkakati wa vigogo hao unaungwa mkono na baadhi ya wabunge wa CCM
mkoani Shinyanga ambao hawamuungi mkono Mgeja.
Baadhi
ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamewaeleza waandishi wa habari mjini
Shinyanga kwamba tayari kuna vikao vingi vya usiku vinavyofanywa na mawakala wa
vigogo hao kwa lengo la kuhakikisha Mgeja hachaguliwi hata kama NEC itakuwa
imerejesha jina lake.
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida mmoja wa wagombea ambaye alipata fununu za jina lake
kupendekezwa kuwa miongoni mwa wagombea nafasi ya uenyekiti wa mkoa, aliamua
kufanya sherehe kubwa katika moja ya baa eneo la Lubaga ambako alisikika
akitamba kwamba yeye ni chaguo la Rais Jakaya Kikwete.
No comments:
Post a Comment