To Chat with me click here

Saturday, September 22, 2012

UASI WANUKIA CCM


VIGOGO WATISHANA WAZIWAZI

HALI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imevurugika, ikiwa zimebaki siku mbili tu kabla ya kuanza kwa vikao vya Halmashauri Kuu (NEC), hapo Septemba 24, kwa ajili ya kuteua majina rasmi ya watakaowania nafasi za uongozi wa juu wa chama hicho.

Habari za kuaminika zimebainisha kuwa, uhasama mkubwa umezikumba kambi mbili kubwa za wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, wale wa mtandao unaoaminika kukubalika na mmoja wa viongozi wa juu wa chama hicho, na ule unaojinasibu kuwa ni wapambanaji wa ufisadi.

Uchunguzi wa Tanzania Daima kwa wiki nzima, umebaini kuwepo kwa vikao vingi vya siri baina ya makundi hayo, huku kundi moja likiwa limejizatiti kuhakikisha kuwa majina ya wagombea kutoka kundi jingine hayapitishwi.

Hata hivyo, katika hatua inayoonesha hali mbaya ya mahusiano baina ya wajumbe wanaounda uongozi wa juu wa CCM ngazi ya taifa, mmoja wa wajumbe ambao wameomba tena kuwania nafasi ya NEC na ambaye anashikilia nyadhifa kadhaa za chama na serikali, alimtolea maneno makali katibu wa CCM wa mkoa mmoja (jina linahifadhiwa) baada ya kukutana uso kwa uso katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam juzi majira ya jioni.

Kigogo huyo alisikika akimwonya katibu huyo kukaa mbali naye na kumwagiza akawaambie waliomtuma kufuta mara moja mbinu chafu walizoziandaa dhidi yake, la sivyo angelazimika kuanika kile alichokiita uchafu wote anaoujua dhidi yao kwa Watanzania.

Kadhalika kiongozi huyo alikaririwa akisema kuwa haoni hasara tena ya kuendelea kuwa ndani ya chama kinachoongoza kwa majungu, fitina na chuki, huku akificha siri nyingi za uongo wa viongozi wengi.

“Kawaambie, tena nakutuma ukawaambie hao waliokutuma, sitaki kufuatwa. Iwe mwanzo na mwisho, vinginevyo nitawaanika kwa Watanzania, ingawa najua mwenyekiti atasikitika.

“Msione nimenyamaza, mkadhani sijui kile mnachokifanya dhidi yangu. Jaribuni kufuta jina langu, muone kama nanyi sitawaanika kwa Watanzania, wawajue mlivyo wachafu na sijui mtaweka wapi nyuso zenu,” alisikika akisema kabla hajapanda gari lake na kuondoka.

Wakati hayo yakijiri, kauli iliyotolewa na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, mapema wiki hii kwamba hatakubali jina lake likatwe bila maelezo, imekikoroga vibaya chama hicho, na kuna taarifa kwamba kundi kubwa la viongozi kutoka mkoani Mara, linajiandaa kuchukua maamuzi magumu, ikiwa kikao cha Halmashauri Kuu kitabariki kuondolewa kwa jina lake.

Habari kutoka mjini Musoma, zimedai kuwa hatua yoyote ya kukatwa kwa jina la mbunge huyo na mwanasheria maarufu hapa nchini, itakuwa mwanzo wa anguko kubwa la CCM mkoani humo hata kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Mkono hata hivyo, hakuwa tayari kuzungumzia jambo hilo alipotakiwa kufanya hivyo na gazeti hili, wala kukiri ama kukana kujua juu ya kuwepo kwa kundi la viongozi wanaomshabikia, waliojiandaa kuchukua maamuzi magumu ikiwa jina lake halitapitishwa.

Mbunge huyo alikaririwa akieleza kushangazwa kwake na kukatwa kwa jina lake katika ngazi ya mkoa, na kudai kwamba hatakuwa tayari kukubali kirahisi hali hiyo, bila kuambiwa kosa lake katika ulingo wa siasa ndani ya chama hicho lililosababisha hali hiyo.

Mtifuano mwingine uko katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu ambako mahasimu wakubwa wawili wanachuana.

Mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Dk. Raphael Chegeni inadaiwa anafanyiwa njama za kuenguliwa jina lake ikidaiwa kuwa ni kutokana na uhasama mkubwa alionao dhidi ya mbunge wa sasa, Dk. Titus Kamani.

Wawili hawa wameshitakiana mahakamani kwa tuhuma za kutaka kuuana, zinazomkabili Dk. Kamani. Hali hiyo inakuja huku jina la Dk. Chegeni likidaiwa kukatwa na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mwanza kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wilayani Busega, Samuel Ngofilo, alikiri kuwepo kwa njama hizo alizoziita chafu zinazolenga kumchafua Dk. Chegeni ili asipitishwe na NEC kugombea wilayani humo.

Dk. Chegeni pamoja na wagombea wengine watatu, ambao ni Kashen Fanuel, Miknes Mahela na Amos Onesmo, ndio wanawania u-NEC kupitia Wilaya ya Busega, katika Mkoa mpya wa Simiyu.

“Kuna njama chafu zimeanza kufanywa kwa lengo la kumchafua Dk. Chegeni ili asipitishwe kugombea NEC katika wilaya yetu ya Busega. Kauli ya vijana Busega tunaka NEC itende haki. Dk. Chegeni ni mchapa kazi hodari na CCM wanalijua hili.

“Kwa kutambua uchapakazi, ushawishi na uhodari wa kujenga na kutetea hoja kwa maslahi ya chama na jamii alionao Chegeni, ndiyo kilichotusukuma tumchukulie fomu ya kugombea NEC. Sasa kama NEC watakata jina lake, tuko tayari kuchukua maamuzi magumu. Hatuwezi kusema kama tutaenda Peoples au la, maana bado mapema mno,” alisema.

Aidha, Ngofilo alimtuhumu Dk. Kamani kwa madai ya kuandika barua kwenda kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, akiomba jina la Dk. Chegeni lisipitishwe kwenda ngazi ya taifa.

“Siasa za namna hii sisi vijana wa Busega hatuzitaki. Tunachotaka ni kujenga chama chetu kwa kuwa na viongozi makini, hodari na imara katika kupigania maendeleo ya chama na Watanzania. Tunaisihi sana NEC ipuuze uzushi wa aina yoyote ile, na ituletee majina ya watu wanaokubalika kijamii,” alisema Ngofilo.

Alipopigiwa simu yake ya kiganjani juzi ili atoe ufafanuzi juu ya tuhuma hizo, Dk. Kamani alipokea simu na kusema kwa kifupi: “Baadaye” kisha akakata simu.

Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms), akiombwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, alikaa kimya hadi tunakwenda mitamboni.

Kwa upande wake, Dk. Chegeni alipotafutwa kwa simu yake ya kiganjani ili azungumzie suala hilo la kuundiwa njama chafu kwa lengo la kumchafua, hakuweza kupatikana ambapo baadaye taarifa zilidai kwamba yuko safarini nchini Colombia.

Kutoka mjini Kahama, habari zinasema kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, na Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), jana waliungana na kushiriki katika hafla ya kuaga wanafunzi wa darasa la saba katika shule binafsi ya Kwema Modern.

Sitta ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, inaelezwa kuwa alialikwa ikiwa ni moja ya mikakati ya pamoja na Lembeli, huku kukiwa na taarifa kwamba majina ya wawili hao ni miongoni mwa yale yatakayofyekwa kuwania nafasi ya ujumbe wa NEC.

Duru za kisiasa zimebainisha kuwa wawili hao sasa wameamua kushikamana kwa dhati dhidi ya hila zinazoonekana kufanywa na viongozi wenzao ndani ya CCM, ambazo inadaiwa zimechangiwa na kile kinachoelezwa kauli zao tata ambazo zimekuwa mtaji kwa vyama vya upinzani.

Wakati Sitta akikwaruzana na wenzake ndani ya CCM, Lembeli amekuwa na ‘ugomvi’ wa muda mrefu na Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Hamis Mngeja.

Imeelezwa kuwa wawili hao, wanawania uenyekiti wa chama hicho mkoa.
Jijini Dar es Salaam, kumezuka tafrani kutoka kwa baadhi ya wagombea wanaodai kuwa majina yao yalienguliwa na kuwekwa mengine kwa maslahi binafsi ya makundi katika chama hicho.

Katika uchaguzi uliofanyika mwanzoni mwa wiki hii, kulizuka purukushani kubwa zilizotaka kusababisha kuchapana makonde kutokana na kuwepo kwa mizengwe katika uteuzi wa nafasi za uongozi.

“Jina la kada aliyewahi kuwa Katibu wa Uhamasishaji Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam na aliyewahi kuwa diwani katika Kata ya Ubungo liliondolewa kutokana na kushinikiza arudishwe Diwani wa Makurumla, Rajab Hassan,” kilisema chanzo chetu.

Kwa maelezo ya chanzo hicho, katika vikao vyote vya mkoa, sekretarieti, kamati ya maadili ya mkoa na kamati ya siasa ilimpendekeza kada huyo aliyeondolewa kwa kuwa ana sifa zote, lakini Mwenyekiti wa Mkoa wa CCM, John Guninita, alishinikiza jina la kada huyo kukatwa kwa maslahi binafsi ya makundi Mkoa wa Dar es Salaam.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa, hata katika nafasi ya mkutano mkuu wa taifa, kulikuwa na matatizo kwa kuwa baadhi ya wajumbe walikuwa na maslahi yao binafsi.

Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abilahi Mihewa, alisema kuwa anadhani kuwa wale wanaolalamika hawajui utaratibu wa vikao vya chini kuwa vinashughulika na matengenezo.

Mjini Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ametishia kuwazuia waandishi wa habari watakaotangaza habari ambazo hazijathibitishwa na uongozi wa juu, kuingia ndani ya viwanja vya makao makuu ya chama hicho.

Nape akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa wamewaelekeza walinzi wao kutoruhusu waandishi wa chombo kilichoandika habari za barabarani kuingia ndani ya jengo hilo.

Alisema kwa muda wa siku tatu wamekuwa na kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ambapo kazi yake kubwa ni kupokea taarifa ya mapendekezo kutoka wilayani na mikoani na kuziunganisha pamoja na kuziboresha.

Alisema nafasi ambazo ziliombwa na zitajadiliwa na vikao hivyo ni wajumbe wa NEC kupitia wilaya na wale wa Zanzibar na Tanzania Bara, nafasi ya uenyekiti, katibu uenezi na uchumi wa mkoa na wagombea kutoka jumuiya mbalimbali za chama hicho.

No comments:

Post a Comment