‘Mauaji Ya Waandishi Na Wananchi Yatavuruga Mchakato Wa Kupata Katiba
Mpya Tanzania!’’
JUKWAA LA
KATIBA TANZANIA tumepokea taarifa za kuuawa kinyama kwa Mwandishi Daudi
Mwangosi wa Channel 10 na Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa Habari mkoani
Iringa (IPC) kwa mshtuko na masikitiko makubwa. Kama ilivyokwishaelezwa na
wengi, kifo cha mwandishi huyu ni cha kwanza cha aina yake katika tasnia ya
habari nchini na kinatishia si tu uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa habari kwa
ujumla wake, bali pia kifo hiki na vingine vya siku za karibuni vinauweka
mchakato wa Katiba Mpya njia panda.
Vitendo vya
mauaji ya raia vinazidi kushamiri siku hadi siku. Wapo wananchi wanaouawa na
watu wanaoitwa wenye hasira kali kwa tuhuma za uhalifu. Wapo raia wanaouliwa na
majambazi na wahalifu wengine kwa sababu ya ulinzi duni katika maeneo
wanayoishi. Aidha, wapo pia wananchi wanaopoteza maisha yao kila siku kwa
tuhuma za kwamba ni wachawi. Ukiacha hao, idadi kubwa ya watanzania wanaishi na
ulemavu wa ngozi wamepoteza maisha kwa kukatwa viungo au kuuliwa kabisa kwa
imani za kishirikina. Hali sasa imefikia kuwa mbaya hadi kuna watanzania
wanajisikia salama zaidi wakiwa mwituni kuliko majumbani. Yote haya
yanasikitisha sana kwa ujumla wake! Haki ya kuishi inayowekwa na kulindwa na
ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza kuingia dosari
katika Tanzania.
Ukiacha mauaji
yanayofanywa na watu wasiojulikana au miongoni mwa raia, yamekuwepo pia mauaji
yanayozidi kuongezeka ya raia yanayofanywa na wawekezaji au matajiri nchini.
Zipo kesi kadhaa za mauaji ya namna hii. Hayo nayo yamekuwa yakitokea kwa
sababu ya ulinzi mdogo ambao wananchi wanao kutoka kwa vyombo vya ulinzi na
usalama nchini. Jeshi la Polisi, ambalo ndio lenye dhamana ya kulinda watu na
mali zao haliwezi kukwepa lawama katika aina zote hizo za mauaji. Itakumbukwa
pia kuwa ajali za magari, mabasi na meli zinagharimu sana maisha ya watanzania
katika siku za karibuni. Kwa kiasi fulani, hata kukithiri kwa ajali hizi nako
kunahusishwa na mwenendo mbovu wa usimamizi wa vyombo vya usafiri unaofanywa na
idara mbalimbali za serikali ikiwemo kikosi cha usalama barabarani. Roho za
watanzania zinazidi kupotea kutokana na udhaifu mkubwa unaosababishwa na rushwa
na mambo mengine ya ukosefu wa maadili katika vyombo vya usimamizi wa haki.
Mauaji ya raia
yanayofanywa moja kwa moja na askari wa Jeshi la Polisi nayo yanazidi
kuongezeka sana kiasi cha kutishia amani na utulivu wa nchi yetu. Aidha, mauaji
yanayohusishwa na siasa nayo yanazidi kuongezeka na kuzidisha chuki ya kisiasa
ambayo ni mbaya sana kwa ustawi wa nchi yetu. Kwa mfano katika miezi ya
Karibuni, kumekuwepo matumizi ya nguvu kuzidi kiasi kwa raia wanaokuwa
wakipanga na kufanya maandamano au mikusanyiko yenye lengo la kujadili au
kupinga jambo fulani. Matokeo yake, kumetokea majeruhi na mauaji ambayo
yamesababishwa na vurugu ambazo zinatokana na Jeshi la Polisi kudhibiti vitendo
halali vya wananchi. Kwa sababu hiyo, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tunatoa wito
ufuatao kwa Jeshi la Polisi na idara nyingine za serikali zenye dhamana ya
kulinda usalama wa raia, mali na mipaka ya Nchi yetu:
1.
Jeshi la Polisi
liache kutumia nguvu kuzidi kiasi katika matukio yote ya kulinda mikutano na
matukio ya hadhara. Tujuavyo sisi, Jeshi la Polisi linalotumia risasi za moto,
mabomu ya kivita, maji ya kuwasha na gesi ya kutoa machozi dhidi ya raia ambao hawajabeba
hata fimbo za kuchungia mifugo. Ni Jeshi lisilojiamini na linaloonesha woga wa
ajabu.
Kwa hadhira kama za Nyololo, Morogoro, Mbeya, Dar es Salaam na
nyinginezo miezi ya Karibuni, Jeshi la Polisi lingeweza kuwatuliza wananchi kwa
kutumia filimbi tu. Matumizi ya nguvu na kumwagia maji ya kuwasha hata wazee
wastaafu wanaodai haki zao inaweza kuwa ndio laana inayopelekea Polisi kusikia
furaha kuua kila mara. Ipo kanuni ya kimataifa inayowataka Polisi kutumia nguvu
kidogo sana inayolingana tu na nguvu ya umma wanaokabiliana nao katika kutuliza
ghasia.
2. Wakati huu wa
mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Tanzania na hata baada ya hapo, Jeshi la
Polisi lijiepushe kuingilia shughuli za Kisiasa kwa kuziunga mkono au
kuzivuruga. Mikusanyiko mingi ambayo imepelekea mauaji wakati polisi ikijaribu
kuivunja ni matukio yaliyolenga kupata majibu ya kisiasa na siyo ya kipolisi.
Wajibu wa Jeshi la Polisi katika wakati kama huo ni kulinda na kuwezesha
wananchi husika kueleza madai yao kwa uhuru na bila kuvurugwa na kundi jingine
lolote la watu wasiopendezwa na madai ya kundi husika. Tabia inayozidi
kushamiri ya Jeshi la Polisi kutaka kujibu au kuzima hoja za Kisiasa au
kiuchumi kwa mtutu wa bunduki, mabomu, maji ya kuwasha na virungu ni tabia ya
Jeshi kutaka kuingilia kazi isiyo yake na ndio maana inawashinda. Aidha, kama
Polisi wangekuwa ni wataalam wa Siasa, wangegundua kuwa wanachokifanya ni
kuahirisha matatizo na si kuyatatua!
3.
Jeshi la Polisi
na vyombo venye dhamana ya ulinzi vijitambue upya kuwa vina wajibu wa kulinda
raia, mipaka na mali zao si vinginevyo. Mauaji yanayoendelea nchini ni uporaji
wa haki ya kuishi na haki nyingine nyingi chini ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar. Aidha, Jeshi la Polisi na serikali kwa
ujumla wana wajibu wa kuhakikisha na kudumisha ustawi wa wananchi kwa mujibu wa
ibara ya 8 (1) (b) na hawana mamlaka ya kuua raia. Ikumbukwe kuwa mamlaka yote
kikatiba katika Tanzania yako kwa wananchi na serikali pamoja na Jeshi lake la
Polisi watapata madaraka na mamlaka hayo kutoka kwa Wananchi. Nani amewapa
Polisi mamlaka ya kuua watanzania? Nani amewapa Jeshi la magereza mamlaka ya
kuwapiga na kumwaga damu za Waandishi? Nani amewapa askari wanyamapori mamlaka
ya kupiga risasi hovyo na kuua ng’ombe mbele ya wenye mali yao?
4. Athari za
matukio ya mauaji na fujo zinazosababishwa na Jeshi la Polisi kutawanya
waandamanaji au mikusanyiko mingine ni kubwa sana katika kuathiri vibaya hamasa
ya wananchi kwenye Mchakato wa Katiba. Mpaka sasa, tayari watu wengi wameingia
wasiwasi na wameamua kutoshiriki mikutano ya kutoa maoni ya Katiba
inayoendeshwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini. Endapo Jeshi la Polisi
halitaacha kuua na kutishia raia kwa kila wanachokifanya, mchakato wa Katiba
utavurugika kabla Katiba mpya haijapatikana. Kwa mwenendo wa sasa, Jeshi la
Polisi litakuja kupiga mabomu na kuua hata wananchi watakapokuwa katika
Mabaraza ya Katiba wakijadili na kupinga baadhi ya vipengele vitakavyoingizwa
katika rasimu ya Katiba. Pia, itafika wakati wananchi watataka kuandamana kwa
amani kuunga mkono au kupinga mambo Fulani katika Katiba. Kwa hali ilivyo,
Jeshi la Polisi litaona hiyo ni fursa ya kutumia mabomu na risasi kuzuia
wasiseme wanayotaka kusema. Hii ni hatari kubwa sana!
5. Mikusanyiko,
maandamano na shughuli za mikutano ya Siasa ni matendo halali na haki ya kila
mtanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977 ibara ya 8, 20 na
21. Suala la kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la
Polisi ni suala la kuwajulisha tu kwa lengo la kuwaweka tayari endapo
kutahitajika msaada wa Jeshi la Polisi wakati wa shughuli kama hiyo. Tabia
iliyoota mizizi ya Polisi kujiona kama wamepewa taarifa ili watoe au kukataa
kibali ni uelewa finyu wa Katiba na sheria za Nchi. Ipo haja ya kuongeza uelewa
wa wasimamizi wetu wa sheria ili wawe na uelewa mpana wa sheria na ibara za
Katiba wanazozisimamia badala ya kujiona kama wana wajibu wa Msajili wa vyama
vya Siasa wa kuratibu shughuli za vyama. Mikutano, mikusanyiko, mihadhara,
maandamano na mijadala ni haki ya Kikatiba ya Kila mtanzania binafsi na kwa
makundi.
Kwa kuwa haki
ya kuishi iliyoporwa kwa Mwandishi Daudi Mwangosi ndio haki kubwa kuliko zote,
JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tunataka jambo hili lisiishie kuunda Tume za
uchunguzi pasipo kufanyia kazi mapendekezo yake. Aidha, kwa kuwa uchunguzi
unaofanywa hauhusiani na kilichomuua ndugu Mwangosi wala kundi gani limemuua,
tunapendekeza busara itumike kwa viongozi wa Jeshi la Polisi, kuanzia Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Iringa kuachia ngazi ili kupisha uchunguzi huru wa Tume
itakayoundwa na Mheshimiwa Rais ikihusisha na kuongozwa na mhimili wa Mahakama.
Taarifa ya uchunguzi ipelekwe Bungeni na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya
kujadiliwa na ushauri wa kibunge. Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi tunaitamka rasmi kuwa batili kwa kutumia kanuni ya sheria za kiasili
inayosema kuwa mtu au kundi hawezi kuwa hakimu wa kesi inayomhusu mwenyewe.
Bila kufanya hivyo, tunapata wasiwasi kama Tume ya namna hiyo inaweza kufanya
kazi yake kwa uhuru. Kuachia ngazi kwa Kamanda wa Polisi mkoani Iringa kutakuwa
ishara kuwa Jeshi la Polisi linahitaji kuwa makini zaidi katika kufanya kazi
yake ya kulinda amani, mali na maisha ya watanzania. Kwa sasa, zipo hisia kuwa
Jeshi la Polisi lipo juu ya sheria na Katiba, jambo ambalo tunapenda kulikanusha
vikali!
Mwisho,
tunapenda kutoa rai kwa serikali kutangaza rasmi kuwa itachukua jukumu la
kutunza, kusomesha, kulisha na kuhudumia familia aliyoiacha Daudi Mwangosi
kuanzia sasa kwa muda wa miaka 20 watakapoweza kujitegemea wenyewe. Itakuwa ni fedheha
kuiona familia aliyoianzisha Marehemu Mwangosi ikisambaratika kwa sababu kichwa
cha nyumba hiyo kimesambaratishwa na bomu la Polisi ambalo kodi yake Mwangosi
ilichangia kulinunua.
Kufikia hapa,
tunapenda kutangaza rasmi kuwa msiba huu ni msiba wa KIKATIBA na tunaomba
ufahamike hivyo kwa umma wote wa watanzania na kote duniani.
Mungu ailaze
roho ya Marehemu Mwanahabari Daudi Mwangosi mahali pema peponi – Amina!
Imetolewa na
kusainiwa kwa niaba ya JUKWAA LA KATIBA TANZANIA,
Deus M Kibamba
Mwenyekiti
Alhamis,
06 Septemba 2012
No comments:
Post a Comment