ALIYEKUWA Katibu Mwenezi wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) Kata ya Mjimwema katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea,
Magdalena Gama, amejivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kuona kimekosa mwelekeo.
Gama alitoa kauli hiyo jana kwenye
Ofisi ya CHADEMA, Kata ya Mjimwema alipokuwa akikabidhiwa kadi mpya na
Mwenyekiti wa chama hicho, Tawi la Pachanne, Swedi Milanzi.
Alisema ameamua kuihama CCM baada ya
kuona baadhi ya viongozi wake, wamekuwa na tabia ya ubinafsi na kuonekana ni
mali yao binafsi.
Alisema amejiunga na CHADEMA kwa kuwa
ndicho chama pekee chenye sera nzuri zenye tija kwa Watanzania wote bila kuwepo
matabaka.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa ya chama hicho, Samweli Chale, alisema kitendo alichokifanya Gama
ni cha kiungwana, kwani CCM imejaa fitina hasa kwa wale viongozi wanaoonekana
kwa jamii kuwa makini.
Chale
ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Bombambili, alisema msimamo wa
chama hicho ni kuboresha zaidi maendeleo mbalimbali ya wananchi na kina malengo
ya kuhakikisha kinashika dola kuanzia ngazi ya uongozi wa serikali za mitaa,
vitongoji na vijiji na kwamba hakuna chama kingine chenye kipaumbele zaidi ya
CHADEMA.
Tanzania Daima
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment