Mbunge wa Viti Maalum-CUF, Mkoa wa Tanga Mhe. Amina Mwidau |
Wingi
wa wabunge kutoka Chama cha Mapinduzi katika Bunge la Tanzania, umechangia kwa
kiwango kikubwa kukwama kwa maendeleo ya nchi.
Mbunge
wa Viti Maalum, Amina Mwidau (CUF), amesema hayo juzi wakati akikabidhi mashine
ya kusukumia maji yenye thamani ya sh milioni 5, kwa wananchi wa kijiji cha
Mwera katika wilaya ya Pangani mkoani Tanga ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa
ahadi zake kwa wakazi hao.
Alisema
kukosekana kwa wabunge wengi wa upinzani, kumewafanya wabunge wa CCM kuyaacha
mambo yaende jinsi yalivyo na hivyo kusababisha nchi kuwa na matatizo mengi.
“Leo
nchi imekuwa na matatizo kila kona kutokana na kukosekana wabunge wa kweli
ambao wana uchungu wa kupigania mgao wa rasilimali ulio sawa kwa wananchi pia
kuwatetea wananchi na ninayasema haya mchana kweupe, idadi ya wabunge wengi wa
CCM imekuwa ni kikwazo kwetu sisi wapinzani.
“Hata
nanyi wananchi wa Mwera mnalitambua hilo, na hata mbunge mwenzangu wa CCM wa
jimbo hili hana muda wa kurudi tena tangu mlipomchagua hata leo hii mna tatizo
la maji kutokana na mota ya kusukumia maji kuungua na hana habari nanyi.
Amina
alisema ili kupambana na mfumo huu mbovu ulioandaliwa na CCM kutokana na sera
zake mbovu Watanzania wanahitaji kujenga nchi kwa kuwa na viongozi jasiri kama
Profesa Lipumba ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipigania ustawi na haki za
Watanzania.
Mbunge
huyo aliwataka wananchi hao kukiunga mkono chama chake ili kiweze kujenga
demokrasia na ukombozi wa kweli nchini.
Alisema
amefikia hatua hiyo baada ya kutambua kero kubwa ya maji inayowakabili wananchi
hao, ambapo hicho kilikuwa kipaumbele chake katika kampeni zake wakati
alipokuwa akiomba nafasi hiyo.
Amina
aliwaasa wananchi hao, kuhakikisha wanakikataa Chama cha Mapinduzi (CCM),
katika masanduku ya kura itakapofika mwaka 2015 ili Bunge liwe na wabunge wengi
kutoka vyama vya upinzani watakaoweza kuwakomboa wananchi kutoka kwenye
umaskini uliokithiri, uliosababishwa na chama hicho.
“Ninakabidhi
mashine hii yenye thamani ya zaidi ya sh milioni 5, ili kutatua kero ya maji
katika kijiji hiki cha Mwera, ninajua uchungu kwani wanaopata taabu ni wanawake
wenzangu na watoto ambao hutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya
shughuli za uzalishaji,” alisema Amina.
No comments:
Post a Comment