To Chat with me click here

Thursday, September 20, 2012

POLISI WAVAMIA KIJIJI USIKU WA MANANE


NI KWA AMRI YA DC, WAPIGA MABOMU, KUPORA MALI

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha, kwa agizo la Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, wamevamia kijiji usiku wa manane, kupiga mabomu na kupora mali.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia juzi kuanzia saa nane hadi saa kumi katika Kijiji cha Kisangiro, kwa kile kilichodaiwa kuwa walikuwa wakisaka silaha za moto zinazodaiwa kumilikiwa na wakazi wa jamii ya Kisonjo, maarufu kama Watemi.

Uvamizi huo umefanyika ikiwa ni siku chache tangu DC huyo, Elias Wawa Lali, kufanya mkutano na viongozi wa kimila wa jamii hiyo kijijini hapo siku ya Jumamosi wiki iliyopita.

Katika mkutano huo, aliwatisha watu wa jamii hiyo akiwataka wasalimishe silaha hizo za kivita aina ya SMG na SAR pamoja na mifugo aliyodai waliwanyang’anya wafugaji wa Kimasai hivi karibuni wakati wa vurugu za kugombania ardhi.

Wawa Lali alijigamba mbele ya wazee hao kuwa amekwisha kuanza kufunga mizigo kwa ajili ya kuondoka pamoja na familia yake, hivyo akatoa siku tatu agizo lake hilo liwe limetekelezeka, vinginevyo angewaamuru FFU wavamie kijiji hicho kwa nguvu kusaka silaha hizo na mifugo.

Wakizungumza kwa hofu jana, baadhi ya wakazi hao wakiwemo wazee, walisema kuwa walivamiwa usiku wa manane na askari hao waliofika eneo hilo wakiwa na magari mawili na kuanza kupiga mabomu, kuvunja nyumba na kupora mali mbalimbali.

Walisema kuwa hadi jana waliweza kubaini nyumba 31 zilizobomolewa, yakiwemo maduka na mali mbalimbali zikiwa zimeporwa, huku vijana watano wakikamatwa na askari hao na kushikiliwa katika Kituo cha Polisi Loliondo.

“Kwenye mkutano wetu na mkuu wa wilaya, tulikubaliana atupe siku zaidi ili tufanye uchunguzi dhidi ya madai yake kuwa baadhi yetu wanamiliki silaha za moto na kama zitapatikana tutazisalimisha, lakini tumeshangazwa kuona tunavamiwa usiku na askari wakipiga vijana wetu na kupora mali,” alisema mmoja wa wazee hao.

Wazee hao ambao wanamlalamikia mkuu wa wilaya hiyo wakidai anaegemea upande wa Wamasai katika mgogoro huo, walisema kuwa tukio hilo la juzi limesambaratisha kijiji, kwani vijana na watoto wamekimbilia kusikojulikana wakihofia mabomu ya polisi.

“Mpaka sasa hakuna silaha waliyoipata wala mifugo, zaidi wameleta hofu kijijini kwetu, watoto wamekimbia hawaendi shule, hatujui wako wapi. Askari wamekuja kuvunja nyumba zetu na kupora, serikali ipo wapi na huu ni utawala bora upi?” alihoji mmoja wa wazee hao kwa hasira.

Kwa muda mrefu sasa jamii hizi mbili za Wasonjo na Wamasai wa ukoo wa Loita, zimekuwa kwenye mgogoro mkubwa wa ardhi kiasi cha kusababisha vurugu zilizopoteza maisha ya watu, kujeruhi na mifugo kadhaa kupotea.

Agosti 24 na Septemba mosi mwaka huu, jamii hizo ziliingia tena kwenye mapigano katika kijiji hicho eneo la Naan zikigombea ardhi, ambapo kila upande unadai ni sehemu yake.
Mapigano hayo yalisababisha watu saba kujeruhiwa na mifugo zaidi ya 800 kupotea.

Hata hivyo, baada ya msako mkali wa polisi wa Tanzania kwa kushirikiana na maofisa wa Kenya kwa kutumia helikopta, mifugo zaidi ya 700 ilipatikana na silaha kadhaa zilikamatwa kutoka pande zote.

Lakini mkuu wa wilaya hiyo, amekuwa akiwaandama Wasonjo kuwa walisalimisha silaha mbili tu wakati wenzao Wamasai wamesalimisha zote, jambo linalopingwa na Wasonjo hao wakidai anakumbatia jamii hiyo ya Loita ambayo inatokea Kenya.

Kwa mujibu wa wazee hao, Loita ni wavamizi kutoka Kenya kwani jamii nyingine ya Wamasai asili ya Tanzania za Laitayok, Salei na Kisongo wanaishi nazo bila migogoro yoyote.

Madai hayo yaliungwa mkono na mkuu wa wilaya alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya siku Ijumaa iliyopita, akisema hali hiyo ilijidhihirisha wakati wa mapigano ya karibuni kwani baada ya mifugo ya Wamasai hao kutekwa na Wasonjo, maofisa wa Kenya waliingilia kati kusaidia kuitafuta.

Alisema kuwa Wamasai wa Tanzania wamekuwa wakiwaalika wenzao kutoka Kenya na kuishi nao pamoja na kuwapatia malisho, na kwamba serikali kupitia Idara ya Uhamiaji inaendelea kuwachunguza.

Katika kushughulikia mgogoro huo, Julai mwaka 2005, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mohamed Babu, aliandika barua ya kuzuia matumizi ya ardhi husika baada ya juhudi za usuluhishi kushindikana.

Katika zuio hilo, pia Mkuu wa Wilaya wa wakati huo, Kapteni mstaafu Msengi na Katibu Tawala waliandika barua kusisitiza eneo hilo lisitumike kwa matumizi yoyote kama kulima, kutundika mizinga, kulisha mifugo na kukata majani hadi hapo ufumbuzi utakapopatikana.

Lakini katika hatua ya kushangaza Wamasai wameachwa wakiendelea kulikalia eneo husika na kufanya shughuli zao wakati wenzao wa jamii ya Wasonjo kila wanapojaribu kufanya shughuli zao katika eneo hilo, serikali ya wilaya inawakamata na kuwafungulia mashitaka kwa uvamizi.

Alipoulizwa juu ya uwepo za zuio hilo, mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, alikiri lakini akasema ofisi yake haina barua hizo hadi sasa. Na kuhusu hatua ya FFU kuingia kijijini hapo usiku juzi na kufanya uharibifu na uporaji, alidai hizo habari anazisikia kwa mwandishi.

“Hizo habari nazisikia kwako, mimi bado nasubiri majibu kutoka kwa wazee,” alijibu Wawa Lali kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu yake ya kiganjani.

No comments:

Post a Comment