WAMTAKA ACHUKUE HATUA DHIDI YA MAUAJI YA RAIA KINYUME CHAKE SERIKALI
INAHUSIKA
Rais Jakaya Mrisho Kikwete |
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemwandikia barua Rais
Jakaya Kikwete kikimtaka achukue hatua dhidi ya matukio kadhaa ya mauaji ya
raia yaliyotokea kwa nyakati tofauti katika mikutano yake ya hadhara kwenye
Mikoa ya Singida, Tabora, Arusha, Morogoro, Iringa.
Hatua kilichopendeza ni pamoja na kuwawajibisha viongozi wenye dhamana;
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Polisi, IGP Said
Mwema; Mkuu wa Operesheni Maalumu Polisi, Paul Chagonja, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Morogoro, Faustine Shilogile na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael
Kamuhanda.
Barua hiyo ya Septemba 10, mwaka huu iliyoandikwa na Mwenyekiti wake,
Freeman Mbowe baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, imemtaka Rais
Kikwete kuwafukuza kazi watendaji hao katika Serikali yake kwa kuwa wameshindwa
kazi.
Kimesema kwamba mauaji mengi miongoni mwa hayo, yametokea bila hatua
stahiki za kisheria kuchukuliwa na kusema kwamba ukimya huo unaweza kutoa picha
potofu kwa umma kwamba Serikali yake inaunga mkono au imewatuma polisi au watu
wengine waliosababisha mauaji hayo.
Matukio ya vifo ambayo chama hicho kimetaka yachunguzwe ni pamoja na lile la Januari Mosi, mwaka jana mkoani Arusha, Igunga (Novemba, mwaka jana) na Arumeru Mashariki (Aprili, mwaka huu).
Mengine ni lile la Iramba lililotokea Julai 14, mwaka huu, Morogoro
(Agosti 27, mwaka huu) na Iringa Septemba 2, mwaka huu ambalo hata hivyo,
shauri lake limeshafikishwa mahakamani. Kimedai kwamba katika Uchaguzi mdogo wa
Arumeru Mashariki, Kiongozi wa Kata wa chama hicho, Msafiri Mbwambo alichinjwa
huku chanzo cha kifo hicho kikielezwa kuwa ni masuala ya kisiasa.
Pia kilielezea mauaji yaliyotokea katika Kijiji cha Ndago, Wilaya ya
Iramba, Singida na kudai kwamba kikundi cha watu kilivamia mkutano wa Chadema
kwa mawe na kwamba licha ya polisi kuwapo eneo hilo, hawakuchukua hatua zozote.
Chama hicho pia kimekumbusha mauaji ya mfuasi wake mkoani Morogoro, Ally Zona
kikisema kifo hicho pia kina utata kwani taarifa ya polisi imesema alikufa kwa
kugongwa na kitu kizito wakati chama hicho kikidhani kwamba alipigwa risasi.
Kimesema pamoja na matukio yote hayo, viongozi wote hao hawakuchukuliwa
hatua zozote za kuwajibika kwa matukio hayo. Pia Chadema kimeonya kuwa hali
hiyo ikiachwa inaweza kujenga dhana potofu kwa wananchi kuwa Jeshi la Polisi
liko mikononi mwa CCM na kazi yake ni kulinda masilahi ya chama hicho kwa
gharama yoyote ile jambo ambalo Mbowe alisema ikiwa Rais Kikwete atachukua
hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi hao, atakuwa ameudhihirishia umma kwamba
Serikali yake haifumbii macho mauaji yanayofanywa na vyombo vya usalama nchini.
Kimemtaka Rais Kikwete kuunda tume ya kijaji au kimahakama kuchunguza vifo
vilivyotokea katika mikusanyiko, mikutano, maandamano au mazingira ya kisiasa
yanayokihusisha Chadema.
Ikulu yajibu Katibu Mkuu Kiongozi:
Balozi Ombeni Sefue alipoulizwa juu ya barua hiyo alisema haijafika
ofisini kwake, huku akisisitiza kuwa kama imeandikwa kwa Rais si lazima ifike
kwake. “Sijaiona, ila kama wamemwandikia Rais barua sidhani kama itakuja kwangu.
Itakwenda kwake moja kwa moja,” alisema Balozi Sefue. Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye hakutaka kuzungumzia hatua hiyo ya Chadema akisema,
“Siwezi kusema chochote kwa kuwa barua yenyewe sijaiona pia ni barua ya Rais.”
Kauli ya Bavicha Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), limemtaka Rais Kikwete
kuunda tume huru yenye wataalamu wa sheria ili kuchunguza mauaji, utekaji,
vurugu na unyanyasaji wa wananchi unaotokea kwenye mikutano ya siasa hasa
inayokihusisha chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Morogoro baada ya kikao
cha baraza hilo taifa, Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alisema kwamba kama
Rais Kikwete atashindwa kufanya hivyo, baraza lake kwa kutambua kuwa matukio
mengi ya mauaji yamehusisha vijana, litahamasisha maandamano nchi nzima na
kuishtaki Serikali yake.
No comments:
Post a Comment