MBUNGE
wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kuueleza umma kuwa mwendelezaji mwenza
aliyepatikana kwa ajili ya mji wa kisasa wa Luguruni anatoka kampuni gani.
Mbali
na kueleza jina la kampuni hiyo, Mnyika pia amemtaka waziri huyo kueleza kazi
hiyo itaanza lini na nafasi ya serikali na wananchi ni ipi katika mradi huo na
kisha aweke hadharani mkataba ulioingiwa baina ya mwendelezaji mwenza huyo
kutoka sekta binafsi na serikali, ili wananchi watambue mipaka yao.
Mnyika
alitoa kauli hiyo juzi katika eneo la Kibamba mji mpya alipokuwa akihutubia
mkutano wa hadhara, baada ya kufanya kazi ya kichama ya kufungua matawi saba ya
CHADEMA katika kata ya Kwembe.
Alisema
serikali ilichagua eneo la Luguruni kuwa moja ya sehemu zitakazojengwa miji ya
kisasa kwa lengo la kupunguza msongamano mjini na ikaingia gharama za kupima
viwanja kulipa fidia kwa wananchi wa maeneo hayo na kueleza kuwa kitendo cha
kuacha kuwa pori ni kuhatarisha usalama wa wananchi wa maeneo hayo.
“Mwaka
huu serikali iliahidi bungeni juu ya kupatikana mwendelezaji mwenza sasa
watufahamishe basi ni nani kwa kuwa leo wananchi wanalalamikia eneo hili kuwa
sehemu ya maangamizi yao, wanakabwa wanaibiwa na hata kubakwa kama walivyosema
lakini pia kuendelea kuacha eneo hili kuwa pori ni kuwaruhusu watu wavamie
kisha serikali iingie gharama nyingine ya kuwaondoa,” alisema Mnyika.
No comments:
Post a Comment