SIKU moja tangu Msajili wa Vyama vya
Siasa, John Tendwa, ajitokeze na kulaani mauaji ya raia yaliyofanywa na polisi
kwenye mikutano ya kisiasa na kutishia kuvifutia usajili vyama vinavyojihusisha
na vurugu, wanasiasa wamemshukia vikali.
Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba, akidai Tendwa ni bomu na mvurugaji wa vyama vya
siasa, CHADEMA wamemtaka msajili huyo aanze kwa kukifuta CCM ambacho kimekuwa
na matukio ya kufanya fujo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana,
Profesa Lipumba, alisema ameshangazwa na kauli ya Tendwa ambayo inaonyesha wazi
kashindwa kusimamia haki ya vyama vya siasa na matokeo yake ameamua kuvuruga
mambo.
Alisema kuwa Tendwa hapaswi kutoa
vitisho kwa vile vyama vimekuwepo kwa utaratibu wa sheria, na hivyo kazi yake
si kushauri polisi kama ambayo ameonyesha katika kauli yake.
“Najua Tendwa anataka kutuonyesha kuwa
labda yeye ni kada wa chama fulani cha siasa, lakini sitaki kuamini hilo bali
anachotakiwa kufanya ni kuacha kujichanganya na kauli anazozitoa,” alisema.
Prof. Lipumba alisema kuwa hatua ya
kutoa vitisho hivyo sio tu inazidisha chuki kwa wananchi, bali pia inaongeza
vurugu zisizokuwa na msingi.
Alisema kuwa wamekuwa wakitoa taarifa
za kuilalamikia CCM kuhusiana na fujo hizo, lakini Tendwa amekaa kimya na
badala yake anawazushia wao kuwa ndiyo wanafanya vurugu.
Naye Mchungaji wa Pentekoste, William
Mwamalanga kutoka mkoani Dodoma, alisema kuwa Tendwa anatakiwa kuwa na hekima
na busara wakati huu ambao taifa lipo katika majonzi ya kumpoteza mwanahabari.
“CHADEMA ina watu wengi na pia ni kati
ya vyama vinavyolalamikia kuhujumiwa na Jeshi la Polisi, hivyo kauli kama hiyo
anayoitoa inaweza kuzidisha uhasama miongoni mwa jamii,” alisema.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Life Way
Ministries, lenye makao yake makuu mjini Dodoma, Elia Mauza, naye alisema kuwa
kauli ya Tendwa ni ya kukurupuka na haina ufumbuzi wa kutatua tatizo la mauaji
yanayosababishwa na polisi.
Alisema kamwe Jeshi la Polisi halina
nafasi ya kujikwamua katika tukio hilo la mauaji ya mwandishi kwani alikuwa
kazini.
“Hapa Tendwa asitafute njia ya
kulisafisha Jeshi la Polisi na kuonyesha kuwa waliosababisha kifo ni wanasiasa,
polisi hawana nafasi ya kutoka juu ya jambo hili,” alisema.
Naye Kamishna wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa
Dodoma, Kayubo Kaptari, alisema kuwa kwa sasa siasa za nchi zinaelekea kubaya
na kinachosababisha ni Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuingiwa na hofu ya
kuondoka madarakani.
“Tendwa anatakiwa kueleza ni chama gani
cha siasa cha upinzani ambacho kinamiliki silaha kama si Jeshi la Polisi ambalo
lipo chini ya Serikali ya CCM,” alisema.
TCD wamtaka Pinda
Katika hatua nyingine, Kituo cha
Demokrasia nchini (TCD), kimeomba kukutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa
dhumuni la kuzungumzia hali halisi ya mauaji ya utata yanayoendelea kutokea
nchini na kufanywa na vyombo vya usalama.
Akizungumza na wandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kituo hicho, James Mbatia, alisema
kuwa vyama vyote sita vyenye wabunge pamoja na kimoja kinachowakilisha vyama
visivyo na wabunge vimekubaliana kukutana na Pinda haraka iwezekanavyo.
“Kukutana na waziri mkuu ni muhimu kwa
vyama vyote vya siasa tukimuhusisha IGP na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa sababu
viko chini yake, hivyo ni vema kukutana naye kujadili hali hii tete
inayolikabili taifa,” alisema Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa
NCCR-Mageuzi.
Aliongeza kuwa hali hiyo ya mauaji
inapaswa kudhibitiwa haraka ili isiendelee nchini kwa sababu inaweza kuota
mizizi na kusababisha maafa kwa wananchi.
“Tunataka kukutana na waziri mkuu
haraka, wakati wowote uwe usiku au mchana ili kujadili jambo hili la dharura,
juzi tulifika ofisini kwake tukaambiwa yupo katika mkutano na mmoja wa viongozi
kutoka nchini China,” alisema.
Aidha, kituo hicho kimelaani mauaji
hayo na kuyafananisha na ukiukaji wa katiba kwa sababu yanafanyika kinyume na
katiba ya nchi ibara ya 14, inayosema kila raia wa nchi hii ana haki ya kuishi.
“Tunasikitika kutokana na vifo hivyo
ambavyo vimetokea Arusha, Singida, Songea, Morogoro hivi vya karibuni na juzi
Iringa,” alisema Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa.
Vyama hivyo vyenye wabunge bungeni ni
CCM, CHADEMA, CUF, UDP, NCCR- Mageuzi na TLP.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment