To Chat with me click here

Monday, September 10, 2012

CHADEMA WAMWAMBIA TENDWA OLE WAKO


KUMBURUZA NAPE KORTINI

Mwenyekiti wa taifa na Mbunge wa Hai, Mhe. Freeman Mbowe, katika kikao cha kamati kuu ya CHADEMA, kilichokutana jana kwa dhalura kujadili hali ya mauaji na mwenendo mzima wa kisiasa nchini, alibainisha kuwa wanazo taarifa sahihi zinazoonesha kuwepo kwa mbinu chafu zenye lengo la kukihujumu CHADEMA zinazopangwa na viongozi wa serikali.

Alisema kauli ya Tendwa ya kudai atafuta chama hicho, ni ushahidi tosha wa kuwepo kwa mbinu hizo na kuonya kuwa asijaribu hata sekunde moja kutekeleza mpango huo.

“Kauli za Tendwa zinatishia amani ya nchi na asitishie kukifuta CHADEMA.

“Tendwa acheze na chama chochote kingine, lakini si CHADEMA,” alisema Mbowe.

Walimtaka Tendwa kutambua wajibu wake na kutenda haki ili asiingize nchi katika machafuko.

“Tunataka kutengeneza ushindani wa haki bila kujali tunaingizwa katika matatizo kiasi gani. M4C itaedelea nchi nzima,” alisema.

Wanahabari watiwa moyo
Mbowe aliwataka wanahabari kutokata tamaa kutokana na mauaji hayo, bali tukio hilo liwape ujasiri zaidi katika utendaji wao wa kazi.

“Tukio lile lisiwe mwanzo wa kufifisha juhudi zenu, ila likawaimarishe wanahabari mkijua kwamba mna dhamana kubwa kwa taifa. Na ni sahihi kwamba maisha yetu yapo hatarini hasa pale serikali yetu inapokuwa haichukui hatua za makusudi na za haraka,” alisema.

Pamoja na hilo, aliwapongeza wanahabari waliokuwapo mkoani Iringa wakati wa tukio hilo la mauaji na kuonyesha ushujaa kwa kuendelea kuchukua picha.

“Kwa ujasiri waliouonesha wameiokoa Chadena katika mpango wa kutaka kuchafuliwa…picha hizi ndio zimekuwa salama si kwa CHADEMA tu bali kwa taifa na wanahabari kwa ujumla.

“Tunawashukuru wanahabari pamoja na kumpoteza mwenzao waliendelea kutimiza wajibu wao, wanastahili kupatiwa tuzo nasi kama chama tutawatambua kwa kazi kubwa,” alisema.

Aidha, alisema serikali inasahau kuwa mambo yanayojenga chuki na wananchi kwa serikali yao ni ugumu wa maisha, badala yake wanatumia dola kupambana na wananchi.

Alisema CHADEMA kitaendelea kuwaunganisha Watanzania, kwani bila kuing’oa CCM mwaka 2015 nchi itaingia kwenye machafuko makubwa.

Kutoa tamko leo
Mbowe alisema baada ya kikao hicho kujalidili suala hilo kwa undani, chama hicho leo kinatarajia kutoa tamko lake.

Alisema katika kikao hicho watajadili kauli za awali za polisi kuhusu tukio hilo, kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Tendwa, Waziri wa Mambo wa Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi na mustakali wa uhuru wa vyombo vya habari.

Pia alisema watajadili utendaji kazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambalo alieleza sasa linatumika kama kipeperushi cha serikali.

“CHADEMA hatutegemei TBC kutengeneza habari, kwani baada ya kuondoka Tido Mhando sasa imekuwa kipeperushi cha serikali. tutajadili mahusiano yetu na TBC na kutoa tamko zito kuhusu hatma yetu na TBC.

“Hakuna ugomvi na waandishi na wapigapicha wa TBC, kwani tunajua wao wanatumwa, bali uongozi. Tukio hili limetokea wao wanapindisha ukweli, wangekuwa na nia nzuri na busara wasingechukua habari za upande mmoja,” alisema.

Kumburuza Nape kortini
Mbowe alisema watamburuza mahakamani Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kutokana na kauli yake kuwa CHADEMA kinapewa mabilioni ya fedha na wafadhili nje ya nchi.

Alisema watampeleka Nape mahakamani ili aende kuithibitisha kauli hiyo na ukweli uweze kubainika.

“Ukifumbia macho hoja hii inaweza kuonekana kuwa ni ya kweli, sasa atakwenda kuithibitisha mahakamani, mahakama ikitenda haki ukweli utajulikana. Wanasheria wetu wanalifanyia kazi suala hili,” alisema.

Kwa muda sasa Nape amekaririwa akisema kuwa chama hicho kimekuwa kikipewa mabilioni ya fedha na wafadhili nje ya nchi na kuwahadaa Watanzania kupitia harambee mbalimbali.

CHADEMA kilimpa siku saba Nape kuthibitisha madai hayo, lakini hakufanya hivyo na kusema kuwa ana ushahidi kuhusu kauli yake dhidi ya chama hicho.

No comments:

Post a Comment