To Chat with me click here

Friday, September 14, 2012

KWA NINI TUNABORONGA KILA ZOEZI MUHIMU LA KITAIFA?

KUNA swali huwa najiuliza kila siku kwa nini, jinsi miaka inavyokwenda nchi inashindwa kusimamia na kuendesha bila mushkel zoezi au shughuli yoyote kubwa na muhimu ya kitaifa?

Ni kwa sababu ya kukosekana kwa wataalamu, fedha au ni uzembe tu wa watendaji? Au pengine ni ufisadi uliojikita katika utawala na jamii ya watanzania? Pengine ni kuzidiwa (overwhelmed) na idadi ya watu?

Tukiacha kwanza uzorotaji katika utoaji wa huduma za kijamii ambayo ni mazoezi endelevu – kama vile elimu, afya nakadhalika, kuna haya ya muda mfupi mfupi: kuandikisha wapiga kura, upigaji kura wenyewe, zoezi la kuratibu maoni ya katiba mpya, zoezi la sensa ya watu na makazi, na lile la uanzishwaji wa vitambulisho vya taifa.

Sote tunafahamu upungufu mkubwa ambao hujitokeza mara kwa mara katika zoezi la kujiandikisha kupiga kura na la kupiga kura lenyewe. Sidhani iwapo viongozi wetu wamejifunza na yaliyotokea nyuma, hata pale maafa makubwa yalipotokea hususan huko Visiwani Zanzibar mapema mwaka 2001.

Lakini pia kuna hili: Uamuzi wa kuyaendesha mazoezi matatu niliyotaja – zoezi la kuratibu maoni ya katiba mpya, zoezi la sensa ya watu na makazi, na lile la uanzishwaji wa vitambulisho vya taifa. Kwa wakati mmoja (simultaneously) au kwa kuingiliana kunazua maswali mengi kuhusu busara iliyotumika. Na bila shaka kutokana na sababu hii, na nyinginezo, mazoezi yote haya yamekumbwa na matatizo mengi tu (sipendelei hapa kutumia neno ‘changamoto’) katika kuyafanikisha.

Kwa mfano ilikuwa ni lazima kwa zoezi la vitambulisho vya kitaifa kwenda sambamba na lile la sensa na makazi? Na kwa nini, iwapo yangefanyika matayarisho mazuri, mazoezi haya ambayo yanaingiliana sana kimtazamo na kimalengo, yasifanyike kwa pamoja, kufuatana na ile methali isemayo ‘kuua ndege wawili kwa jiwe moja?’

Nina maana hapa kwamba nyenzo zile zile, kwa maana ya watendaji, fedha na vitendea kazi, zingeweza kutumika kufanikisha mazoezi yote mawili yaani kuandikisha sensa ya watu na makazi na hapo hapo kutoa vitambulisho vya kitaifa.

Nakiri kuna matatizo mengi katika kutimiza hilo, lakini kama nilivyosema, kwa matayarisho mazuri, nia thabiti, hili lingewezekana. Lingeokoa fedha na muda.

Lile zoezi la vitambulisho lingeachwa kuendelea kwani ni la kudumu hasa ikizingatiwa kuwa kila siku kuna malaki ya Watanzania wanatimiza umri wa miaka 18 na hivyo kuwa na sifa za kupata vitambulisho.

Ilishangaza kuona kuwa serikali, kupitia mamlaka yake ya vitambulisho- NIDA, iliweka muda maalum wa kuandikisha watu kupata vitambulisho katika mikoa wakati zoezi lenyewe ni la kudumu.

Kuna baadhi wanatoa hoja kwamba kwa kuwa fedha nyingi sana zinatumika katika mazoezi haya ya kitaifa, basi ni vyema yakafanyika kila moja peke yake kwa sababu za utafunaji wa fedha na wajanja wachache, yaani ufisadi.

Tukirudi kuhusu zoezi la sensa kwa mfano, inashangaza kwamba sensa ya kwanza kabisa nchini baada ya uhuru – miaka 45 iliyopita ilifanyika kwa mafanikio makubwa wakati ambapo utaalamu na wataalamu tulikuwa bado hatuna wa kutosha. Ufisadi pia ulikuwa haukuwapo. Sensa hiyo ilifanyika mwaka 1967, nyingine zikiwa za 1978, 1988, 2002 na hii ya sasa ya 2012.

Ufanisi wa sensa ya 1967 bila shaka ulitokana na namna ilivyofanyika, kwani makarani wa sensa (enumerators) katika nchi nzima walikuwa ni wanafunzi wa vidato vyo kwanza, pili, tatu na tano nami nikiwa mmoja wao nilipokuwa nasoma Tabora School. Baada ya sensa hiyo ya mwaka 1967 sensa zilizofuatiwa ziliendeshwa na walimu wa shule za sekondari na za msingi kama makarani.

Katika kundi letu tulipangiwa kuhesabu watu katika wilaya ya Nzega na tukasambazwa sehemu mbali mbali za wilaya hiyo. Mimi na wenzangu wengine tukapelekwa tarafa ya Itumba, kama kilometa 150 mashariki mwa Nzega, kijiji ambacho sasa kiko katika wilaya ya Igunga.

Posho yetu ilikuwa ni shilingi 8 kwa siku na tulipelekwa kule wiki mbili kabla ya siku ya sensa kwa ajili ya maandalisi yakiwemo kutambua vijiji na nyumba za wakazi wa kuhesabiwa.

Katika kufanikisha zoezi hili kila mmoja wetu alikodishiwa baskeli kutoka kwa wakazi wa kijijini hapo kwa shilingi mbili kila siku. Hapo ndipo nilipojifunzia kupanda baskeli.

Wenyeji waliotusaidia ni pamoja na Makatibu Tarafa na wajumbe wa nyumba kumi kumi (wa chama pekee cha TANU wakati huo). Mawasiliano na makao makuu ya wilaya mjini Nzega ulikuwa duni sana kwani kulikuwa hakuna simu za mikononi wala za mezani katika eneo hilo lakini gari ya aina ya Land Rover- 109, ilikuwa inakuja kila baada ya siku tatu hivi ikileta wasimamizi kuratibu maendeleo ya zoezi na kutuletea vifaa na posho.

Itakuwa si sahihi iwapo serikali itatoa tathmini chanya ya sensa ya mwaka huu, kwamba imekwenda kwa mafanikio makubwa, na nathubutu kusema kwamba kwa kiasi kikubwa, matatizo yaliyolikumba zoezi hilo, yalitokana na upungufu uliojitokeza.

Suala la Waisilamu kususia sensa baada ya tamko la uongozi wa Baraza Kuu la Waisilamu (BAKWATA) ulitokana na taarifa iliyotolewa na chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali (TBC1), taarifa ambayo iliwakera Waisilamu wengi na serikali kushindwa kwa haraka kuthibitisha au kukanusha ukweli wake.

Lakini hata hivyo serikali iliomba radhi kuhusu taarifa ile ingawa athari (damage) tayari ilikuwa imefanyika miongoni mwa jamii ya Kiisilamu na hivyo hata pale baada ya muda mfupi BAKWATA ilipobatilisha uamuzi wake, uliacha waumini wa dini hiyo kugawanyika, wengine wakishikilia uamuzi wao wa awali wa kususia.

Mambo yalionekana kuharibika zaidi pale baadhi ya waumini wa Kiisilamu walipokamatwa na polisi kwa makosa ya ama kukataa kuhesabiwa au kushawishi wengine kutohesabiwa.

Haya zaidi yalitokea mikoani ingawa wengi walishangaa kuona kulikuwapo kiongozi mmoja wa kitaifa aliyekuwa akiripotiwa na vyombo kadha vya habari akihamasisha waziwazi waumini wa dini ya Kiisilamu kukataa kuhesabiwa ingawa hakukamatwa.

Kwa ujumla mamlaka za serikali zilizokuwa zinasimamia zoezi la sensa zilionekana kuvurunda kuhusu suala hili kwa kutokuwa makini katika uamuzi.

Lakini kibaya zaidi ni pale serikali ilipoonekana ‘kusalimu amri’ baada ya maandamano makubwa ya waumini wa dini Kiisilamu jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita. Serikali, kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ilikubali kuwaachilia waumini wote wa Kiisilamu waliokuwa wanashikiliwa na polisi kutokana na kukataa kuhesabiwa au kushawishi wengine kutohesabiwa.

Wadadisi wa mambo wanaona kuwa huenda hii imeiweka serikali pabaya (bad precedent) kwani itakuwa vigumu kwa serikali kuwakatalia waumini wa dini nyingine kwa madai yao iwapo nao watatumia njia hiyo ya maandamano, au hata kwa waisilamu hao hao katika madai yao mengine dhidi ya seriklai.

Na tayari kuna dai moja ambalo wamelizungumzia – la kutaka kumng’oa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani NECTA. Je, serikali itakuwa na ubavu wa kukataa?

No comments:

Post a Comment