To Chat with me click here

Wednesday, September 26, 2012

KAMATI YA MAADILI YAWATOSA WAGOMBEA CCM

JK ASEMA BAADHI YA MAPENDEKEZO YA VIKAO WILAYANI, MIKOANI YAMEKATALIWA. NI BAADA YA KUJADILI KWA NINI HAWA WALIPITISHWA NA WALE WALIACHWA
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amesema Kamati ya Maadili imefumua baadhi ya mapendekezo ya wagombea yaliyotolewa katika vikao mbalimbali vilivyotangulia.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM Mjini Dodoma kilichoanza jana.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mchujo wa majina hayo ulikuwa mzito na kwamba, Kamati ya Maadili iliyokuwa imalize kazi Ijumaa wiki iliyopita, ililazimika kumaliza kazi yake juzi Jumapili, saa 9.30 usiku. Alisema kwamba, ugumu wa kazi hiyo ulitokana na wingi wa wagombea tofauti na ilivyotarajiwa.

Alisema kamati hiyo ilipitia jina moja baada ya jingine, ili kuangalia wagombea waliopendekezwa wana sifa zipi na kwa nini walipendekezwa na wagombea walioachwa waliachwa kwa sababu gani.

“Idadi ya wagombea waliojitokeza kugombea ni kubwa, kazi ilikuwa kubwa, majina ya waliojitokeza kugombea ndani ya chama ni 2,853 na waliojitokeza kugombea ndani ya jumuiya za chama ni 2,104, hivyo kamati ilipitia majina karibia 5,000.

“Tumepitia jina moja baada ya jingine kuona yule aliyependekezwa kapendekezwa kwa sababu gani na yule aliyeachwa ameachwa kwa sababu zipi.

“Maeneo mengine tumekuja na mapendekezo tofauti kabisa na yale mapendekezo ya awali kutoka mikoani na vikao vilivyotangulia.

“Wagombea ni wengi, hali hii inafurahisha kwani wengi wao ni wasomi jambo ambalo ni la kujivunia na wanaosema CCM inakufa watakufa wao wataiacha CCM.

“Jana tulimaliza kikao cha Kamati ya Maadili saa 9.30 usiku, hivyo leo tukimaliza saa 6 usiku itakuwa siyo mbaya kwa kuwa itaturahisishia katika Kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kitakachofuata baada ya kikao hiki,” alisema Rais Kikwete.

Kikao hicho cha Kamati Kuu, kilianza majira ya saa sita mchana na kilitarajiwa kuwa cha siku mbili, ili kuruhusu kikao cha Halmashauri Kuu kuanza.

Ratiba ya kikao cha Halmashauri Kuu ndicho kitafanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama ambacho kinatarajiwa kukaa kwa siku mbili.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama alisema jumla ya wajumbe 34 walihudhuria siku hiyo ya kikao kati ya wajumbe 39.

Wakati hayo yakiendelea Mjini Dodoma, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah, amesema taasisi yake imeanza uchunguzi wa vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaoendelea mkoani Dodoma.

Dk. Hoseah aliyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika mkutano wa wadau wa kupambana na rushwa nchini.

Alisema kwamba, rushwa katika chaguzi ni tatizo kubwa na linahusisha vyama vyote vya siasa ukiwamo uchaguzi wa nafasi mbalimbali ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Pamoja na hayo, alisema taasisi yake iko kazini na kwamba atakayejihusisha na vitendo vya rushwa atachukuliwa hatua za kisheria.

“Rushwa katika chaguzi ni tatizo kubwa na hii inatokana na kwamba kila anayegombea anatumia fedha, suala hili ni kwa vyama vyote vya siasa vinavyogombea,” alisema Dk. Hoseah.

1 comment: