Uchaguzi
wa mameya wa wilaya mbili za Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza, unatarajiwa
kufanyika leo huku mnyukano mkali ukiwa katika halmashauri ya Nyamagana kutokana
na CCM na CHADEMA kuwa na idadi sawa ya viti vya madiwani na hivyo kutegemea
kura za CUF ziamue mshindi.
Katika
Halmashauri ya Ilemela, CHADEMA ina uhakika wa asilimia mia moja kutokana na
kuwa na madiwani wengi kuzidi wenzao wa CCM huku mikakati yao ikilenga
kuwashirikisha CUF ili waitwae pia Nyamagana.
Uchaguzi
huo unafanyika baada ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kugawanywa na hivyo kuzaa
halmashauri hizo mbili. Lakini pia Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa sasa muda
kadhaa haikuwa na Meya baada ya Baraza la Madiwani kumvua wadhifa huo, Jackson
Manyerere (CHADEMA).
Baada
ya meya kuenguliwa, kulizuka mtafaruku ndani ya CHADEMA jijini hapa ambao
ulisababisha madiwani wawili kutimuliwa uanachama kwa kile kilichodaiwa ni
usaliti wa kuanzisha hoja ya kumtosa kiongozi huyo.
Hivyo
kutokana na CHADEMA kutokuwa na madiwani hao, inaingia kwenye uchaguzi wa leo
ikiwa na madiwani sita na mbunge Ezekiel Wenje katika wilaya ya Nyamagana
wakati wenzao CCM wana madiwani saba na CUF wawili.
Kwa
mnyukano huo ni dhahiri kuwa CHADEMA na CCM watakuwa wamefungana kwa kura na
hivyo kuhitaji huruma ya madiwani wa CUF ili upande mmoja uibuke kidedea.
Taarifa
za uhakika kutoka jijini hapa ni kwamba CHADEMA wamefanya mazungumzo ya
kushirikiana na CUF kwa kuwaachia nafasi ya Naibu Meya ambayo itagombewa na
diwani wao wa kata ya Mirongo, Daud Mukama.
Kwa
halmashauri ya Ilemela CHADEMA wana uhakika wa kuibuka kidedea kutokana na kuwa
na madiwani wanane na mbunge Highness Kiwia huku wenzao wa CCM wakiwa na
madiwani sita na CUF ina mbunge wa Viti Maalum, Mkiwa Kimwanga.
Kamati
za utendaji za CHADEMA katika wilaya hizo zimefanya vikao tofauti kwa
kushirikiana na kamati za madiwani na kukamilisha mchakato wa kupata wagombea
wao.
Kwa
mujibu wa ofisa habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, kamati ya utendaji ya wilaya
pamoja na madiwani wa Nyamagana walimteua aliyekuwa Naibu Meya kabla, Diwani wa
Kata ya Maina, Charles Chibara, kuwa mgombea wa umeya wa Halmashauri ya Jiji la
Mwanza.
Kwa
upande wa Ilemela, kikao cha kamati ya utendaji pamoja na madiwani walimteua
Diwani wa Kata ya Nyamanoro, Abubakar Kapera, kuwa mgombea wa umeya Halmashauri
ya Manispaa ya Ilemela.
Kikao
hicho cha Ilemela, pia kilimteua Diwani wa Kirumba, Danny Kahungu, kuwa mgombea
wa nafasi ya Naibu Meya halmashauri hiyo wakati kamati ya utendaji ya Nyamagana
imekubali kumwachia kugombea nafasi ya Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la
Mwanza, Diwani wa Mirongo, Daudi Mkama (CUF).
Wao
CCM wamemteua Diwani ya Kata ya Mkolani, Stanslaus Mabula, kugombea nafasi ya
umeya katika halmashauri ya jiji la Mwanza huku diwani wa kata ya Igogo, John
Minja, akigombea unaibu meya na Ilemela wagombea ni Renatus Kalunga na naibu
wake Sarah Ng’hwanu.
No comments:
Post a Comment