To Chat with me click here

Thursday, September 27, 2012

MBUNGE CCM AKAMATWA KWA TUHUMA ZA RUSHWA

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Zaynab Mattitu Vullu
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, imemtia mbaroni Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Vullu (CCM) kwa tuhuma za rushwa.

Vullu alikamatwa juzi pamoja na wenzake wawili ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT), Wilaya ya Kisarawe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Asia Madima pamoja na Katibu wa UWT wa wilaya hiyo, Mwajuma Mombwe.

Chanzo chetu cha habari kilichopo wilayani Kisarawe kilisema jana, kuwa Vullu na wenzake hao, walikamatwa juzi saa 12 jioni baada ya kudaiwa kugawa fedha kwa wajumbe waliohudhuria kikao cha Baraza la UWT, Wilaya ya Kisarawe kilichokuwa kikifanyika makao makuu ya CCM, Wilaya ya Kisarawe.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Vullu, Asia na Mwajuma, walikamatwa na Kamanda wa TAKUKURU, Wilaya ya Kisarawe, aliyetajwa kwa jina moja la Noel.

“Kabla hawajakamatwa, tuliingia katika kikao cha Baraza la UWT la Wilaya ambako tulichagua wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji.

“Tulipomaliza kuchaguana, akaja Mama Vullu (Zainab Vullu), akapewa nafasi ya kuzungumza, akatwambia kwamba, Oktoba 3 mwaka huu, baadhi yetu tukalale nyumbani kwake na wengine tukalale katika ofisi za chama chetu hapa Kisarawe kwa ajili ya kufika mapema kwenye uchaguzi wa jumuiya yetu utakaofanyika Oktoba 4 katika Ukumbi wa Filbert Bayi.

“Yeye Mama Vullu ndiye Mwenyekiti wa UWT, Mkoa wa Pwani na anatetea nafasi yake, kwa hiyo, alitwambia atakayeshindwa kufuata maelezo yake, ajue hatapata kitu.

“Alipomaliza kuzungumza hayo, yule Asia Madima, akaanza kutugawia Sh 10,000 kila mmoja kwa wajumbe wote 44 tuliokuwa katika ukumbi huo. Wakati fedha zikiendelea kugawiwa, yule Kamanda wa TAKUKURU wa Wilaya anaitwa Noel, akaingia ukumbini akiwa na mwenzake mmoja.

“Walipofika, wakamkamata Asia akiwa na burungutu la noti ambalo alikuwa akiendelea kuligawa kwa wajumbe, akakamatwa pia Mama Vullu na Mwajuma na kupelekwa katika ofisi za TAKUKURU pale chini.

“Kwa ujumla, viongozi wetu walipokamatwa, ilikuwa ni mshike mshike maana watu walijaa hapa ofisini kisha kule TAKUKURU kwa sababu walitaka kujua hatima ya viongozi hao,” kilisema chanzo chetu hicho.

Kamanda Noel alipopigiwa simu ili kuzungumzia tukio hilo, alipokea simu, lakini mwandishi wetu alipojitambulisha, alikata simu na alipopigiwa tena simu yake ilikuwa ikiita bila majibu.

Kamanda wa TAKUKURU, Mkoa wa Pwani, Joyce Shirima, alipozungumza kwa simu juu ya tukio hilo, hakukubali wala kukataa ila akasema anasubiri taarifa kamili kutoka wilayani Kisarawe. Pia aliahidi kumpigia simu mwandishi wetu baada ya muda lakini hakufanya hivyo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Fatuma Kimario, alipozungumza kwa simu, alipokea simu lakini mwandishi wetu alipojitambulisha, alisema yuko kwenye kikao hawezi kusema chochote. Hata hivyo, alipopigiwa tena, simu yake haikupatikana.

Wakati hayo yakiendelea, Vullu na Asia walizungumza na waandishi wa habari na kukiri kwamba walikamatwa na TAKUKURU ingawa hawakujua ni kwa nini walikamatwa.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa CCM, Wilaya ya Kisarawe, Mbunge Vullu alisema, “Ni kweli TAKUKURU walitukamata mimi na huyu mwenzagu Asia pamoja na Mwajuma.

“Mnajua katika vikao kuna posho zinazotolewa kihalali na ndiyo maana waliokuwa wakipokea hizo Sh 10,000 tulizokuwa tukiwapa, walikuwa wakisaini, jamani haikuwa rushwa hata kidogo, hizo siyo rushwa kwa sababu rushwa mtu hasaini.

“Pia mimi (Vullu) sikukamatwa na fedha zozote, aliyekuwa akigawa fedha ni huyu Asia, yeye ndiye anayejua alizitoa wapi, lakini bado nasema tulikuwa hatutoi rushwa na kwa kuzingatia hilo, hata tulipopelekwa pale ofisi za TAKUKURU tulikataa kujaza fomu alizotupatia yule Noel kwa sababu hatukuwa na kosa.

“Pamoja na hayo, naomba mkamuulize huyo Noel ni kwa nini alikuja kutukamata na ‘gate keeper’ (mlinzi wa getini) anaitwa Kingu, hivi huyo Kingu nia nani hapo, mkamuulize,” alisema Vullu.

Kwa upande wake, Asia alisema wakati anakamatwa alikuwa na burungutu la noti zenye thamani ya Sh 550,000 kwa kuwa baadhi ya wajumbe alikuwa ameshawasainisha kiasi fulani cha fedha.

“Kikao kilikuwa na wajumbe 49 na mhudumu mmoja, kwa hiyo hao TAKUKURU walipofika hapa, walitukamata na wakachukua fedha zangu ambazo baadaye nitazifuatilia ili wanirudishie maana hizo hazikuwa rushwa bali ni posho za kawaida ambazo nimezipata kwa njia halali.

Kwa mujibu wa Asia, maofisa hao wa TAKUKURU mbali na kuchukua fedha hizo, walichukua pia Katiba ya UWT, walichukua nyaraka za vikao, orodha ya wajumbe waliokuwa wakitakiwa kusaini posho na kitabu cha Kanuni.

Juzi, Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akifungua kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Mjini Dodoma, alikemea vitendo vya rushwa ndani ya chama hicho na kuwataka wana CCM wasijihusishe na rushwa kwa kuwa rushwa inakichafua chama.

No comments:

Post a Comment