Mhe. John Mnyika |
MBUNGE
wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemjia juu Rais Jakaya Kikwete akimtaka atoe
maelezo ya utekelezaji wa ahadi zake wakati wa kampeni za mwaka 2010 kuhusiana
na mambo mbalimbali, likiwemo suala la ajira milioni moja kwa Watanzania.
Mnyika
pia amemtaka Rais Kikwete awaambie wakazi wa Ubungo kuhusiana na viwanda kadhaa
vilivyo ndani ya jimbo lake, ambavyo vingekuwa chachu ya maendeleo ya wananchi,
lakini vimefungwa.
Mbunge
huyo alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kuzindua
ofisi, pamoja na kuweka mawe ya misingi katika kata ya Mabibo ambapo alieleza
kushangazwa kwake na kutotekelezwa kwa ahadi hewa zilizotolewa na kiongozi huyo
wakati wa uchaguzi mkuu uliyopita.
Mnyika
alivitaja baadhi ya viwanda hivyo vilivyobinafsishwa kuwa ni Ubungo Garments,
Spinning Mill, Polysack Lmt, Tanzania Sewing Thread, Coastal Diaries, pamoja na
kiwanda cha Zana za Kilimo (UFI).
“Tunamshinikiza
Kikwete kama kiongozi wa nchi pamoja na Baraza la Mawaziri kurejesha viwanda
vilivyobinafsishwa kiholela katika jimbo la Ubungo ili kuondokana na tatizo la
ukosefu wa ajira linalowakabili Watanzania,” alisema Mnyika.
Katika
hilo, alimtaka mwenyekiti wa baraza hilo ambaye ni Rais kutoa kauli ya matokeo
ya maafikiano ya pamoja waliyoafikiana na mawaziri juu ya ajira hizo ili
kuondoa utata uliopo baina ya wananchi na viongozi wao wa kada husika.
Alitanabaisha
kuwa ili kukabiliana na tatizo la ajira katika jimbo hilo, manispaa ya
Kinondoni imetenga fedha zaidi ya sh milioni 200 kwa ajili ya mikopo kwa
vikundi vya kinamama pamoja na vijana.
Alitumia
fursa hiyo kuitaka manispaa hiyo kutoa kipaumbile katika suala la ajira hasa
kwa kuwafikia walengwa badala ya kuishia mikononi mwa wachache.
“Nawataka
na ninyi wananchi mliojiunga katika vikundi mbalimbali vya kukopeshwa
kufuatilia kwa makini fedha hizo ngazi husika, ila mkikwama tafadhali rudini
kwangu kwa ripoti maalumu ili nifuatilie suala hilo ambalo ni muhimu kwetu,”
alisema mbunge huyo.
Rais
Kikwete ndiye mgombea aliyeongoza kwa kutoa ahadi nyingi wakati wa kampeni za
uchaguzi kuliko wagombea wengine wa nafasi ya urais kutoka vyama hasa vya
CHADEMA na CUF.
No comments:
Post a Comment