To Chat with me click here

Friday, September 28, 2012

VULLU (CCM) AKALIA KUTI KAVU

NI ANAYEDAIWA KUKAMATWA KWA RUSHWA KISARAWE, NAPE ASEMA ATACHUNGUZWA NA KAMATI YA MAADILI

Hon. Zaynab Vullu (CCM) Special Sit
MBUNGE wa Viti Maalum, Zainab Vullu (CCM), Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), Wilaya ya Kisarawe, Asia Madima na Katibu wa UWT wa wilaya hiyo, Mwajuma Mombwe, wako hatarini kung’olewa katika nafasi wanazogombea.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, jana alisema kwamba baada ya vyombo vya habari kuripoti jana, kwamba Vullu na wenzake hao walikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilaya ya Kisarawe, Kamati ya Maadili ya CCM itakwenda Kisarawe kuchunguza tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa Nape, kama kamati hiyo ikithibitisha kwamba Vullu, Asia na Mwajuma walikamatwa wakigawa rushwa, wataondolewa mara moja kwenye mchakato wa kugombea nafasi mbalimbali za chama hicho.

Vullu ndiye Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Pwani na anatetea nafasi yake.
“Mgombea yeyote atakayebainika kukiuka maadili kwa kutoa rushwa katika chaguzi mbalimbali zinazoendelea ndani ya chama, ataondolewa kwenye mchakato wa uchaguzi.

“Nasema hivyo kwa sababu majina ya wanachama yaliyopitishwa katika vikao vya chama hayamaanishi kwamba wagombea wamehakikishiwa ushindi wa kufanya watakavyo.

“Chama hakitasita kumwondoa mwanachama yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati huu wa mchakato ndani ya chama.

“Sasa nasema hivi, Kamati ya Maadili itakwenda huko Kisarawe kuchunguza tuhuma hizo na kama ikibainika wanachama hao wamejihusisha na vitendo vya rushwa, wataondolewa mara moja kwenye mchakato wa uchaguzi.

“Ni juzi tu Halmashauri Kuu imeonya wote wanaodhani kwamba kupitishwa kwa majina yao katika vikao vya Halmashauri Kuu ni tiketi ya kufanya watakavyo, wanajidanganya.

“Kupitishwa majina yao ni jambo moja na kushiriki mchakato wa uchaguzi ni suala jingine, hivyo wakibainika kukiuka maadili, nasema wataondolewa mara moja kwenye mchakato,” alisema Nape kwa kifupi.

Juzi TAKUKURU, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, iliwatia mbaroni Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Vullu (CCM), Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT), Wilaya ya Kisarawe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Asia Madima, pamoja na Katibu wa UWT wa wilaya hiyo, Mwajuma Mombwe, kwa tuhuma za rushwa.

Chanzo chetu cha habari kilichopo wilayani Kisarawe kilisema kuwa, Vullu na wenzake hao, walikamatwa Jumanne wiki hii, saa 12 jioni, baada ya kudaiwa kugawa fedha kwa wajumbe waliohudhuria kikao cha Baraza la UWT, Wilaya ya Kisarawe, kilichokuwa kikifanyika makao makuu ya CCM, Wilaya ya Kisarawe.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Vullu, Asia na Mwajuma, walikamatwa na Kamanda wa TAKUKURU, Wilaya ya Kisarawe, aliyetajwa kwa jina moja la Noel.

No comments:

Post a Comment