SIKU
chache baada ya Jeshi la Polisi kumuua kinyama mwandishi wa habari wa kituo cha
Channel Ten, Daudi Mwangosi, baadhi ya askari waaminifu wamefichua siri za
mauaji yanayofaywa na jeshi hilo.
Wakizungumza
na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, askari hao
walisema wakuu wao wanatumiwa kwa amri za watawala ili kuingilia kudhibiti
matukio ambayo wakati mwingine husababisha vurugu zinazopoteza uhai wa
wananchi.
Walisema
tatizo kubwa ni wakuu wa polisi wilaya (OCD), makamanda wa mikoa (RPC) na
maofisa upelelezi wa mikoa (RCO) ambao hulazimishwa kufanya kazi kwa amri ya
wakuu wa wilaya na mikoa.
“Hawa
wakuu wa wilaya na mikoa ni viongozi wa chama tawala, CCM. Hivyo, ili viongozi
wetu wa polisi waweze kupanda vyeo ni lazima wajipendekeze kwao; yaani hata
kipindi cha kampeni mkuu wa wilaya anampa amri OCD kudhibiti wapinzani,”
alisema mmoja wa askari hao.
Walifafanua
kuwa ili tatizo hilo liweze kuisha na jeshi hilo kufanya kazi kwa mujibu wa
sheria na uhuru, ni lazima vyeo hivyo vya wakuu wa wilaya na mikoa vifutwe
kwenye katiba mpya ijayo.
Katika
tukio linaloshabihiana na madai ya askari hao, Tanzania Daima limedokezwa kuwa
huko mkoani Pwani, hivi karibuni jeshi hilo limelazimishwa kupindisha sheria
kwa lengo la kumlinda kigogo mmoja wa CCM aliyekuwa ametiwa mbaroni.
Lakini
katika hali ya kushangaza, mtuhumiwa huyo alirejeshwa kituo kikuu cha polisi na
kuhifadhiwa hapo. Na alikuwa akitaka kuonana na mumewe, anakabidhiwa kwa askari
polisi wa kike ambaye alikuwa anampeleka zaidi ya kilometa 25 kwenda kuonana
naye.
Taarifa
toka ndani ya jeshi hilo mkoani humo zinasema kuwa, yote hayo yalifanyika kwa
amri ya kigogo mmoja wa CCM mkoa, na uongozi wa polisi ulifyata mkia hadi juzi
mtuhumiwa huyo alipoachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Ni
katika mfano wa tukio kama hilo, askari hao waliozungumza na gazeti hili
walisema kuwa matukio ya raia kupigwa na wakati mwingine kujeruhiwa na polisi
hadi kufa, hayawezi kukoma ikiwa sheria hazifuatwi; na badala yake
zinazingatiwa amri za viongozi wa kisiasa.
Mwangosi
aliwashtukia askari
Naye
Mkuu wa Operesheni ya M4C ya CHADEMA, Benson Kigaila, jana alifichua siri mjini
Iringa, akisema kuwa Mwangosi aliwatilia shaka mapema polisi waliokuwa kwenye
tukio hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Kigaila alisema kuwa muda mfupi kabla ya kuuawa kwake,
Mwangosi alimweleza kuwa askari wengi anaowafahamu si wale waliokuwa eneo la
tukio kudhibiti mkusanyiko wa CHADEMA.
“Marehemu
aliniambia kuwa hapa nina shaka na hawa polisi kwa kuwa wengi ninawafahamu
lakini ninaowaona si wale ninaowafahamu.Wanaofanya kazi za jeshi ni
mamluki wasio na mafunzo,” alisema Kigaila.
Wakati
siri hiyo ikifichuliwa, taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo mkoani Iringa
zinadai baadhi ya askari wanaodaiwa kumuua Mwangosi wamekamatwa kwa siri na
kuwekwa chini ya ulinzi.
Chanzo
chetu kinasema kuwa jeshi hilo mkoani Iringa tangu juzi linahaha kuchukua hatua
za dharura za kuwafundisha askari wake matumizi sahihi ya silaha wakati wa
kutuliza ghasia.
Tanzania
Daima imedokezwa kuwa tayari askari watano kati ya saba walioonekana kwenye
picha mbalimbali za magazeti na mitandao wakimpiga Mwangosi, wametiwa mbaroni.
“Hili
suala limetuweka katika wakati mbaya sana na hivi ninavyoongea na wewe tayari
askari watano kati ya saba wanashikiliwa katika kituo cha polisi Mufindi,
lakini habari hizi zinafanywa siri sana,” kilisema chanzo chetu.
Miongoni
mwa askari watatu ambao hawajakamatwa kwa mujibu wa chanzo hicho, ni pamoja na
yule anayeonekana katika picha mbalimbali akiwazuia wenzake waliomzunguka
Mwangosi kwa kunyoosha mkono juu na na baadae akiwa amejeruhiwa.
Mbali
na askari huyo anayetambulika kwa jina moja la Mwampamba, pia yule anayeonekana
pichani akiwa ameshikilia silaha aina ya bastola anayetajwa kwa jina la
Gabriel, naye hajakamatwa.
Habari
zaidi zinaeleza kuwa askari wengi waliokuwa katika operesheni hiyo siku ya
tukioa eneo la Nyololo, hawakuwa na mafunzo sahihi ya kutumia mabomu ya
machozi.
“Kiutaalamu
mabomu ya machozi yanatakiwa yalengwe juu na kuwe na umbali wa mita 60 mpaka
120, lakini ikitumika kinyume chake yanaweza kudhuru au kuua.
“Katika
kutuliza ghasia kuna mabomu ya aina mbalimbali ambayo yanatakiwa kutumiwa
kulingana na wakati, mabomu hayo ni yenye moshi mzito, mwepesi na rangi ambayo
lengo lake ni kuwaweka alama watu watakaokuwa katika kundi linalotakiwa
kudhibitiwa ili waweze kujulikana,” kilibainisha chanzo hicho.
Kwamba
askari wengi wa usalama barabarani siku hiyo walikuwa ni wanawake kwani wale wa
kiume wote walitakiwa kuvaa nguo za Kikosi cha Kuzuia Fujo (FFU).
Habari
hizo zinaongeza kuwa, kutokana na hali hiyo maafisa wa jeshi hilo walilazimika
kutoka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda Iringa kutoa mafunzo kwa askari
wa mkoa huo juu ya matumizi sahihi ya silaha.
Alipoulizwa
kuhusu kukamatwa kwa askari hao wanaotuhumiwa kuua, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Iringa, Michael Kamuhanda, alikataa kuzungumzia suala hilo akisema
limeshaundiwa tume.
“Hizo taarifa mimi sina na
siwezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa limeshaundiwa tume. Tusubiri majibu
yake, lakini hilo la kuja kwa maofisa kwa ajili ya kutupatia mafunzo mimi
sijui, wewe umezipata wapi?” alisema Kamuhanda.
No comments:
Post a Comment