MWENYEKITI
wa Chama Cha Mpinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, bado haamini kama chama
anachokiongoza kimekufa. Badala yake ametoa tambo kuwa wale wote wanaokichulia
kifo, watakufa wao kabla ya chama.
Kikwete
anapima uhai wa CCM kwa kuangalia wingi wa wanachama wanaojitokeza kuwania
nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama bila kujali kama wana sifa stahiki
au hapana.
Kauli
hii ya mwenyekiti ni nzito yenye kuhitaji ushupavu katika kuitamka hasa
unapozungumzia na kusifu kitu dhaifu ukiamini kuwa bado kiko imara.
Pengine
nikuulize wewe unayesoma makala hii, hivi ni kweli Rais Kikwete hajui kuwa CCM
imekufa siku nyingi hasa baada ya yeye kuchukua wadhifa wa mwenyekiti?
Nauliza
hivyo kutokana na utata wa kauli ya Rais Kikwete. Huyu anajaribu kujipa
matumaini ambayo hayapo tena. Kama ni kupima uhai wa CCM kwa sasa ni sawa na
mgonjwa aliyeko mahututi ICU akipumulia mashini yaani nusu mfu.
Kwanini
Kikwete anasema CCM haitakufa wakati imekuta tayari. Hivi anaweza kuifananisha
miiko ya chama kwa sasa na ili ya miaka kadhaa iliyopita. Kweli anaamini
anaongoza chama cha wakulima na wafanyakazi wanyonge?
CCM
aliyorithishwa Kikwete ilikuwa ya wafanyabiashara, mafisadi na uongozi wa
kupokezana kifamilia? Kama si hivyo kwanini mwenyekiti huyo amediriki kuwahadaa
wajumbe wa Kamati Kuu kuwa chama hicho hakitakufa, anataka kife mara ngapi?
Rais
amesahau kuwa hata dhana ya kujitakasa upya aliyoiasisi mwaka jana ya kujivua
gamba imeshindikana kutekelezeka kwa sababu mafisadi aliyokuwa amewalenga
kuwang’oa wamejijengea mizizi kwenye chama kuliko yeye.
Jamani
mwenyekiti huyu anataka tumpe mifano gani zaidi ili atambue kuwa CCM
anayoiongoza imekufa, haina dira, mwelekeo na sasa imeishia kudandia hoja za
wapinzani ndani na nje ya Bunge ikijitapa kuwa zimeasisiwa kwao?
CCM
ya leo ambayo Kikwete bado haamini kama imekufa, ina muundo wa viongozi wasiyo
na dira ya kuwaunganisha wanachama bali kutengeneza makundi ya uchaguzi ujao.
Wakati
wa CCM hai, viongozi wake waliikwepa sana rushwa, walijali uzalendo na maadili
ya taifa, hawakupena madaraka kifamilia, uwazi ulitawala hasa kwenye chaguzi za
ndani na michango ya kuendesha chama. Rais Kikwete anataka kutuambia kuwa CCM
ya sasa iko hivyo?
Leo
CCM ambayo mwenyekiti wake haamini kama imekufa, mkewe anagombea ujumbe wa
Halmashauri Kuu (NEC) kupitia Lindi na mwanaye anagombea kupitia wilayani
Bagamoyo. Hivi ni kweli familia nzima ina wito wa siasa na lazima wote waingie
huko?
Pengine
Rais Kikwete haamini kifo cha CCM kwa vile anaiona bado iko madarakani. Lakini
hakika hicho si kipimo kwani hata uchaguzi ujao wanaweza kushinda. Swali la
msingi hapa ni wamefikaje uongozini, wana mipango endelevu, uwezo wa kusimamia
sera na ilani yao?
CCM
iliyoaminiwa na kuahidi kupambana na rushwa, uhalifu, dawa za kulevya,
umasikini, kuinua wakulima, kusomesha wanafunzi kwa kuboresha sekta ya elimu,
afya, maji safi na salama mjini na vijijini halafu ikashindwa, Kikwete
atasemaje haijafa?
Mwenyekiti
wa CCM anataka maono gani kujua anaongoza chama mfu ikiwa hata uwezo wa wabunge
wake bungeni umekuwa na shaka, kutokana na kupitisha kila kitu kwa makofi na
vigelegele halafu baadaye wanajuta?
Kama
kweli CCM ingekuwa hai kama anavyoamini Rais Kikwete, leo isingekuwa na makundi
ya wabunge hadi ya mawaziri wanaosutana hadharani kwa tuhuma tofauti kwa sababu
tu ya kupigania urais mwaka 2015.
CCM
ingekuwa hai isingesita kuwachukulia hatua mawaziri na wanachama wake
wanaotuhumiwa kwa rushwa na ufisadi, isingehonga mahindi kwenye kampeni za
uchagzu mdogo kama ilivyofanya Igunga, Katibu Mkuu wake na baadhi ya mawaziri
wasingewatisha wapiga kura.
Rais
Kikwete anajua wazi kuwa kwa sasa ili uweze kuwavuta wananchi kuhudhuria
mkutano wa CCM lazima ukodi wanamuziki au vikundi vya uchekeshaji kwaajili ya
kutumbuiza, vinginevyo ni aibu tupu.
CCM
kama ingekuwa imara inatenda yale iliyoahidi bila shaka Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, asingezomewa mkoani Mwanza, badala yake angesomewa risala za pongezi na
kupigiwa makofi. Tafakari!
No comments:
Post a Comment