To Chat with me click here

Friday, September 14, 2012

WAWEKEZAJI WAANZA KUJIONDOA TANZANIA

KUFUNGWA kwa migodi ya dhahabu ya Tulawaka Biharamulo, Resolute ya Nzega, na Barrick kuwa katika mipango ya kuuza zaidi ya hisa zake asilimia 70 kwa makampuni ya madini ya China yaitwayo China National Gold Group, ni ishara kwamba Tanzania itapoteza nafasi yake kama nchi ambayo kwa kipindi cha miaka zaidi ya ishirni, imeweza kuvutia mitaji mikubwa ya kuwekeza katika uchumi wa nchi.

Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita Tanzania imeweza kupokea au kuingiza kwenye uchumi wa nchi vitega uchumi vyenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 433, kiasi kikubwa kimewekezwa kwenye sekta ya madini, sekta ya viwanda, usafirishaji, fedha na mawasiliano. Tanzania imekuwa na sera ya kufungua milango kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kutoka nje. Nchi za Uingereza, Afrika ya Kusini, Canada, Kenya na India zinaongoza kwa kuwekeza vitega uchumi nchini. Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania imenufaika sana na uwekezaji kutokana na kupatikana ajira zipatazo zaidi ya 150,000 za wazi na za kuhudumia miradi.

Hata hivyo uwekezaji nchini Tanzania na katika nchi changa ulipungua sana kutokana na mtikisiko wa uchumi duniani ambao ulitokea kati ya mwaka 2008 na bado unaendelea. Miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na miradi ya uwekezaji ilisimama hapa Tanzania kama vile mradi wa madini ya Nickel wa Kabanga Ngara na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi huko Mtwara ambao ulikuwa utekelezwe na Kampuni ya Artumas ya Canada. Hata hivyo Tanzania ilipita katika kipindi hiki kigumu kutokana na ukweli kwamba uchumi wetu unategemea uchumi wa dunia kwa kiasi na si kikubwa sana.

Sababu nyingine ambazo zimeanza kufanya wawekezaji wapunguze kasi yao kuwekeza Tanzania zinatokana na mpangilio wetu wa ndani hasa kuhusiana na malumbano ya kisiasa na jinsi sera na sheria za uwekezaji zinavyotazamwa na jamii nzima hasa vyama vya siasa na wanasiasa kwa upande mmoja na pia wanaharakati na mashirika ya kutetea haki za binadamu, pamoja na jinsi vyombo vya habari vinavyoandika masuala yanayohusu miradi ya uwekezaji.

Kwa muda wa miaka saba sasa vyombo vya habari, wanasiasa na hata Wabunge, kwa kiasi kikubwa wamechangia kuwaona wawekezaji kutoka nje kama wezi wa mali ya umma na rasilimali za nchi. Mtazamo huo umetokana na jinsi mikataba ya uwekezaji inavyokuwa ya siri, inavyokuwa na vipengele vinavyowapendelea wawekezaji na pia kiasi halisi ambacho nchi inapata kwa kipindi cha muda mfupi ambapo shughuli za uzalishaji au utoaji huduma zinapoanza.

Kwa namna moja au nyingine dhana ya mrahaba haikueleweka. Watu wengi walifikiri malipo ya mrahaba ndiyo malipo nchi inayoyapata kutokana na madini yanayochimbwa. Lakini dhana ya mrahaba ni tofauti na ufahamu wa watu wengi.

Maana ya mrahaba ni kiasi cha thamani ya madini (kati ya asilimia 2 mpaka 10) ambacho nchi inapata kwa ajili ya vizazi vijavyo ambavyo vitakuta madini yamemalizika. Hivyo kiasi hicho siyo malipo kwa madini ya nchi ambapo yanachimbwa bali ni kwa shughuli nyingine.

Kwa upande mwingine madini yana mikataba yake ambayo inatamka wazi masuala ya kodi na malipo mengine. Suala la mikataba ni suala la kitaalamu na uzoefu katika fani hiyo. Kutokana kwamba nchi nyingi hasa nchi changa hazina uzoefu na wataalamu wa kutengeneza mikataba yenye manufaa kwa nchi zao basi mikataba mingi imekuwa ya kinyonyaji na hivyo haileti faida kwa nchi husika.

Mikataba mingi ina vipengele ambavyo vinazifunga nchi zenye madini kutoweza kutumia enzi na haki za kisheria kufanya mabadiliko ambayo yataleta faida kwa pande mbili zinazokabiliana. Hivyo mikataba mingi ya uwekezaji katika madini ni kweli haina faida hasa kwa kuzingatia mapungufu katika miundombinu na pia mapungufu katika utoaji huduma za kitaalamu, kiteknolojia na kifedha.

Manung’uniko ya watu wengi kwa kiasi kikubwa yamewalenga wawekezaji wageni badala ya kutambua kwamba ni Watanzania wenzetu ndiyo wamesababisha misiba na rasilimali ya nchi kuondoshwa bila chochote tunachokipata. Hata hivyo tabia ya Watanzania kutojifunza haraka na kuchangamkia tenda hasa katika maeneo yale ambayo akili, nguvu na uwezo vinahitajika kwa madhumuni ya kudhibiti mazingira imewafanya Watanzania wengi wapende kufanya kazi za uchuuzi badala ya kufanya kazi za kutumia nguvu, akili na mahesabu kwa malengo ya muda mrefu lakini yenye faida kubwa.

Tukichukulia mfano wa nini mahitaji ya huduma katika migodi yetu, ni wazi chakula, huduma za usafiri, huduma za fedha, na huduma nyinginezo ni mambo muhimu ambayo yanagharimiwa kwa kiasi kikubwa cha fedha na makampuni ya migodi. Lakini Watanzania wanalalamika kwamba makampuni ya migodi yanaleta chakula na kutegemea huduma nyingine kutoka nje badala ya kuzipata huduma hizo kutoka ndani ya nchi.

Tukijiuliza kuna makampuni mangapi ya kutoa huduma kwa mahitaji ya makampuni makubwa ya migodi, ni makampuni machache ya watanzania yanayoweza kutoa huduma hiyo na pia kutokana kwamba watu wengi wamezoea kufanyia shughuli zao katika sehemu za mijini, ni makampuni machache yanaweza kuwa tayari kwenda kufanyia kazi huko maporini kwenye migodi.

Tukirejea katika Bunge na kwenye vyombo vya habari, mambo mengi yaliyokuwa yanasemwa na kuandikwa hayakuainisha matatizo ya mfumo na sheria dhidi ya matatizo ya hujuma ambazo zinafanywa na makampuni. Kwa namna moja au nyingine madai ya wizi, ufisadi na serikali kuonekana inashambuliwa kwamba imeshindwa kazi ni mambo ambayo wawekezaji wanayafuatilia sana na yanatabiri bila kuwa na uhakika kwamba Tanzania inawezekana ikakumbwa na machafuko. Kwa upande mwingine Wabunge wamekuwa wakitoa shutuma kali ambazo zinawafanya wawekezaji kutangazwa kama wezi ambao kazi wanayojua kuifanya vizuri ni kuziibia nchi changa kama Tanzania.

Kwa wataalamu wa masuala ya uwekezaji Tanzania ni nchi ambayo imejengewa na taswira kwamba huko mbeleni inaweza ikawa na machafuko. Waliojenga taswira hiyo ni Watanzania wenyewe ambao baadhi yao ni wasomi, wanasiasa na watu wengine walioko katika biashara na menejimenti ya viwanda.

Shirika la Barrick ambalo linaongoza katika uchimbaji madini ya dhahabu kwa kuamua kufunga virago na kuuza migodi yake wakati dhahabu ni madini ambayo thamani yake imepanda sana katika soko la dunia ni wazi kwamba kuna matatizo ya kimkakati ambayo Shirika la Barrick na wawekezaji wengine wamebaini.

Tanzania haina sababu ya kujivunia kuwa na wanasiasa wenye uwezo wa kulumbana. Tanzania tunapaswa kujivunia kuwa na watu wenye uwezo wa kuchambua hali na kutafuta majibu ya matatizo yetu ya ndani na matatizo ya nje. Suala hili la wawekezaji kupunguza kasi yao ya kuwekeza ni suala ambalo lazima tulifanyie kazi na kujua kwa nini yamezuka matatizo.

Toa Maoni yako.

No comments:

Post a Comment