IMEBAINIKA
kuwa mwenendo wa mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi katika mikutano na
maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni mkakati wa
makusudi uliosukwa na watawala ili kukivuruga chama hicho, na kuwatisha
wananchi kwamba ni chama cha fujo.
Hii
si mara ya kwanza kwa watawala kufanya njama hizi dhidi ya wapinzani. Mara ya
mwisho, waliofanyiwa hivyo ni Chama cha Wananchi (CUF), kilipokuwa chama kikuu
cha upinzani.
Njama
hizo zilikiangusha chama hicho, hadi kikajisalimisha kwa kufunga ndoa na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) katika uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, huku
kikipoteza mvuto Tanzania Bara.
Wachambuzi
wa masuala ya kisiasa wameliambia gazeti hili kuwa, CHADEMA inapaswa kuwa macho
na njama hizi, kwani CCM imegundua kwamba inazidi kudhoofika na CHADEMA
kinazidi kuimarika katika jamii; hivyo walio madarakani wanafanya kila njama
kuua wapinzani ili wabaki madarakani.
Siku
chache zilizopita, polisi walimuua kijana Ally Zona wakati wakitawanya waandamanaji
wa CHADEMA mjini Morogoro. Jumapili iliyopita wameua mwandishi wa habari wa
kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi, mkoani Iringa na kuleta sokomoko la
kitaifa, ambalo limelichafua mno Jeshi la Polisi na Tanzania mbele ya jumuiya
ya kimataifa.
Matukio
haya yanatokea wakati ambapo vita ya kisiasa baina ya chama kilichoko
madarakani na CHADEMA ikizidi kuongezeka kutokana na uungwaji mkono mkubwa
unaopata chama hicho cha upinzani kwa sasa kuliko historia ya wakati mwingine
wowote.
Kasi
ya kukua kwa CHADEMA katika miaka ya karibuni inatishia madaraka ya watawala
ambao wamekuwa madarakani kwa miaka ipatayo 50, na ambao chama chao, CCM,
kimepoteza mvuto kwa umma, na hakiaminiki kutokana na kuzongwa na tuhuma nyingi
za ufisadi, na kukumbatia makundi hasimu yanayotafuta madaraka na masilahi
mengine, huku yakiendelea kudhoofisha uongozi wa CCM uliokwisha nyong’onyea.
Wakati
CHADEMA kikipambana kukumbatia mapenzi ya umma unaokiunga mkono, huku
kikifungua misingi na matawi vijijini, CCM inahaha kukidhibiti kwa propaganda
na nguvu za polisi.
Kwa
muda mrefu, CCM imejaribu kukipaka CHADEMA matope ya ukanda, ukabila na udini,
kama ilivyofanya kwa CUF miaka ya nyuma; lakini baada ya kuona mbinu hizo
zimeshindikana, sasa imeamua kutumia jeshi kutisha viongozi wake na wananchi
kwa visingizo mbalimbali.
Hata
hivyo, CHADEMA kinasema kimejiandaa vema kukabililiana na propaganda zote na
vitisho vya watawala; na kwamba kimejifunza kwa makosa waliyofanya wengine
katika NCCR-Mageuzi na CUF.
Mnadhimu
wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki
(CHADEMA), Tundu Lissu, anazo tafsiri tatu za matukio ya mauaji yanayofanywa na
polisi katika mikutano ya CHADEMA.
Anasema:
“Hawana majibu na matatizo ya wananchi, hawana majibu na tatizo la maji, elimu,
matibabu ya uhakika na kero kadha wa kadha zinazowakabili wananchi. Kwa sababu
hawana jibu, wanatumia nguvu. Sasa hawatumii vitisho tu, wanatumia nguvu.
“Hii
ni taswira ya ‘system’ (mfumo) inayojua inaondoka. System imara haitumii nguvu,
inatumia vitisho, kama kupeleka watu mahakamani. Sasa huko tumekwishapita,
tumeingia katika hatua ya kuuawa.”
Tafsiri
ya pili ya Lissu, ambayo ina uhusiano na ile ya kwanza, ni kwamba kwa vile
watawala wanaona wako hatarini kuondoka, wanatafuta namna ya kuwachafua CHADEMA
kwa wananchi ili wawaogope.
“Ikishindikana
kutuchafua kwa propaganda wanaua. Wanaua watu kwenye mikutano na hadharani.
Maana yake ni nini? Ni kwamba wanatuma ujumbe kwa jamii kwamba ukienda kwenye
maandamano ya CHADEMA utakufa. Tafsiri yake ni kwamba watu waogope,” anasema
Lissu.
Tafsiri
yake ya tatu ni kwamba, watawala wanatengeneza mazingira ya kisiasa ili CHADEMA
kionekane chama cha vurugu, ili utafutwe msingi wa kukifutia usajili.
“Ukishafanya
mauaji kwenye mkutano unajenga mazingira ya kusema hiki chama hakina sifa,
unamtengenezea mazingira msajili wa vyama vya siasa akiondoe…ukikiondoa CHADEMA
maana yake umeondoa mgogoro na bungeni…utawaondoa akina Lissu, akina nani kule…
Hivyo, nasema wanatafuta sababu ya kuendelea kutawala kupitia kuua raia,”
anasema Lissu.
Anasisitiza
kwamba kwa mantiki hiyo, Jeshi la Polisi limeacha kazi yao ya msingi ya kulinda
raia na mali zao, na sasa limegeuka jeshi la kulinda walio madarakani ili
waendelee kutawala.
“Jeshi
limegeuzwa chombo cha ulinzi wa watawala. Hilo la kusema kwamba kazi ya Jeshi
la Polisi ni kulinda raia na mali zao ni siasa, lakini the primary function
(kazi yao ya msingi) ambayo hawaisemi ni hii ya kulinda watawala ili waendee
kuwepo,” anasema Lissu.
Aidha,
wachambuzi wanasema kinachotokea sasa ni kwamba watawala wanaanza kuhamanika,
na wanaweza kutumia polisi kutenda mambo ambayo hatima yake itakuwa mbaya kwao,
kama ilivyokuwa kwa watawala wa mataifa mengine waliofikishwa kwenye Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya binadamu, The Hague, Uholanzi.
No comments:
Post a Comment