To Chat with me click here

Friday, September 28, 2012

TAARIFA YA CHADEMA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


KAMATI za Utendaji za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Wilaya ya Nyamagana na Ilemela katika vikao tofauti kwa kushirikiana na kamati za madiwani katika kila wilaya husika, zimekamilisha mchakato wa kupata wagombea wa nafasi za umeya na naibu meya, Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. 

Kamati ya Utendaji ya Wilaya pamoja na madiwani wa CHADEMA Wilaya ya Nyamagana walimteua aliyekuwa Naibu Meya kabla, Diwani wa Kata ya Maina, Charles Chibara kuwa mgombea wa Umeya Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Kwa upande wa Ilemela, kikao cha Kamati ya Utendaji pamoja na madiwani wa wilaya hiyo walimteua Diwani wa Kata ya Nyamanoro, Abubakar Kapera kuwa mgombea wa Umeya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. Kikao hicho cha Utendaji na madiwani wa CHADEMA Wilaya ya Ilemela, pia kilimteua Diwani wa Kirumba, Danny Kahungu kuwa mgombea wa nafasi ya Unaibu Meya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. 

 Vikao hivyo tofauti vya uchaguzi vilivyoketi kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za chama chini ya usimamizi wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, vilihusisha wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Wilaya na madiwani katika eneo husika. Itakumbukwa kuwa katika kutafuta namna bora ya kusimamia vyema utendaji wa chama katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo ilikuwa ni halmashauri pekee nchini iliyokuwa ikihusisha wilaya mbili, yaani Nyamagana na Ilemela, Baraza Kuu la CHADEMA liliamua kuwa masuala yote yanayohusu jiji hilo yasimamiwe na Ofisi ya Katibu Mkuu. Utekelezaji wa maamuzi hayo ya kikatiba, ulianza siku nyingi, ikiwemo kusimamia uchaguzi wa Meya wa Jiji la Mwanza mapema baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010. 

Wakati huo huo Kamati ya Utendaji ya Wilaya Nyamagana imekubali kumwachia kugombea nafasi ya Unaibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Diwani wa Mirongo Daudi Mkama, katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Septemba 28, 2012. Aidha, kutokana na vurugu zilizosababishwa na kundi la watu waliovamia na kuvuruga kikao cha uteuzi wa mgombea wa Umeya na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela hivi karibuni, uongozi wa CHADEMA Wilaya umefungua kesi polisi kwa jalada lenye namba MZN/RB/8226/2012, kwa ajili ya hatua za kisheria.

 Imetolewa jana Septemba 27,  2012, Dar es Salaam; Tumaini Makene Ofisa Habari wa CHADEMA

No comments:

Post a Comment