Mhe. Tundu Lissu |
Wakati Dk. Slaa akiibua tuhuma nzito
kwa Serikali ya Rais Kikwete, zenye kuhitaji majibu stahili, Waziri wake wa
Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, ameshindwa kutolea ufafanuzi hoja
zilizoibuliwa na Lissu kuhusu baadhi ya majaji, aliodai waliteuliwa bila
kufuata utaratibu.
Chikawe ambaye kimsingi ni miongoni mwa
wasaidizi wa Rais Kikwete, anayepaswa kuitetea serikali yake, alipoulizwa juu
ya hoja hiyo aliishia kusema, “hoja za Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, Tundu
Lissu nimezisikia, nimezisoma na sina maoni yoyote juu ya hilo.”
Akizungumza jana, Waziri Chikawe
alisema: “Ungekuja ofisini, nipo safari kwa sasa, hata hivyo hoja za Lissu
nimeziona, nimezisoma na sina ‘comment’ kwa sasa.”
Ni waziri huyo huyo, ambaye aliliambia
Bunge kuwa Tume ya Mahakama inamshauri rais wakati wote na kwamba hakuna
ukiukwaji wowote uliofanyika katika uteuzi wa majaji.
Alisema haijatokea hata siku moja rais
akamteua jaji wa Mahakama Kuu bila kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Uajiri ya
Mahakama.
Awali akijibu hoja za Lissu bungeni,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, ambaye jana simu yake
iliita bila majibu, alimuonya Lissu kuwa ataburuzwa kwenye Kamati ya Maadili ya
Bunge kwa ‘taarifa potofu anazoziwasilisha bungeni’.
Lakini mapema wiki hii, Lissu alirejea
hoja yake na kusisitiza kuwa alishatoa maelezo hayo hata katika Kamati ya Haki,
Kinga na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi.
“Nilieleza jinsi rais alivyofanya uteuzi
wa baadhi ya majaji pasipokupata ushauri wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Wamekuwa wakijibu kiujumla, mimi niliwataja kwa majina yao na hata hili
nilieleza katika Kamati ya Ngwilizi ambayo taarifa yake haikuwekwa hadharani
pasipo sababu za kueleweka,” alisema.
Alipotafutwa jana, Lissu ambaye pia ni
mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, alisema kuwa kwa sasa serikali haiwezi
kusema chochote zaidi ya kukubali, kwani tayari ameshawapa ushahidi kwenye
Kamati ya Bunge.
Alisema hoja yake kuwa kuna ukiukwaji wa
katiba inaungwa mkono na nyaraka za ndani ya serikali na hasa Ofisi ya Rais,
Ikulu yenyewe, ambayo Desemba 6, 2007, mkutano kuhusu ajira ya majaji
waliostaafu ulifanyika Ikulu chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi wakati
huo, Philemon Luhanjo.
Lissu aliongeza kuwa, wajumbe wengine
walikuwa pamoja na Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika na Naibu wake, Sazi
Salula, Katibu Mkuu Utumishi George Yambesi, Msajili wa Mahakama ya Rufani,
Sophia Wambura na Susan Mlawi wa Sekretarieti ya Baraza la Mawazi.
“Serikali iseme suala hili ni la kweli
au si la kweli, na wale niliowataja kuwa hawana sifa kwa mfano ya elimu
serikali iseme wamesoma wapi, na kwanini kulikuwa na kikosi kazi kwa ajili ya
majaji wanaoajiriwa kwa mkataba ikiwa mimi sijasema kweli,” alisema.
Alisema kuwa anazidi kuuliza
inawezekanaje jaji asome shahada ya kwanza ya Sheria Chuo Kikuu Huria sasa,
kwamba aliteuliwaje kuwa jaji, maana hiyo ndio sifa ya msingi?
No comments:
Post a Comment